Wakati tunaelekea kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2015, tayari yanasemwa mambo mengi kuhusu ni nani atakayekuwa mrithi wa nafasi ya Rais Jakaya Mrisho Kikwete.

Wananchi wanasema yao na ni halali yao kikatiba na kiutaratibu, kwa sababu wanayemsema ni kiongozi wao mkuu wanayemchagua wao. Sidhani kama ni kosa la jinai kusema kwamba fulani ndiye anayepaswa kuwa au atakayekuwa rais wao.

Kwa hiyo, hata mimi nimetumia njia hiyo kuonesha kilicho moyoni mwangu. Nataka nitaje ni mtu gani ambaye naona anafaa kupewa nafasi ya kuongoza nchi yetu baada ya muda wa rais aliyepo kwa sasa kwisha. Nalisema hili kwa nia njema nikisukumwa na mapenzi niliyo nayo kwa nchi yangu.

Mtu mwenye mapenzi mema na nchi yake ni lazima atizame ni namna gani nchi yake itaongozwa vyema, kwa ufanisi, ikiwa inapiga hatua kwenda mbele huku kila jambo la ustawi wa nchi likiwa limezingatiwa — usalama wa nchi na wananchi, maendeleo na mahitaji mengine ya kiutu na kadhalika.

Hayo yote yanahitaji mtu aliye makini katika kuhakikisha yanapatikana bila aina yoyote ya visingizio. Sababu  kama tunavyoona, matatizo mengine katika nchi yetu yanatokana na uzembe katika uongozi na usimamizi. Na hilo linatokana na ukosefu wa umakini.

Kwa hiyo, kwa upande wangu mimi mtu ninayemwona kuwa anatufaa kuwa kiongozi wetu mkuu — rais — ni Mheshimiwa Edward Ngoyai Lowassa (pichani juu). Ni mtu makini, mbunifu na mwenye kujisimamia kiuamuzi.

Nilianza kuuona uwezo wa Lowassa zamani kidogo, tangu alipokuwa Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha, AICC. Namna alivyokiongoza kituo hicho bila matatizo yoyote ya kukifanya kishindwe kujiendesha, ndilo jambo lililonifanya nianze kumwona kuwa anafaa. Nilitamani sana mtu huyo aingie kwenye siasa za nchi yetu ili aweze kutumia uwezo wake aliokuwa akiuonesha pale AICC kuusaidia uongozi wa nchi yetu.

Mungu si Athumani, taratibu Lowassa akaingia kwenye siasa za nchi yetu. Akaingia bungeni kwanza,  na baadaye akaupata uwaziri. Aliyoyafanya akiwa waziri ndiyo yaliyozidi kunidhihirishia uwezo wake.

Kinachonisukuma nimwone Lowassa ana uwezo tofauti na watu wengine ni moyo wake wa uchapakazi. Pamoja na hiyo yeye ana uwezo wa kuthubutu, ni mtu asiyebabaika katika kufanya uamuzi. Hiyo ni tabia ambayo kiongozi yeyote anatakiwa kuwa nayo.

Viongozi wengi wana tatizo la kushindwa kuchukua uamuzi. Tatizo hilo halijioneshi kwa Lowassa. Tunaweza kujikumbusha uamuzi aliochukua Lowassa wakati akiwa waziri wa kawaida.

Wakati fulani akiwa Waziri wa Ardhi aliwahi kuchukua uamuzi ambao mara nyingi wengi unawashinda na hivyo kufanya mambo yaende kombo. Mfano, kuna mtu alikuwa ametumia njia za kughushi na kujifanya eti anawekeza kwenye viwanja vya wazi vya Mnazi Mmoja, akavizungushia uzio wa mabati eti kwa lengo la kujenga mabanda kuzunguka viwanja hivyo.

Baada ya watu kulalamika, Lowassa alisema mara moja kwamba alichokifanya mhusika ni ukiukwaji wa Sheria za Mipango Miji, kwa hiyo akataka mabati hayo yaondolewe mara moja. Wananchi waliokuwa wanafuatilia kauli ya Serikali, baada ya kusikia kauli hiyo walimsaidia mwekezaji huyo feki kwa kuuondoa uzio wa mabati katika viwanja hivyo kwa muda mfupi sana. Walichojilipa kwa kazi hiyo ni kujibinafsishia mabati yenyewe.

Kwa hiyo, naweza kusema kwamba uamuzi wa Lowassa ndiyo uliovinusuru viwanja hivyo. Si ajabu bila yeye eneo hilo kwa sasa lingekuwa vingine kabisa, pengine viwanja vya wazi vya Mnazi Mmoja visingekuwapo na badala yake kungekuwapo na maduka, hoteli na kadhalika.

Vile vile, Lowassa aliweza kuunusuru ufukwe wa bahari unaotazamana na Hoteli ya Kilimanjaro. Kuna mtu aliyekuwa amejitokeza eti naye ni mwekezaji akitaka kulichukua eneo hilo!

Kitu kingine alichofanya Lowassa akiwa waziri wa kawaida, ni kuifuta kazi kampuni iliyokuwa imepewa zabuni ya kuendesha masuala ya maji Jijini Da es Salaam iliyokuwa ikiitwa City Water, wakati huo akiwa Waziri wa Maji. Kwa hiyo, tunaona kwamba mambo mengi yanazorota na kufikia kuwa matatizo katika utendaji wa Serikali yetu, kutokana na ukosefu wa uamuzi kutoka kwa wanaokuwa wamepewa jukumu la kusimamia.

