Wilaya ya Kisarawe, Mkoa wa Pwani imepunguza idadi ya vifo vya kina mama wajawazito kutoka vifo 9 hadi 1 kwa mwaka.

Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Kisarawe, Glason Mlamba, amesema mafanikio hayo yamepatikana baada ya kuona vifo vinaongezeka, wakaanza kufikiria namna ya kupunguza vifo hivyo.

Mlamba amesema waliamua kuunda kikundi kupitia mtandao wa kijamii wa WhatsApp ambao umewaunganisha madaktari na wauguzi kuanzia chini hadi ngazi ya wilaya.

Baada ya kuunda kundi hilo, Mlamba amesema walianza kupeana taarifa za mara kwa mara za hali za wajawazito kuanzia ngazi ya zahanati hadi hospitali ya wilaya ili kujua namna ya kutatua changamoto za wajawazito waliopo katika vituo hivyo.

“Kundi hilo la WhatsApp lilikuwa likisaidia sana kuwatambua haraka kina mama wenye viashiria vya hatari, daktari au mkunga anachotakiwa kufanya ni  kutoa taarifa haraka kwa wana kundi wakati huo, hapo hapo tunashirikiana kutoa ushauri wa haraka ili kuokoa maisha ya mzazi mwenye viashiria hatarishi kabla ya madhara zaidi,” amesema Mlamba.

Mbali na kuunda kundi hilo, amesema wameweka vifaa vyote vya msingi katika vituo vya afya na zahanati, lengo likiwa ni kukabiliana na dharura yoyote itakayotokea kwa mjamzito.

Mlamba ameliambia Gazeti la JAMHURI kwamba wana mkakati wa kuanzisha huduma ya upasuaji katika vituo vyote vya afya ili kuboresha zaidi na kuzuia kabisa vifo vinavyotokana na kujifungua.

Mtaalamu wa afya ya uzazi, Alex Nyaruchary na mwanzilishi wa kundi hilo, amesema baada ya kufanya kazi katika wilaya hiyo kwa miaka 12, aligundua kuna changamoto ya kuzuia vifo vya wajawazito, maana vilikuwa vinaongezeka kila mwaka.

Nyaruchary ameliambia JAMHURI kwamba mwaka 2018 baada ya kuguswa na vifo hivyo alianzisha kundi hilo la WhatsApp, sambamba na mafunzo ya mara kwa mara kwa watumishi.

Amesema wakati wanaanzisha mtandao huo wa kuwaokoa kina mama wajawazito kulikuwa na jumla ya wanawake 1,947 waliokuwa na viashiria vya hatari, ambapo kufikia Julai mwaka huu wajawazito 1,007 wamegundulika kuwa na viashiria vya hatari.

Takwimu hizo ni za kipindi cha Juni 2017 hadi Juni 2018, ambavyo zinaonyesha kulikuwa na vifo 17. Baada ya kuunda mtandao na kufanya kazi kwa pamoja kwa kutumia kundi hilo, vifo hivyo vimepungua hadi kufikia kifo kimoja kwa mwaka huu.

Anazitaja sababu kuu tatu zilizochangia tatizo la vifo kwa wajawazito kuwa ni kushindwa kuwahi kliniki pindi wanapojigundua ni wajawazito, kushindwa kuwa na ufuatiliaji wa karibu kwa njia ya kwenda kliniki pamoja na kushindwa kuzitambua dalili za hatari zinapowakabili.

Amesema kina mama wajawazito wamekuwa wakichelewa kwenda hospitali wanapoambiwa wana matatizo ya uzazi, hali inayosababisha zahanati na vituo vya afya kushindwa kuokoa maisha ya baadhi ya wajawazito.

“Wakunga wengi wa wilaya yetu wana uwezo mdogo wa kutambua magonjwa ya dharura ya uzazi, inapotokea dharura wanashindwa kuikabili, na mara nyingi wanapoletwa hospitalini hali inakuwa mbaya zaidi, hivyo baadhi tunashindwa kuokoa maisha yao,” amesema  Nyaruchary.

Elizabeth Maiko (44), mkazi wa Kijiji cha Kauzeni amesema wakati wa ujauzito alikuwa akiumwa kichwa lakini baada ya kupelekwa kituo cha afya aligundulika kuwa na tatizo la shinikizo la damu isiyoshuka, lakini kwa msaada wa madaktari alijifungua salama.

Ofisa Muuguzi Mkuu wa Kituo cha Afya Masaki wilayani humo, Vincent Gaya, amesema mtandao huo umewawezesha kuondoa kabisa vifo vya kina mama wajawazito katika kituo hicho.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Guninyi Kamba, amesema Wilaya ya Kisarawe imepiga hatua kubwa katika kupunguza vifo vya kina mama.

Kamba amesema wilaya hiyo imekuwa msitari wa mbele katika uandikishaji wa mfuko wa bima ya afya iliyoboreshwa. Ameliambia JAMHURI kuwa mpaka sasa takwimu zinaonyesha Wilaya ya Kisarawe inafungana na Wilaya ya Mafia kwa kuwa na kifo kimoja, ikifuatiwa na Mkuranga yenye vifo 2, Bagamoyo 4, Rufiji 4 na Chalinze yenye vifo 4.

Ameongeza kuwa wilaya nyingine ni Kibiti yenye vifo 6 huku Hospitali ya Mkoa wa Pwani ikiwa na vifo 11.

Amezitaja mimba za utotoni kuchangia vifo vya kina mama wajawazito kwa kiasi kikubwa, kwani idadi ya wasichana wanaobeba mimba huwa katika umri mdogo usiofaa kubeba mimba na kujifungua.

Ameitaja changamoto nyingine kwamba ni pamoja na wajawazito kutofika kwa wakati katika vituo vya afya, huku wengine wakiishi umbali mrefu kutoka vilipo vituo vya afya.

Ameongeza kuwa kwa sasa wana mkakati wa kuongeza wataalamu zaidi hasa wa dawa za usingizi pamoja na kuongeza idadi ya vituo vya afya katika Mkoa wa Pwani.

Ili kuboresha afya za wananchi wa Pwani, amesema wanatakiwa kujiunga katika bima za afya ili wasipate shida ya kupata matibabu wanapofika kwenye vituo vya afya na zahanati.