Hivi karibuni, gazeti la JAMHURI limefanya mahojiano na Amri Athumani, anayejulikana pia kama King Majuto. King Majuto amekuwa mwigizaji wa vichekesho kwa miaka 55 iliyopita. Mtanzania huyu mwenye umri wa miaka 65 anajivunia tasnia ya uigizaji, ila anaomba Serikali imsaidie trekta aweze kushiriki Kilimo Kwanza.
King Majuto ameshiriki kwa kiasi kikubwa katika shughuli za kijamii kupitia vipindi vya redio, televisheni na sinema ambazo anaonekana, kushiriki kujenga jamii iliyo salama, utawala bora, heshima kwa binadamu na maisha mazuri kwa wote. Pata uhondo…
JAMHURI: Lini ulianza kuigiza?
King Majuto: Nilianza kuigiza mwaka 1958 nikiwa na umri wa miaka 10. Nakumbuka nilikuwa katika Shule ya Msingi ya Msembweni miaka 55 iliyopita, ambapo mlevi mmoja alikuwa anapita karibu na shule yetu huku akipiga ngoma kwa nguvu huko nje.
Mtoto mmoja alitoka darasani akaenda akajiunga na mlevi yule kucheza ngoma kwa sababu yule mtu alikuwa anapiga mdundo mzuri. Mwalimu wetu alikasirika na kumtuma mwanafunzi mwingine kumfukuza yule mlevi. Badala ya kumfukuza, mwanafunzi yule naye akajiunga na ngoma.
Mimi nilikuwa darasa la pili. Mwalimu wetu akatoka nje ya darasa kwa kishindo kwenda kumfukuza yule mlevi. Sote tulikuwa kimya huku tunamwangalia mwalimu wetu kupitia dirishani. Mwalimu alipomkaribia [yule mtu], akaanza kutingisha mabega yake kufuatisha mdundo. Kwa mshangao, badala ya kumfukuza mlevi, Mwalimu naye akajiunga na ngoma… baada ya muda mfupi, shule nzima ilikuwa inacheza ngoma.
JAMHURI: Iliishia vipi?
King Majuto: Baada ya saa moja au zaidi ya kucheza ngoma, Mwalimu alimshukuru mlevi na kuwambia wanafunzi umuhimu wa burudani kama kitu cha kuunganisha watu, zana ya kutunza utamaduni na kutunza historia. Kuanzia wakati huo, niliamua kuwa kazi [ya sanaa] inaendana na maslahi yangu. Nikaanza kuifanyia mazoezi, na kujiunga na kwaya ya shule.
JAMHURI: Nini kilifuatia baada ya masomo yako?
King Majuto: Mwaka 1966 nilimaliza darasa la nane. Mwaka mmoja baadaye, nilijiunga na Jeshi la Kujenga Taifa. Tulikuwa tunalipwa shilingi 20. Nilibakia kule kama askari hadi mwaka 1970, lakini mmoja wa viongozi wetu alikuwa ananikera sana. Kila nilipokuwa ninatunga nyimbo au kichekesho, alikuwa ananisumbua. Nikaliona jeshi la kujenga taifa [kuwa] si bandari ya salama kwangu, kwa hivyo nikaacha kazi.
[Baada ya kufanya kazi kadhaa], mwaka 1976 niliamua kujishughulisha na kazi ya sanaa muda wote. Baada ya hapo, nikaanza kujiingizia hadi shilingi 6,000 kwa mwezi kutokana na kuimba na kuigiza, na nikamudu kujenga nyumba yangu ya kwanza.
Mwaka 1983 nikajiunga na Bendi ya DDC Kibisa ya Dar es Salaam, na mwaka 1985 nikajiunga na Bendi ya Muungano Cultural Troup.
JAMHURI: Tuelezee kuhusu Muungano Cultural Troup.
King Majuto: Tulikuwa tunatengeneza filamu, wakaniteua kuwa Mkuu wa Idara ya Sinema, ambayo ilikuwa inashughulika na filamu na vichekesho ambavyo vilikuwa vinakuza Umoja wa Afrika.
Kile tulichokuwa tunatetea kikawa kweli. Tulikuwa tunaomba uwepo Umoja wa Afrika, na sasa tunao Umoja wa Afrika. Hii ni moja ya michango mikubwa kabisa kwa Umoja wa Afrika kupitia sanaa yangu.
JAMHURI: Ni katika kampeni gani nyingine ulishiriki?
King Majuto: Nimecheza sehemu ya filamu dhidi ya mauaji ya albino. Katika miaka mitatu iliyopita, nchi yetu imekumbwa na wimbi la mauaji ya kiasi cha albino 57 waliuliwa kutokana na imani za kishirikina kwamba kiungo chochote au mfupa wa albino unaweza kumfanya mtu awe tajiri.
Mwaka 2010 nilianzisha kampeni kubwa katika Mikoa ya Kanda ya Ziwa (Mwanza, Kagera, Kigoma, Shinyanga na Mara) kuhusu suala hili na naamini ujumbe wetu ulieleweka. Mauaji ya albino yamesita. Ujumbe wangu kupitia filamu na vichekesho vifupi ulikua wazi. Ulisema, “huwezi kuwa tajiri kwa kuwaua albino”. Ilikuwa kampeni ya miezi sita na ilifanikiwa.
JAMHURI: Sanaa inawezaje kuleta mabadiliko Tanzania?
King Majuto: Bila sanaa katika nchi hii umoja wetu ungekuwa umeharibiwa muda mrefu. Naendelea kuwakumbusha Watanzania kuwa umoja wetu, amani na utulivu lazima vibakie kuwa kipaumbele chetu cha kwanza. Naweza kusema kwa kujiamini kuwa filamu na vichekesho vyangu vimesaidia kuiunganisha Tanzania kwa muda wote.
JAMHURI: Je, ungepewa fursa ya kuchagua jambo lolote katika fani yako, ungechagua ufanyiwe nini?
King Majuto: Chaguo langu litashangaza wengi. Katika umri huu, napungukiwa nguvu. Kuigiza kunahitaji nguvu na kukimbia hapa na pale, basi nasema ingewezekana naomba nipatiwe trekta. Nikiapata trekta nitashiriki kwa vitendo Sera ya Kilimo Kwanza.