Kuna tetesi ambazo zinaendelea kushika kasi kwamba afisa wa ngazi ya juu wa serikali ya Korea Kaskazini ambaye amefanya ziara ya ghafla nchini China ni kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong-un.
Vyombo vya habari Japan vilikuwa vya kwanza kuibuka na taarifa kwamba afisa wa ngazi ya juu mno kutoka Korea Kaskazinia alikuwa amewasili Beijing kwa kutumia treni maalum ya kidiplomasia.
Treni hiyo ilipokelewa kwa ulinzi mkali.
Korea Kusini imesema haifahamu ni nani huyo aliyefanya ziara hiyo lakini inafuatilia tukio hilo kwa makini sana.
Ikithibitishwa kwamba aliyefanya safari hiyo alikuwa Bw Kim, basi itakuwa mara yake ya kwanza kufanya ziara nje ya nchi yake tangu alipochukua madaraka mwaka 2011.
Bado hakujakuwa na taarifa yoyote rasmi kutoka China wala Korea Kaskazini, lakini tukio kama hilo litakuwa kubwa.
Mwezi jana, Rais wa Marekani Donald Trump alikubali mwaliko usio wa kawaida wa kukutana na Bw Kim.
Maafisa wa Marekani wanadaiwa kushughulika sana kuhakikisha taratibu zote zinawekwa sawa kidiplomasia kuhakikisha mkutano huo unafanyika na kuwa wa kufana.
Wachanganuzi wanasema viongozi wa Korea kaskazini na China wanaweza kuwa wameamua kukutana kabla ya mkutano huo wa Bw Kim na Bw Trump kufanyika.
China ndiyo mshirika mkubwa zaidi wa kiuchumi wa Korea Kaskazini.
Picha za video za treni hiyo ambazo zimepeperushwa na kituo cha habari cha Nippon News Network chenye makao yake Tokyo zimeonesha treni hiyo ina mistari ya mlazo ya rangi ya manjano.
Kituo hicho cha runinga kimesema treni hiyo inafanana sana na aliyoitumia babake Bw Kim, mtangulizi wake Kim Jong-il alipozuru Beijing mwaka 2011.
Kim Jong-il aliogopa sana kutumia ndege kusafiria.
Safari za Kim Jong-il nchini China zilikuwa zinathibitishwa tu baada yake kuondoka.
Msimamizi wa duka moja nje ya kituo cha treni Beijing amesema ameshuhudia “shughuli zisizo za kawaida” kituoni.
“Kulikuwa na maafisa wengi wa polisi nje na kwenye barabara upande wa mbele wa kituo. Kituo hicho kilikuwa kimefungwa ndani,” ameambia AFP.
Polisi pia waliwaelekeza watalii hadi nje ya uwanja maarufu wa Tiananmen, Beijing kwa mujibu wa Reuters jambo linaloashiria kwamba kulikuwa na mkutano wa ngazi ya juu sana katika ukumbi maarufu wa mikutano ulio hapo karibu wa Great Hall of the People.
Msafara wa magari uliosindikizwa na maafisa wa polisi ulionekana ukiondoka eneo hilo, Reuters wanasema.
Katika jiji la mpakani kati ya China an Korea Kaskazini la Dandong, ambapo kuna reli inayounganisha China na Korea Kaskazini, matukio yasiyo ya kawaida yalishuhudiwa pia.
Shirika la habari za Korea Kaskazini NK News limesema limepata picha zinazoonesha vibao vya muda vikitumiwa kuziba njia moja ya kuingia eneo hilo, ingawa kuna uwezekano kwamba pengine kulikuwa na kazi ya ukarabati.
Bloomberg wamewanukuu watu watatu wakisema mgeni huyo alikuwa Bw Kim.
Wachambuzi waliozungumza na kituo cha habari cha Korea Kusini Yonhap wanasema aliyezuru huenda pia akawa dada mdogo wa Bw Kim, Kim Yo-jong, ambaye majuzi alihudhuria Michezo ya Olimpiki ya majira ya baridi nchini Korea Kusini, au iwe ni afisa mkuu wa kijeshi Choe Ryong-hae.
Mapema mwezi huu wa Machi, waziri wa mambo ya nje wa Korea Kaskazini alihudhuria mazungumzo na waziri mkuu wa Sweden mjini Stockholm Stefan Lofven, kabla ya mkutano huo wa Bw Trump na Bw Kim mbao bado unapangwa.
Wakifanikiwa kukutana kama ilivyotarajiwa mwezi Mei, itakuwa ni mara ya kwanza kwa viongozi wa Marekani na Korea Kaskazini kukutana.
Bw Kim pia anatarajiwa kukutana na mwenzake wa Korea Kusini Moon Jae-in mwezi ujao.