Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia,Mkuranga

Zaidi ya sh.milioni 7.3 zinahitajika kwa ajili ya kumalizia mradi wa ujenzi ofisi ya Kata ya Kiparang’anda Mkoa was Pwani.

Akizungumza na wadau wa maendeleo katika kikao maalum cha maendeleo,Diwani wa kata hiyo, Shomari Mwambala ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti Halmashauri ya Mkuranga, amesema, ni wakati sasa kwa wadau kujitokeza kuchagiza maendeleo ili kata hiyo iibuke kidedea kwenye sekta mbalimbali.

Amesema lengo hilo haliwezi kufikiwa endapo wadau watakaa pembeni na kuwaachia viongozi peke yao hivyo ni muhimu kujenga ushirikiano baina ya pande zote hizo ambao utasaidia kuondoa changamoto zilizopo.

Pia amesema tayari wapo kwenye mchakato wa kuboresha miundombinu ya shule ndani ya kata hiyo ili kuongeza
ufaulu wa wanafunzi na hatimaye kufikia lengo la Serikali.

Diwani wa Kata ya Kiparang’anda, Shomari Mwambala, ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga, akizungumza na wadau wa maendeleo katika kikao maalum cha maendeleo kilichofanyika jana wilayani humo. 

Ameongeza kuwa ili kufikia malengo hayo ni vema wadau wa maendeleo ndani ya kata hiyo wakajitokeza kushiriki shughuli
za maendeleo lengo ikiwa ni pamoja na kujenga kata iwe bora ya mfano na itasaidia kukuza ushirikiano wa kimaendeleo.

“Wapo baadhi ya wadau wanafanya shughuli zao za maendeleo ndani ya kata hii lakini baadhi yao wanajivuta kuchangia maendeleo hivyo ni muhimu wakajitafakari vinginevyo hatua za kisheria zitaanza kuchukuliwa,” amesema Mwambala.

Mwambala amesema fedha nyingi za mikopo ndani ya halmashauri hiyo huwa zinarejeshwa Serikali Kuu kwa sababu waombaji wengi wanashindwa kutimiza masharti.

Hata hivyo amewataka waombaji mikopo kutafakari aina nyingine ya miradi kwa kuwa waombaji wengi wamekuwa wakinunua bodaboda ambazo zimekuwa zikisababisha athari ndani ya familia nyingi kuachwa yatima au ulemavu wa kudumu.

Akizungumzia kuhusu awamu ya pili ya unganishwaji umeme ndani ya kata hiyo amesema unatarajiwa kuanza hivi karibuni ambapo tayari wataalam wamekwishafanya ukaguzi wa maeneo yatakayopitishwa umeme.

Awali bajeti za halmashauri iliyopita ilikuwa ni kuendeleza kata zake ambapo fedha hizo hazikutosheleza kumaliza miundombinu ya ofisi hiyo.

” Bajeti ya mwaka huu haina ofisi ya maboresho ya kata…iliyopo imelenga zaidi kwa kata ambazo hazina majengo,” amesema.

Please follow and like us:
Pin Share