Ligi Kuu ya soka Tanzania Bara maarufu kama Ligi ya Vodacom, inazidi kushika kasi. Moja na vitu ambavyo vimeongeza chachu katika ligi ya msimu huu ni jinsi baadhi ya timu zilizopanda msimu huu zinavyoleta upinzani kwa vigogo wa soka hapa nchini.

Timu ambazo tayari zimeonekana kuwa mwiba mkali kwa vigogo vya soka — Simba na Yanga — ni Mbeya City, Rhino Rangers ya Tabora, Coastal Union ya Tanga na Kagera Sugar ya Bukoba.

 

Wakati timu hizi zikionesha upinzani wa hali ya juu, Ashanti United ya jijini Dar es Salaam ambayo pia imepanda Ligi Kuu msimu uliopita, imejikuta katika wakati mgumu kwani hadi sasa inashika mkia katika msimamo wa ligi.

 

Katika mechi ya fungua dimba, Ashanti walijikuta wakipata kipigo cha magoli 5-1 kutoka kwa mabingwa watetezi wa ligi hiyo, Yanga. Baada ya mechi na katika hali ya kujitetea, aliyekuwa kocha wa timu hiyo ambaye kwa sasa ameachia ngazi, Hassan Banyai, alisema kuwa timu yake imefungwa kutokana na wachezaji wake kuogopa majina, na kwamba imecheza na timu kubwa huku akiahidi kwamba timu hiyo ingeweza kufanya vizuri katika michezo iliyofuata.

 

Hata hivyo, kocha huyo aliamua kuachia ngazi baada ya kuona timu yake inaendelea kuboronga katika ligi hiyo. Huu ulikuwa mwanzo mbaya katika ligi, hasa pale kocha anapoamua kuachia ngazi badala ya kupendekeza kipi kifanyike anapoona timu yake inafanya vibaya. Mashabiki wa Ashanti bado wana imani kwamba endapo timu yao itafanya usajili mzuri katika dirisha dogo, bado ina nafasi kubwa ya kufanya vizuri na kujinusuru kushuka daraja.

 

Baadhi ya mashabiki na wachezaji waliopata kuichezea timu hiyo na wengine kuwa viongozi, wameonesha hisia zao dhidi ya mwenendo wa timu hiyo. Jambo kubwa linalosemwa kwa sasa ni usajili mbovu wa timu hiyo ambao umesajili wachezaji bila kuzingatia viwango vya wachezaji  wanaoweza kumudu mikikimikiki ya soka la sasa, ambalo limejaa vijana wenye damu changa.

 

Mashabiki wa Ashanti wanaiona timu yao kuwa ina wachezaji wachache wenye uwezo wa kusakata kabumbu kwa sasa. Wengi wao wanachukuliwa kama wakongwe ambao kwa namna moja ama nyingine wameishiwa mbinu za kucheza mpira kwa sasa na hivyo kukubali matokeo ya kufungwa kila mara.

 

“Hivi kaka kama unakumbuka Ashanti ya mwaka 2005 iliyowatoa wachezaji kama vile Juma Nyoso, Ramadhani Redondo na wengine wengi utaweza kuilinganisha na Ashanti ya sasa hivi ambayo imesajili wachezaji wazee?” Alihoji mmoja wa mashabiki wa timu hiyo ambaye pia alipata kuwa mmoja wa viongozi wa ngazi ya juu za timu hiyo.

 

Anaendelea kusema; “Unajua mimi sitaki kutaja jina langu kwa sababu kuna wengine watafikiri labda mimi nataka uongozi  katika timu hiyo, nilishawahi kuiongoza timu hiyo na nimewahi kuichezea pia timu hiyo, ninakumbuka jinsi ilivyokuwa Ashanti ya ukweli. “Ninachoongelea hapa ni aibu tunayoipata kwa sababu mimi bado naipenda timu hiyo,” amesema.

 

Aidha, shabiki huyo ameongeza kuwa kitendo cha kuwasajili wachezaji wakongwe ambao kwa sasa wamechoka kisoka katika timu hiyo, kimedhihirisha kwamba timu hiyo imekosa mipango thabiti na badala yake kukumbatia mambo ya kikabila.

 

“Hivi kama viongozi wa timu hiyo wanatokea Kigoma lazima wachezaji wote watokee Kigoma? Hatukatai, basi kama ni hivyo watafuteni damu changa kuliko hawa wazee ambao wakikimbizwa kidogo wako hoi. Bila kufanya marekebisho wakati wa dirisha dogo nakwambia ukweli Ashanti inashuka tena msimu huu,” amesema mkereketwa huyo.

 

Mkereketwa huyo alikwenda mbali zaidi na kusema kuwa kumekuwa na tabia ya baadhi ya watu kujipendekeza kwa uongozi wa juu wa timu hiyo bila kutoa mawazo ya kujenga, badala yake ni majungu ambayo alisema kuwa na yenyewe yanachangia timu hiyo kurudi nyuma.

 

Hivi karibuni, kiongozi wa juu wa timu ya Ashanti amekaririwa na vyombo vya habari akisema kwamba uongozi wa klabu hiyo utafumua kikosi hicho kwa kuwa ni kibovu na kufanya usajili wakati wa dirisha dogo Januari, mwakani.

 

Kwa mujibu wa kiongozi huyo, lengo la usajili mpya wakati wa usajili wa dirisha dogo ni kuhakikisha kuwa timu hiyo inaweza kuhimili vishindo vya ligi ya msimu huu. Kiongozi huyo anakiri kuwa timu hiyo imeshindwa kuhimili mikikimikiki ya ligi kutokana na viwango vya wachezaji kutokuwa na ubora unaoendana na soka la kisasa.

 

0783 106 700