Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Mbeya
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Kanali Mstaafu Abdulrahman Kinana amemmwagia sifa Rais Samia Suluhu Hassan kutokana na kazi kubwa anayofanya ya kuleta maendeleo ya Watanzania.
Kanali Mstaafu Kinana ametoa sifa hizo kwa Rais Samia wakati akizungumza na wananchi na wanachama wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) katika Mkoa Mbeya.
Amesema Rais Samia Suluhu Hassan anafanya kazi kubwa maeneo mbalimbali nchini na kwamba amekuwa ni kiongozi anayezungumza polepole lakini vitendo vyake ni vingi kwani kila mkoa , kila sekta kuna fedha nyingi za maendeleo.
“Kote ambako nimepita tangu nilipoanza ziara mkoani Katavi na baadae Rukwa ,Songe Rais Samia amepeleka fedha nyingi kwa ajili ya miradi ya maendeleo na hapa Mbeya Mkuu wa Mkoa ametoa ushahidi wa fedha nyingi zilizotolewa na Rais kwa ajili ya miradi ya maendeleo,”amesema Kinana
Aidha Kinana amewapa salamu za Rais kwa wananchi hao kwamba atafika katika mkoa huo kwenye Maonesho ya Wakulima Nane yatakayofanyika kitaifa katika mkoa huo na kabla ya Rais Samia Makamu wa Rais Dk.Philip Mpango naye atakwenda katika mkoa huo.
“Mkoa wa Mbeya umepewa hadhi ya aina yake na ndio maana mmekuwa mkipokea wageni wengi na Rais Samia amenip salamu zenu kuwa atakuja hapa kuhudhuria maonesho ya Nane Nane.
Pamoja na salamu hizo Kinana amesisitiza Rais Samia anajituma anatafuta hela kwa njia mbalimbali na wananchi wakiwemo wa mkoa wa Mbeya wamekuwa mashuda.“Tangu Rais ameingia madarakani kuna fedha zinatolewa kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
”Katika hatua nyingine Kinana amezungumzia umuhimu wa reli ya TAZARA kwa wananchi wa mkoa huo katika kusafirisha abiria na mizigo na kwamba Serikali ya China iko tayari kuikarabati na Rais Samia yuko tayari kuisimamia ukarabati huo.
Amesema reli ya TAZARA mbali ya kuwa kichocheo muhimu cha kukuza uchumi wa wananchi pia imekuwa kiunganishi kikubwa kati ya nchi za Tanzania na Zambia.“Tukiimarisha reli hii tutakuwa na usafiri wa uhakika”.