Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya imekamata jumla ya kilo 399.28 za dawa za kulevya aina ya bangi katika Kitongoji cha Sokoni, Kiji cha Chogoali, Kata ya lyogwe, tarafa ya Gairo, wilaya ya Gairo, mkoani Morogoro.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka katika mamlaka hiyo imesema kuwa ukamataji huo umefanyika kufuatia operesheni iliyofanywa na Mamlaka mkoani humo Desemba 22,mwaka 2022 ambapo watu wawili wanashikiliwa kuhusika na usafiishaji wa kiasi hicho cha bangi.

Aidha,watuhumiwa hao wamekutwa na bunduki mbili aina ya gobole zenye namba MG-188 na MG-148 pamoja na ngozi ya mnyama anayedhaniwa kuwa ni Kakakuona. Watuhumiwa hao watafikishwa Mahakamani baada ya taratibu za kisheria kukamilika.

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya inaendelea kufanya operesheni katika maeneo mbalimbali nchini ili kuhakikisha inadhibiti uzalishaji na usafirishaji wa dawa za kulevya.