Nimemsikia Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, akisema Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) hakina hazina ya viongozi kama iliyonayo Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Ametamba kwamba CCM inaweza kusimamisha wagombea urais 20 wenye sifa zinazofanana, lakini Chadema inamtegemea Dk. Wilbrod Slaa pekee. Kwa maelezo yake, mtu kama Mbowe, hana sifa za kuwa rais kwa sababu ni mchezesha disko la usiku!

 

Madai haya ya Mzee Sitta si ya leo. Ameanza kuyazungumza siku nyingi. Yamechusha kuyasikia. Wakati mwingine si jambo la busara sana kwa mtoto kuingia kwenye malumbano na mtu aliyemzidi umri, lakini inapotokea mzee akapuuza hatari iliyo mbele yake; hatari ambayo mtoto anaijua, huyo mtoto asipomweleza ukweli huyo mzee, atakuwa amefanya kosa hubwa.

 

Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, katika maandiko yake kupitia Kitabu cha Tujisahihishe aliyoyatoa Mei, 1962 (miaka 50 sasa) alisema, “Ukweli una tabia moja nzuri sana, haujali mkubwa wala mdogo, hujali adui wala rafiki. Kwake watu wote ni sawa. Pia ukweli unayo tabia ya kujilipiza kisasi kama ukipuuzwa. Ukiniona nataka kupiga teke jiwe kwa kuwa unafikiri kuwa ni dongo au mpira, natumaini utanionya. Lakini nikilipuuza onyo lako kwa sababu eti wewe ni mdogo au kwa sababu sikupendi, nikalipiga teke, basi litanivunja dole japo ningekuwa nani. Ukweli haupendi kupuuzwapuuzwa.” Mwisho wa kunukuu.

 

Nukuu hii nimeitumia ili Mzee Sitta na wahafidhina wengine ndani ya CCM wasidhani kuwa nawakosea adabu kuwakosoa.

 

Pili, Baba wa Taifa, kwa kutambua kuwa kuna watu wanaoacha kujadili hoja ya msingi na kurukia mambo yasiyoendana kabisa na ukweli wa mambo, kupitia kitabu hicho hicho cha Tujisahihishe, alisema, “Wakati mwingine mtu tunayempinga huwa ana makosa kweli, lakini hoja tunazotoa ni za kibinafsi na hazihusiani kabisa na hoja zake. Nikisema mbili na tatu ni sita, nakosa. Lakini ni bora kunionyesha kwamba pengine nafikiri tunazidisha kumbe tunajumlisha. Ni kweli mbili mara tatu ni sita, lakini mbili na tatu ni tano, siyo sita. Lakini ukijaribu kuwashawishi wenzetu wakatae mawazo yangu na kukubali yako kwa kusema kuwa meno yangu ni machafu, au natoa kamasi daima, utakuwa unatumia hoja ambazo hazina maana. Huu ni mfano wa upuuzi, lakini mara nyingi hoja tunazotumia kuwashawishi watu wakatae mawazo ya wale tusiowapenda, au kukubali mawazo yetu huwa hazihusiani kabisa na mambo tunayoyajadili.” Mwisho wa kunukuu.

 

Hapa utaona kuwa hoja kwamba Mbowe ni mcheza au mwendesha disko, hazihusiani kabisa na suala la kumpata Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Dunia imeshuhudia mataifa mengi duniani yakiongozwa na watu waliopitia mazingira na kazi mbalimbali (wakiwamo tunaowaita waasi).

 

Kuna mataifa yameongozwa na wana muziki. Yapo yaliyoongozwa na wacheza mieleka. Sidhani kama kuna mtu kazaliwa, kaa bila kufanya shughuli yoyote, mwisho wa siku akaipata kazi aliyopangiwa akingali tumbani, yaani kazi ya urais. Hata Mzee Sitta mwenyewe si ajabu alikuwa mchunga mbuzi kabla ya kuijua siasa! Je, tuseme sasa kuwa hafai kuwa rais kwa sababu amepata kuwa mchunga mbuzi?

 

Kichwa cha makala yangu, “Kimwili ni CCM, rohoni ni Chadema”, kinajieleza vizuri. Sitta anajidanganya kwa nadharia zake za kwamba Chadema anayoiona sasa ndiyo Chadema baada ya kuingia madarakani. Mara zote nadharia hizi zimethibitika kinyume kabisa. Kwa mfano, wazee waliokuwapo wakati wa harakati za TANU kudai Uhuru wa Tanganyika wanasema Mwalimu Nyerere na wapambanaji wengine walipuuzwa na kubezwa mno.

 

Wabezaji hawakuwa Wazungu, Waarabu, machotara na Wahindi pekee, bali hata Waafrika weusi. Hawa ni wale walioamini kuwa hakuna Mwafrika anayeweza kuwang’oa wakoloni. Mwafrika alionekana kuwa dhaifu katika kila idara. Kigezo cha elimu kilitumika kama moja ya nyenzo za kuhalalisha fikra hizo potofu. Wapo waliohoji, “Wanataka Uhuru, wakiupata nchi itaongozwa na nani ilhali hakuna wasomi?”

 

Maneno hayo hayakuwakatisha tamaa wapambanaji mahiri wakiwamo kina mama kama Bibi Titi Mohamed ambao hawakuwa na elimu kubwa. Baada ya Uhuru wakapatikana watu wenye sifa ya kuwa viongozi, hata kama kwa idadi walikuwa wachache. Wakawamo watu kama kina Dereck Bryceson, Amir Jamal, Alnuur Kassum na kadhalika. Hawa wakaungana na wenzao weusi kuliongoza taifa jipya la Tanganyika.

