Msanii maarufu wa maigizo ya runinga nchini, Amri Athumani (65), maarufu King Majuto amealikwa nchini Rwanda.

King Majuto (pichani) amealikwa na Serikali ya Rwanda kwenda kukabidhi zawadi kwa wasanii bora wa mwaka nchini humo.


Akizungumza na JAMHURI mwishoni mwa wiki, King Majuto alisema amepata fursa hiyo baada ya Wanyarwanda kushuhudia kazi zake kupitia runinga mbalimbali za ndani na nje ya nchi na kuzikubali.


“Ndo hivyo mwanangu kesho (Jumamosi Machi 9) nakwea pipa na kutua Kigali. Tiketi ninayo mkononi, nimekubalika sasa nakwenda kuwakabidhi zawadi wasanii wa huko. Jitahidi unicheki kwenye runinga,” ameliambia JAMHURI.


King Majuto, aliishukuru Rwanda kuwajali wasanii wa Tanzania na kusema kuwa akiwa Rwanda atalitangaza jina la Tanzania. Amesema katika ziara hiyo anaongozana na Ray, JB na Irene Uwoya.