Nianze kwa kuwatakia heri ya mwaka mpya, wasomaji wa JAMHURI. Ni jambo jema kusema, “inatupasa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuuvuka mwaka 2017 salama.”

Pamoja na salaam hizo, mwaka mpya unaibua matumaini mapya, upendo penye chuki na heshima palipo na dharau.

Ndivyo Mpita Njia ninavyotarajia, kamba 2018 itakuwa mwaka wenye kuleta tumaini la heri kwa wakazi wa eneo la kuanzia Kimara hadi Bonyokwa, wanaohangaika ‘miaka nenda, miaka rudi’ kutokana na ubovu wa barabara ya eneo hilo.

Barabara hiyo inayounganisha halmashauri za manispaa ya Ubungo na ile ya Ilala, inatumiwa na maelfu ya watu wanaozidi kuongezeka kutokana na kuzaliwa watoto ama wahamiaji.

Ongezeko hilo la watu linaendana na ongezeko la mahitaji na bidhaa kama vile vifaa vya ujenzi, vyakula, maji nakadhalika.

Lakini zaidi ya hayo, watu hao wanahitaji usafiri wa uhakika ili kutoka salama kwenye makazi yao kwenda kushiriki shughuli za uzalishaji na ujenzi wa taifa.

Kinachoshangaza ni kwamba kwa miaka mingi barabara ya Kimara-Bonyokwa imekuwa mbovu na imezidi kuharibika zaidi kutokana na mvua za hivi karibuni, zilizosababisha maeneo hasa yenye madaraja kubomoka.

Hali hiyo ikiendelea, si ajabu ukafika wakati wakazi wa maeneo yanayopitiwa na barabara hiyo wakashindwa kutoka upande mmoja kwenda mwingine.

Inawezekana hivyo kwa sababu katika siku za karibuni, kumekuwapo ongezeko la magari yanayotumbukia kwenye daraja lililopo kati ya Kimara na Vinane.

Wakati hali ya barabara ikiwa mbaya upande huo, eneo la manispaa ya Ilala kutokea Segerea hadi karibu na Kwa Mahita, yanapitiwa na barabara ya lami.

Hivyo mkazi wa Bonyokwa anapotokea Ilala kupitia Segerea, ana uhakika wa kusafiri kwenye barabara ya lami hadi anapoingia upande wa Ubungo, anapokutaka na vumbi, tope (wakati wa mvua) na mashimbo.

Inafaa sasa, kwa kadri ya maoni ya Mpita Njia, mamlaka zinazohusika kuwasaidia wakazi wa Kimara-Bonyokwa ili waondokane na adha zinazotokana na ubovu wa barabara. Ijengwe kwa kiwango cha lami.