Barabara inayounganisha mikoa ya kusini mwa Tanzania; Mtwara, Lindi na mikoa ya Pwani na Dar es Salaam ni miongoni mwa barabara kubwa na muhimu nchini.

Ni barabara ambayo ilikuwa imesahaulika kama si kutelekezwa kwa miaka mingi baada ya Uhuru, na imeanza kutumika kikamilifu ndanii ya miaka 20 tu iliyopita.

Kabla ya hapo wakazi wa mikoa ya kusini walijiona kana kwamba wametengwa na wenzao katika kugawana keki ya taifa kwani hawakuwa na usafiri wa uhakika zaidi ya maji na anga.

Ujenzi wa barabara hiyo ulipoanza miaka ya 2000, Watanzania hawakuamini kama kuna miaka itafika ambapo walau sehemu ya pwani ya Bahari ya Hindi itakuwa imeungwanishwa kwa barabara na kupitika mwaka mzima.

Kikwazo kikubwa kilichokuwa kikifahamika kwa wengi ni Mto Rufiji, mmoja kati ya mito mikubwa nchini, na ujenzi wa Daraja la Mkapa ulipokamilika, kila mmoja akaamini sasa suluhu imepatikana.

Ghafla, eneo (oevu) tifutifu kati ya Somanga na Nangurukuru likageuka kuwa kikwazo kingine kwa usafiri wa barabara hiyo hasa nyakati za masika; na kipande hicho kilichokua muda mrefu sana ujenzi wake kukamilika.

Lakini hata baada ya kukamilia sasa kipande hicho, hasa Daraja la Somanga Mtama kimegeuka kuwa kidonda ndugu kisichosikia dawa au tiba ya aina yoyote kila mvua kubwa zinaponyesha.

Msimu wa mvua wa 2023/24 ulioambatana na mvua za El Nino ulisoma barabara na madaraja katika eneo hilo na kuilazimisha serikali kueleekza huko mabilioni ya fedha kurejesha hali kuwa ya kawaida.

Wananchi tukaamini kwamba kwa mabilioni ya fedha yaliyoelekezwa katika eneo hilo dogo tu la nchi, basi suluhu ya kudumu ingekuwa imepatikana.

Hali haikuwa hivyo kwani mwaka mmoja tu baadaye, mvua za kawaida zilizonyesha msimu huu wa masika zimeharibu tena barabara na kukata mawasiliano kati ya Dar es Salaam na mikoa ya kusini.

Kazi ya dharura ikafanyika na wataalamu usiku na mchana na kurejesha usafiri; lakini ndani ya wiki mbili au tatu tu, eneo hilo hilo likakumbwa na janga la aina ile ile na kusababisha mshangao kwa wananchi wa kawaida.

Je, ni kwamba wataalamu wetu wameshindwa kufahamu chanzo na ukubwa wa tatizo? Je, hali hii iyaendelea kujirudia hadi lini? Ni fedha kiasi gani zinahitajika kumaliza kabisa tatizo hilo?

Maswali haya yanapaswa kujibiwa na wahandisi wazawa na kisha kushirikiana na serikali kumaliza kabisa tatizo eneo la Somanga kwa kuwa tunaamini kuwa kujirudia kwa tatizo hili ji aibu kwa taifa.