Baada ya hapo, Lowassa alikuwa Waziri Mkuu wakati   Kikwete alipoingia Ikulu. Kwa kipindi kifupi aliweza kufanya mambo kama mtu aliyekalia cheo hicho kwa muda mrefu. Sababu ya kuonekana hivyo ilikuwa ni uwezo wake wa kuchukua uamuzi bila kusita.

Tuliona jinsi alivyolishughulikia suala la ukosefu wa umeme nchini ingawa watu waliligeuza wakasema ameingia mkataba na kampuni “feki” ya Richmond. Ukweli si yeye aliyefanya hivyo bali watu wasiokuwa waaminifu waliokuwa chini yake. Lengo la Lowassa lilikuwa zuri — kuiona nchi inaendeshwa bila matatizo ya umeme.

Na hivi karibuni imedhihirika kuwa uamuzi ule ulikuwa shirikishi. Rais Jakaya Kikwete alibariki kila hatua aliyoichukua Lowassa kuhusu Richmond na ndiyo maana alipomuuliza kwenye mkutano wa NEC pale Dodoma kuwa ni lipi alifanya bila maelekezo yake, Kikwete alikaa kimya hadi leo.

Ikumbukwe kwamba si kila uamuzi wenye lengo zuri unakuwa na matokeo mazuri. Kuna matokeo mengine yanayoweza kuwa kama ajali, wakati kilicholengwa ni kizuri ila matokeo yanakuwa mabaya. Ni sawa na mtu anayepanga safari bila kuelewa kuwa gari litapata ajali. Ajali ikishatokea huwezi kumlaumu aliyepanga safari. Kutokana na upungufu wa shule na ongezeko la watoto wanaoingia sekondari, Lowassa alibuni ujenzi wa sekondari za kata. Lengo lilikuwa  kila kata iwe na shule yake ya sekondari. Huo ni ubunifu mzuri ambao wengi waliomtangulia hawakuwahi kuufikiria.

Kwa hiyo, kukosekana kwa vifaa vya kufundishia pamoja na upungufu wa walimu kamwe hakufanani wala kulingana na kutokuwapo kabisa kwa shule za sekondari, yaani kuwaacha watoto wakirandaranda mitaani baada ya darasa la saba bila mahali pa kuwapeleka.

Nina imani Lowassa angeendelea kuikalia nafasi ya uwaziri mkuu ni lazima angebuni pia namna ya kupata walimu na vifaa vya kufundishia, kwa vile ubunifu unaonekana kuwa kipaji chake.

Wakati fulani alikuwa amebuni njia ya kupunguza msongamano wa magari katika barabara za Jiji la Dar es Salaam. Alisema barabara zenye njia nne ziwe na njia tatu kila siku kutegemea na muda ambao magari yanakuwa mengi.

Huo wote ni ubunifu anaopaswa kuwa nao kiongozi wa wananchi, ubunifu unaoongozwa na uamuzi katika mamlaka anayopewa kiongozi na wananchi. Kushindwa kubuni na kufanya uamuzi ndiyo mwanzo wa matatizo yanayotupata kwa sasa. Jambo dogo linageuka kubwa na wananchi wanaishia kwenye matatizo yasiyo ya lazima.

Kwa mtazamo wangu, tukimpata urais mtu kama Edward Lowassa, akawa mtu wa mwisho kufanya uamuzi katika nchi hii pasipo kuhojiwa na yeyote kabla ya kutekelezwa, tutakuwa tumepata kura ya turufu. Mtu huyu, kwa uwezo wake, ni lazima atatuvusha salama kwenye haya matatizo tuliyomo kwa sasa ambayo si kila jambo litafutiwe suluhisho nje ya nchi.

Kwa maana hiyo ni sababu hizo zinazonifanya nimwone  Lowassa kama mtu anayefaa kuwa kinara wetu ifikapo 2015. Kwa hiyo wananchi wanaoifikiria nchi yao kwa mapenzi mema wanapaswa kulitilia maanani jambo hilo. Si kwa kumpenda mtu kwa sura yake tu bali kwa uwezo wake.

Tukiondoa mambo ya mizengwe, ambayo nahisi hayamsaidii lolote mwananchi wa kawaida, Lowassa ndiye anayefaa kuwa rais wetu ajaye. Sisemi haya kwa vile tunafahamiana na Lowassa, la hasha, hanifahamu hata kidogo, ila nayasema kwa mapenzi mema niliyo nayo kwa nchi yangu.

Hivyo ninapomsema Lowassa, pamoja kuona kuwa ndiye mtu anayefaa kuwa rais wetu mtarajiwa, nayasema haya kutokana na uwezo huo alio nao, na mapenzi niliyo nayo kwa nchi yangu. Nchi yangu naitakia mema na mazuri, ndiyo maana namtaja mtu ninayeamini anafaa kuiongoza.

Watanzania tujiangalie, tusifanye makosa kama ambayo tumekuwa tukiyafanya muda wote. Tukumbuke kwamba kosa ni kurudia kosa na wala si kufanya kosa.

Mwandishi wa makala haya anapatikana kwa namba 0717 599 579