Na Is-haka Omar,Zanzibar
Katibu wa Kamati Maalum ya NEC,Idara ya Organazesheni CCM Zanzibar Omar Ibrahim Kilupi,amesema zoezi la kura za maoni ndani ya Chama Cha Mapinduzi lisiwagawe wanachama badala yake wawaunge mkono wagombea watakaopitishwa na vikao vya maamuzi.
Ushauri huo ameutoa katika mwendelezo wa ziara ya Sekretarieti ya Kamati maalum ya NEC,CCM Zanzibar kwa niaba ya Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dkt.Mohamed Said Dimwa wakati akizungumza na Kamati za siasa za matawi,wadi,majimbo na Wilaya ya Dimani kafika.

Alisisitiza ushirikiano kwa wanachama wote kwa lengo la kulinda hadhi,nguvu na heshima ya Chama Cha Mapinduzi kisiasa kwa kuhakikisha wagombea waliopitishwa na Chama wanashinda katika uchaguzi Mkuu wa dola mwaka huu.
Aliwasihi wajumbe hao kuweka kando misimamo na makundi yasiyofaa ndani ya Chama na badala yake wabaki na kundi moja la CCM litakalosimamia maslahi ya wanachama wote bila upendeleo.
Kilupi,alisema kuwa CCM tayari imetangaza rasmi mchakato wa ndani ya chama wa kura za maoni wa kuwania nafasi za kugombea ubunge,uwakilishi na udiwani katika uchaguzi wa dola octoba mwaka huu,ambao fumu zitaanza kutolewa kuanzia Mei 1 saa 2:00 asubuhi hadi Mei 15 saa 10:00 jioni mwaka 2025.
Aliwasihi wanachama wote wenye nia ya kuwania nafasi hiyo wajitokeze kwenda kuchukua fomu kwa mujibu wa utaratibu uliowekwa ili kuimarisha demokrasia ndani ya Chama.

Alisema, hiyo ni fursa kwa wanachama wa makundi yote kushiriki katika mchakato huo ili waweze kupata nafasi za uongozi kwa njia halali na zenye ushindani kwa dhamira ya kuwatumikia wananchi.
“Kila mwanachama ana haki ya kuchagua na kuchaguliwa katika mchakato ya ndani ya Chama,utaratibu huu unaruhusu ushindani na hatimaye vikao vya juu vinafanya maamuzi ya mwisho ya uteuzi kwa mujibu wa sifa za kila mgombea”alisema Kilupi.
Katika ziara hiyo Kilupi, alifafanua mabadiliko ya Katiba ya CCM ya mwaka 1977 toleo la mwaka 2022 yaliyofanyika katika Mkutano mkuu maalum wa januari 18 hadi 19, mwaka 2025 ya kuongeza idadi ya wapiga kura kwenye vikao vya kura za maoni kwa wagombea wa ubunge,uwakilishi na udiwani.
Kwa upande wake Katibu wa Kamati Maalum ya NEC,idara ya itikadi,uenezi na mafunzo CCM Zanzibar Khamis Mbeto Khamis,alisema kuwa wakurugenzi wote wa uchaguzi kwa ngazi mbalimbali za Chama wahakikishe wanatenda haki kwa wanachama wote katika mchakato wa ndani wa kura za maoni kwani vikao ndio vitakavyofanya maamuzi ya uteuzi kwa mujibu wa vigezo na sifa zilizowekwa.

Alisisitiza kuwa muda wa kufanya kampeni katika majimbo bado haujafika na majimbo hayo bado yapo chini ya viongozi wake,hivyo wanachama waendelee kuwapa nafasi ya kutekeleza majukumu yao ipasavyo.
Akizungumza Mnadhimu wa CCM katika Baraza la wawakilishi Zanzibar ambaye pia ni Mjumbe wa Sekretarieti ya Kamati Maalum ya NEC,CCM Taifa Zanzibar Yahya Rashid Abdulla, amewasihi wanachama wote wa CCM na jumuiya zake kuwa wamoja na kushikamana ili kuhakikisha Chama kinapata ushindi mkubwa katika uchaguzi Mkuu wa dola wa Octoba 2025.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa UVCCM Zanzibar Abdi Mahmoud Abdi,aliwataka viongozi na wanachama kwa ujumla kuhakikisha wanaweka mazingira rafiki kwa vijana watakaoamua kuwania nafasi za uongozi na kwamba wasipewe vitisho na kukatishwa tamaa kwa vigezo vya uzoefu na umri wao kwani nao wana haki ya kuchagua na kuchaguliwa.
Katibu wa CCM Wilaya ya Dimani Alawi Haidar Foum, akisoma taarifa ya kazi amesema Wilaya hiyo imeendelea kupata mafanikio makubwa katika utekelezaji wa kazi za Chama Cha Mapinduzi na jumuiya zake zikiwemo kuwa ya kwanza Tanzania katika zoezi la usajili wa wanachama katika mfumo wa kazi za kielektroniki.
Alisema Kamati ya siasa ya Wilaya hiyo imekuwa ikitatua changamoto mbalimbali za kisiasa na kiutendaji kwa njia za busara na kufuata miongozo na kanuni za Chama Cha Mapinduzi.