 

Hii maana yake nini? Maana yake ni kwamba wakati wa harakati za mapambano ya kudai Uhuru si Wazungu, Wahindi au machotara wote waliotaka kuonekana wakiwa mstari wa mbele moja kwa moja. Wapo walioamua kuonekana mbele, lakini wapo walioiunga mkono TANU kimya kimya na wakaamua kujitokeza hadharani baada ya mambo kuiva.

 

Hili ni somo kwa Sitta na wenzake. Wasidhani kwamba nguvu hii ya Chadema, CUF na vyama vingine ni nguvu inayoonekana na kuishia majukwaani. Nyuma ya Chadema, CUF na vyama vingine vya upinzani kuna jeshi kubwa mno la Watanzania wanaowaunga mkono, tena Watanzania wa rangi zote. Kuna Watanzania wenye uwezo mkubwa kifedha na kiuongozi wanaovisaidia vyama hivi.

 

Hawa ni wale ambao kama ilivyokuwa wakati wa kupambana na wakoloni wa Kiingereza, hawataki kujionyesha moja kwa moja majukwaani. Kama ni sifa ya kuwania urais, Sitta asubiri “muziki” mwaka 2015 au 2020 ndipo aseme. Sitta anataka kutuaminisha kuwa Mbowe ni mchezesha disko. Sawa. Kwani kuchezesha disko ni dhambi? Disko inamzuia vipi mtu kuliongoza taifa? Je, wale wanaocheza disko au dansi nao tuseme hawana maana wa la uwezo wa kuongoza?

 

Maudhui yangu hapa ni kuwa Mzee Sitta asidhani kwamba haya mambo yataendelea hivi kama yalivyo. Wala asijipe matumaini kuwa kwa uongozi legelege ndani ya CCM na hata Serikali, kunaweza kuwazuia watu kumchagua DJ kuwaongoza. Madagascar wamefanya hivyo. Wananchi wa Madagascar kama unataka kukosona nao sasa, mseme vibaya Rais wao mchezesha disko, Andry Rajoelina. Wanampenda kwa sababu amekidhi kile kinachotakiwa na wengi – maisha bora kwa kila (Mmadagascar). Tena wapo wanaohoji kuwa imekuwaje kwa muda mrefu hawakuweza kufunuliwa au kupewa maono ya kuongozwa na DJ!

 

Anachokiona Sitta sasa kwa Chadema na vyama vingine vinavyoipinga CCM si mambo ya kupuuza. Kuna mambo ambayo wananchi wa kawaida wanaona heri kutawaliwa na yeyote awaye, alimradi asiwe kichaa!

 

Kusema hivyo si kwamba nabeza mazuri yaliyopatwa kufanywa na CCM kwa miaka yote hii, la hasha. Yapo mazuri yaliyofanywa, lakini wananchi wangetaka kuona mazuri zaidi. Mara zote Serikali ilipofanya jambo jema, wananchi wameonekana kufufua mapenzi na matumaini yao kwa CCM. Lakini pale Serikali ilipozembea au kupuuza kushughulikia kero zilizo wazi, wananchi wameonekana kuwa tayari kuongozwa, acha na DJ, bali hata na mwendawazimu!

 

Lakini wakati mwingine binadamu wametaka mabadiliko tu kwa sababu ndivyo walivyoumbwa. Sitta na wenzake wanaweza kujiuliza, hivi inakuwaje, licha ya Serikali kujenga miundombinu kama vile Chuo Kikuu cha Dodoma, bado vijana wengi wanaonekana kuichukia CCM? Je, kwanini pamoja na ujenzi wa barabara za lami katika maeneo mengi nchini, bado wananchi wanaonekana kuichoka CCM?

 

Hawaichoki kwa sababu wamo kina Sitta na wenzao bali kwa sababu wanataka mabadiliko. Kwani katika nyumba zetu hatuoni watoto wakigoma kula nyama, badala yake wakitaka maharage? Hawagomi kwa sababu wanaichukia nyama, bali kwa sababu wanataka kubadili mlo.

 

Vivyo hivyo, CCM haiwezi kung’ang’ana kwamba itaongoza taifa hili milele. Haiwezi kwa sababu watu wanataka mabadiliko, na hakuna cha kuzuia mabadiliko. Mtoto aliyezaliwa mwaka 1990 hana habari na kitu kinachoitwa CCM, tena sana sana anayesoma historia atahoji, “Kwanini hawa waendelee kutawala kwa nusu karne sasa?” Jibu la swali hilo wanalisambaza kupitia maandamano ambayo vijana wengi wanashiriki bila kuogopa mitutu na mabomu ya polisi waliovaa mavazi ya kutisha mithili ya askari wa Kirumi.

 

Alimradi mfumo wa vyama vingi vya siasa upo kikatiba, basi tuukubali. Kubezana ndiko kunakoufanya mfumo huu uonekane sasa kama ni wa vurugu.

 

Kubwa kuliko yote na ambalo Sitta mwenyewe analijua ni kauli za baadhi ya wabunge na mawaziri shupavu ambao bila kujali yatakayowapata ndani ya CCM, hujitokeza hadharani kukikosoa chama hicho. Siri za vigogo zinazovuja kila siku zinatolewa na wale wanaoamini kuwa DJ anaweza kuwa afadhali kuliko mcheza disko! Wenye lugha yao wanasema, “Everything changes, nothing ever stays the same.” Wengi ni CCM kimwili tu, kiroho wako Upinzani!