Baada ya Morocco kutinga hatua ya nusu fainali ya Kombe la Dunia nchini Qatar kumeubuka hisia mbalimbali miongoni mwa mashabiki na makocha wa timu mbalimbali kuhusu namna ya kuziandaa timu zao za taifa kuelekea mafanikio.
Huko Afrika Kusini kocha wa Chippa United, Morgan Mammila, amenukuliwa akisema, “tusione aibu kuwaiga wa Morocco.” Kocha huyo wa Chippa anakocheza beki mtanzania Abdi Banda amesema iko wazi kwamba ili timu ipate mafanikio inahitaji kocha mzawa na kijana na sio kocha mzee kama Hugo Broos ambaye anainoa timu yao ya taifa ya Afrika Kusini.
Morgan amesema sio tu Afrika Kusini bali nchi zote za Afrika zinatakiwa kuchukua makocha wazawa na vijana na sio kutegemea makocha wa nje ambao hawana jipya kimbinu na hawajui namna ya kukaa na wachezaji wetu wa kiafrika.
“Kocha mwenye umri wa miaka 70 anatakiwa kuwa nyumbani na sio kufundisha mpira,” Morgan amesema hayo akionesha moja kwa moja kumlenga kocha wa timu yao ya taifa ‘Bafana Bafana’ Hugo Henri Broos raia wa Ubelgiji mwenye umri wa miaka 70.
Morgan Mammila ameshauri chama cha soka nchini Afrika Kusini [SAFA] kumrejesha nyumbani kocha Pitso Mosimane ili ainoe timu ya taifa hilo Kwa mtazamo kwamba Morocco wamefanikiwa kwa kumuamini kocha mzawa na kijana Walid Regragui mwenye umri wa miaka 47 tu.