Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma

MKURUGENZI Mtendaji wa Kituo cha Kuendeleza Kilimo Nyanda ya Juu Kusini mwa Tanzania ( SAGCOT), Bw.Geoffrey Kirenga amesema mafanikio yaliyopatikana katika Ukanda huo kiuwekezaji kwenye kilimo yametokana na ushirikiano wa pamoja kati ya serikali na sekta binafsi na kufikia uwekezaji wa pamoja wa takriban bilioni 3.8 katika mipango yake ya kuendeleza kilimo hapa nchini.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa ukanda mpya wa kuendeleza kilimo katika kanda tatu (ACGOT) ulioanzishwa kutokana na mafanikio ya SAGCOT, Bw Kirenga amemueleza Rais Samia Suluhu Hassan kuwa serikali peke yake iliwekeza bilioni 2.5 katika maeneo mbalimbali ya miundombinu ikiwemo barabara na umeme, huku kiasi kingine cha bilioni 1.3 ikiwa ni mchango wa sekta binafsi.

Mkurugenzi wa Kituo cha Kuendeleza Kilimo Nyanda za Juu Kusini (SAGCOT), Bw Geoffrey Kirenga (kushoto) akimuelezea Rais Samia Suluhu Hassan namna Taasisi hiyo inavyofanya kazi ya kuwainua wakulima wadogo na wa kati , pia kuwaunganisha wakulima wakubwa ili kuyafikia masoko, kabla Rais hajazindua rasmi Benki ya Ushirika juzi jijini Dodoma. Katikati ni Waziri wa Kilimo Bw Hussein Bashe.

“Ubia huu umekuwa na tija sana katika kukuza kilimo katika Ukanda wa nyannda ya juu kusini,”alisema Bw kirenga na kuishukuru Wizara za Kilimo na Mifugo kwa msaada na ushirikiano.

“ Kilichovutia ushiriki wa sekta binafsi ni ushirikiano wa viongozi wa mikoa, wilaya hadi vijini na uzoefu huu sasa tunauepeleka katika maeneo mengine ya kanda mpya zilizoanzishwa kwa ajili ya kuendeleza kilimo hapa nchini,” amesema Bw Kirenga.

Kwa mujibu wa mkurugenzi mtendaji huyo, uanzishwaji wa shoroba nyingine za kilimo umetokana na maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan katika kuendeleza sekta ya kilimo hapa nchini.

“Kwa kupitia ushirikiano huu, tumeweza kupata mafanikio makubwa ikiwa ni pamoja na uzalishaji wa maziwa ya unga baada ya wakulima na wafugaji wa ndani kuwezeshwa rasilimali fedha na utaalamu,” aliongeza Bw.Kirenga.

Akielezea moja ya mafanikio ya SAGCOT, Waziri wa Kilimo, Bw Hussein Bashe amesema umetokana na mafanikio ya mradi wa Jenga Kesho iliyo Bora (BBT) unaowezesha vijana mitaji ya kuwekeza katika kilimo.

Waziri Bashe amesema kuwa mmoja wa wanufaika wa mradi huo ni msichana aitwaye Raya, ambaye alipewa mkopo wa milioni 20 uliomsaidia kuongeza ukubwa wa shamba lake na hivi sasa ameweza kuajiri takriban vijana 20 na kufanikiwa kulipa mkopo huo kutoka mfuko wa pembejeo.

“ Tulimsaidia Raya kupata kiasi hicho cha fedha na amefanikiwa kurejesha kiasi chote cha fedha na hivi sasa ameomba milioni 100 ili kuendeleza kilimo chake,” Waziri Bashe amemueleza Rais Samia na kuongzea;.

“Kwa hiyo tumemuomba Kirenga, baada ya kufanya vizuri kwenye SAGCOT, yeye atakuwa mratibu katika shoroba hii mpya kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo “ (TARI) chini ya Mratibu wa Kilimo,”

“ Na tumeamua kufanya hivi ili kufuata mchakato na kama tungeamua kuishirikisha SAGCOT peke yake basi ingeleta maswali kwa Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) kuwa tumekiuka utaratibu;” Waziri Bashe alimwambia Rais Samia.

Amesema kuwa kutokana na ukubwa wa shoroba hiyo, Serikali inatekeleza maagizo ya Rais ya kuhakikisha maji kutoka Ziwa Victoria yanapita mkoani Dodoma na tayari tenda kwa ajili ya upembuzi yakinifu imeshatangazwa.

Ukanda wa Kusini mwa Tanzania (SAGCOT) umekuwa mfano wa kuigwa katika maendeleo ya kilimo hapa nchini na kupelekea kuanzishwa kwa Mpango wa Kukuza Kilimo nchini ( AGCOT) wenye lengo la kukuza kilimo hapa nchini kwa kuanzisha kanda (shoroba) nyingine tatu za kilimo ili kuongeza tija kwa wakulima hapa nchini.

Ukanda huo wa Kusini ambao umepata mafanikio chini ya usimamizi wa SAGCOT unajumuisha mikoa ya Morogoro, Iringa, Njombe, Mbeya, Songwe, Rukwa, Katavi, Dar es Salaam na Pwani.