Nakumbuka kipindi hicho kabla hatujacheza na Nigeria, kocha wa Taifa Stars aliwaita wachezaji wetu kadhaa wa kigeni. Lilikuwa na bado linabaki kuwa wazo zuri sana. 

Timu karibu zote ambazo hivi karibuni zimecheza mechi za kutafuta kufuzu zimeundwa na wachezaji wengi wanaocheza soka kwenye ligi za nje ya Bara la Afrika.

Uwezo wa vyama vya soka kuwatumia barua pepe wachezaji wa kigeni huchangiwa na ukaribu kati ya vyama hivyo na wachezaji wenyewe. TFF wanapaswa kuwa na taarifa sahihi za wachezaji wetu wote wanaocheza kwenye ligi mbalimbali duniani na taarifa hizi zinapaswa kuendana na muda uliopo.

Mtandao wa shirikisho letu la soka uwe ukizifahamu kila hatua za wachezaji wetu wanaocheza nje ya nchi, pindi wanapohama kutoka klabu moja kwenda nyingine. Iko haja ya kuhakikisha hata zile video zinazowaonyesha wakicheza, kuonekana kwa makocha wa timu ya taifa mara kwa mara.

Wakati benchi zima la ufundi la Taifa Stars linapowatazama kwa ukaribu wachezaji wanaocheza Ligi Kuu, ni vizuri wale walio nje ya nchi wakatazamwa maendeleo yao ndani ya wakati husika. TFF itoe ushirikiano mkubwa katika hili suala, inao uwezo wa kufanya hivyo.

Wachezaji wetu wanaocheza nje ya nchi wanazo mbinu wanazozipata kutoka kwa makocha wao, zinaweza kabisa kuiongezea Taifa Stars ari ya utafutaji wa ushindi.

Ukusanyaji wa taarifa za wachezaji wetu walioko nje uende sambamba na zoezi la kuwasaidia wale wenye uwezo kupata timu katika ligi za mabara mengine. Tunawakosa wachezaji wachache wenye kuweza kuituliza timu wakati inapokutana na wachezaji wakubwa wa timu za mataifa mengine ya Afrika.

TFF ambayo kwa sasa inawapeleka watoto wa chini ya miaka 13 nchini Afrika Kusini, watumie jitihada hizo hizo katika kuwafuatilia wachezaji wetu wanaotafuta maisha nje ya nchi.

TFF wasibweteke wakidhani kwamba wachezaji wenye asili ya Tanzania wataitikia mwito wa kuja kuichezea Taifa Stars kirahisi tu. Wengine wamekwenda nje kwa nguvu zao wenyewe, wamesota sana mpaka kufikia hapa walipo.

Waheshimiwe kama watu waliotoka nje ya mipaka kwa sababu ya utafutaji wa maisha, kama wafanyavyo Watanzania wengi tu wanaoishi ughaibuni. Isiwe ni amri inayotoka kwa mkubwa kwenda kwa mdogo. Lazima heshima ya kile wakifanyacho iwepo wakati TFF inapoanzisha maongezi na wachezaji wetu wanaocheza soka nje ya nchi.

Huu ndio wakati muafaka kuanzisha mawasiliano ya barua pepe kati ya TFF na wachezaji wenyewe au mawakala waliowapeleka huko waliko. Wenzetu wanafuatilia wachezaji waliotoka kwenye ligi za nyumbani mpaka wale ambao wamezaliwa nje ya Afrika lakini baba zao ni Waafrika waliokwenda ughaibuni miaka ya zamani.

Vyama vyao vya soka viko tayari kupokea taarifa za wachezaji waliozaliwa Afrika na wale waliozaliwa ughaibuni ndani ya mwaka mzima. Miezi yote kumi na mbili hutumika katika kumjua ni mchezaji gani ameumia, mchezaji gani ameuzwa wapi, mchezaji gani hana nidhamu na taarifa nyingine za aina hiyo.

TFF ipokee changamoto hii ya kuwa karibu na wachezaji wetu wote walio nje ya Tanzania. Haipendezi kumwambia mchezaji wa Tanzania arudi kuichezea timu yake ya taifa wakati ndani ya muda wote aliokuwa akihangaika kutafuta maisha huko nje hakuwahi kukumbukwa na TFF kwa namna yoyote ile.

Hivi sasa TFF inao wadhamini wakubwa, hili suala la kupata taarifa za wachezaji wetu haliwezi kuwa na gharama za kutisha hata kidogo.

Timu ya taifa inaweka kambi Uturuki, inatumia fedha nyingi. Sidhani kama inashindwa kuanzisha mawasiliano na wachezaji wetu walio nje ya nchi.