*Asafishwa biashara ya meno ya tembo

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emanuel Nchimbi, amemtetea Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana, akisema kampuni yake ya utoaji huduma melini, haikuhusika na usafirishaji meno ya tembo kwenda ughaibuni.

Katika hali ambayo ni nadra kutokea bungeni, Spika Anne Makinda alimpa Nchimbi nafasi ya kuchangia baada ya Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Peter Msigwa, kumaliza kuwasilisha hotuba yake.

 

Kwenye hotuba hiyo, Msigwa aliwashambulia makada kadhaa wa CCM, akiwamo Kinana, akisema wanashiriki ujangili kwa kuua tembo na kusafirisha meno nje ya nchi. Kada mwingine aliyeguswa ni Mohsin Abdallah (Shein).

 

Katika kujibu mapigo, Dk. Nchimbi alisema Kinana hakusiki na ujangili, na kwamba kampuni inayopaswa kulaumiwa ni ile iliyojihusisha na uwakala wa kupeleka na kupokea (clearing and forwarding).

 

“Kampuni ya Mheshimiwa Kinana ni ya shipping agency-inajihusisha na kazi ndogo ndogo za kuhudumia vyakula melini, usafi na mahitaji mengine muhimu. Kazi za kampuni ya clearing and forwarding ni tofauti. Chadema wanajua, Mheshimiwa Msigwa anajua, lakini wameamua kupotosha umma wa Watanzania. Mtu wa shipping agency hahusiki na upekuzi wa mizigo. Kuna uvumi wa makusudi kuwa Kinana anamiliki meli. Ni uzushi,” alisema.

 

Alisema watuhumiwa wote wa shehena iliyokamatwa walifunguliwa kesi ya uhujumu uchumi namba 3&4 ya mwaka 2009. Aliwataja watuhumiwa walioshitakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa ni Eradius Tesha, Gabriel Chambo, Shaaban Yasin, Erick Kileo, Issa Athuman, Nerbat Kiwele na Abubakar Hassan.

 

Alisema watuhumiwa hao waliachiwa kutokana na kukosa ushirikiano kutoka Serikali ya Vietnam ambako meno yalikamatwa. Tanzania na Serikali ya nchi hiyo hazina mkataba wa kuziwezesha kushirikiana kwenye masuala kama hayo.

 

Dk. Nchimbi alisema kwa sasa juhudi zinaendelea kwa kuushirikisha ubalozi wa Tanzania nchini China ili kupata ushirikiano kutoka Vietnam . “Kesi iliondolewa, ushahidi ukipatikana itarejeshwa mahakamani.

 

“Upinzani si siasa za matope, kuchafuana, uongo, uzushi au kutoa kucha watu na siasa za kuchafuana. Mheshimiwa Spika, Bunge lako likatae. Haya ni maono mafupi. Hivi leo tukiwakabidhi Serikali itakuwaje? Mimi ni Mkristo, Biblia inasema bora mchawi kuliko mwongo. Genge la waongo husababisha maafa zaidi ya mchawi. Chama hiki kilianza kusifiwa. Baba wa Taifa alikisifu, lakini leo Mwalimu angekuwapo angesema Chadema haiji vizuri.

 

“Msigwa amwombe radhi Kinana. Yeye ni Mchungaji, aliombee Taifa liende mbele. Aombee Kambi ya Upinzani itoke mapepo,” alisema Dk. Nchimbi.

 

Telele asubiri Waziri Mkuu

Mbunge wa Ngorongoro, Aika Telele (CCM), amesema mgogoro kati ya wananchi na Serikali katika eneo la Loliondo, sasa unastahili kupatiwa suluhu ya kudumu.

 

Amesema tume mbalimbali zilizoundwa hazijafikia hatua ya kutoa suluhu ya mgogoro huo, na kuongeza kuwa sasa Waziri Mkuu Mizengo Pinda, anapaswa kusimama kuumaliza.

 

Alisema hakuna kiongozi wa CCM Ngorongoro anayetaka kujiuzulu, bali viongozi hao, akiwamo yeye, wataendelea kusimama kidete kuhakikisha suala la Loliondo linazungumzwa na kupatiwa ufumbuzi wa kudumu.

 

“Baada ya Mungu, ni Serikali. Naamini Serikali ya CCM itamaliza tatizo hili. Waziri Mkuu suala hili ulitolee tamko. Bunge hili halijawahi kuunda Tume au Kamati na ilete taarifa ya Loliondo…zinachukua fedha na muda. Serikali ya CCM haijashindwa kumaliza tatizo hili,” alisema Telele.

 

Shelukindo aipongeza TANAPA

Kwa upande wake, Mbunge wa Kilindi, Beatrice Shelukindo (CCM) akichangia hotuba ya Waziri Kagasheki, aliipongeza TANAPA kwa kupeleka miradi mingi ya kijamii katika jimbo lake.

 

Katika hatua nyingine, alimtetea Kinana kwa kusema asingekuwa Katibu Mkuu wa CCM, asingesemwa.

 

“Hapa ndani hatuji kushindana. Hapa ndani tunaongelea wananchi. Kutajana majina. Napata uchungu sana. Nimeongea na watu wa Loliondo. OBC hawajamilikishwa ardhi. Naibu Katibu Mkuu wa CCM hakwenda hivi hivi. Amekwenda kule wametupa kura. Naibu Katibu Mkuu kwenda ni jambo la kawaida kabisa,” alisema.