Rais wa Uganda Yoweri Museveni mwenye umri wa miaka 80 ametetea matumizi ya mahakama za kijeshi kuwashitaki raia, kufuatia malalamiko ya kukamatwa na kushtakiwa kwa kiongozi wa upinzani Kizza Besigye.
Besigye mwenye umri wa miaka 68 ameshtakiwa katika mahakama ya kijeshi kwa kumiliki bastola na kujaribu kununua silaha nje ya nchi, madai ambayo anayakanusha.
Besigye, ambaye alitekwa nyara wakati alipozuru Kenya mwezi uliopita na kupelekwa Uganda kwa nguvu, aligundua Jumanne kwamba atasherehekea Krismasi akiwa kizuizini kwa kuwa kesi yake imeahirishwa hadi mwezi Januari.
Museveni alisema uhalifu wowote unaohusisha bunduki unashughulikiwa katika mahakama ya kijeshi ili kuhakikisha utulivu wa nchi hiyo kwa kuwa mahakama za kiraia zinachukua muda mrefu kushughulikia kesi.
Mamia ya raia wameshtakiwa katika mahakama za kijeshi nchini Uganda, licha ya kwamba mahakama ya katiba imetoa uamuzi dhidi ya kuendeshwa kwa kesi za raia katika mahakama za kijeshi.
“Nimeona hoja katika makaratasi ya baadhi ya wanasheria kuhusu usahihi wa baadhi ya raia kufikishwa katika mahakama ya kijeshi,” Rais Museveni alisema katika ujumbe mrefu wa X.
Alisema chama chake cha National Resistance Movement (NRM) kilitunga sheria kupitia bunge mwaka 2005 kuruhusu matumizi ya mahakama za kijeshi kwasababu ya “shughuli za uhalifu na magaidi ambazo zilihusisha matumizi ya bunduki kuua watu kiholela’’.
Besigye amepinga kushtakiwa na mahakama akisema kuwa kama kuna mashtaka yoyote dhidi yake, anapaswa kushtakiwa katika mahakama ya kiraia.