NA MWANDISHI WETU
Mwakilishi wa Umoja wa Afrika (AU) nchini Comoro ameingilia kati mgogoro wa kuwekwa kizuizini kwa Rais mstaafu wa Visiwa vya Comoro, Ahmed Abdallah Mohamed Sambi.
Mwakilishi huyo, Hawa Youssouf, amemtembelea Rais mstaafu Sambi kizuizini alikowekwa kwa amri ya Rais Azali Assoumani, kwa takriban miaka minne sasa.
Baada ya kuonana naye, Hawa amezungumza na waandishi wa habari lakini hakutaka kuweka wazi alichoteta na mwanasiasa huyo anayeheshimika duniani.
“Nitapeleka ripoti kwa Rais Azali Assoumani, ambaye pia nitazungumza naye, halikadhalika nitapeleka taarifa kwa Rais wa Umoja wa Afrika,” amesema Hawa.
Pamoja na Hawa, viongozi wengine waliokwenda kumuona Sambi ni pamoja na Balozi wa Umoja wa Ulaya (EU) nchini Comoro, Giovanni Girolamo na ofisa mwingine wa EU, na Pierre Beziz.
Mwakilishi Mkazi wa Umoja wa Mataifa (UN) katika Visiwa vya Comoro, Francois Batalinganya, alipata kibali cha kumuona Rais Sambi kizuizini wiki kadhaa zilizopita.
Taarifa zinasema baadaye kiongozi huyo alionana na Rais Azali, dhamira kuu ikiwa kumsihi amwachie huru kiongozi huyo anayeheshimika mno ndani na nje ya Comoro.
Lakini ombi jingine lilikuwa kumuomba Rais Azali amruhusu ‘mfungwa huyo wa kisiasa’ aende kutibiwa nchini Tanzania ambako alishapewa hisani hiyo na aliyekuwa Rais wa Tanzania, hayati Dk. John Magufuli.
Watu waliokuwa karibu wakati Batalinganya anakwenda kumjulia hali Sambi, wanasema gari lake lilizuiwa kuingia, hivyo akalazimika kuliacha nje.
Hii ilikuwa ni mara ya pili kwa kiongozi huyo kuomba kumuona Sambi. Mara ya kwanza licha ya kukubaliwa, baadaye alizuiwa kumuona.
Sambi akiwa tayari ameshapata tiketi ya ndege kwenda Dar es Salaam kwa matibabu, Rais Azali akaagiza ruhusa hiyo ifutwe.
Mahakama ilishatoa kibali Rais mstaafu huyo apewe matibabu, lakini Rais Assoumani mara zote amekaidi na kuhadaa ulimwengu kuwa Sambi amenyimwa ruhusa na Mahakama ya Comoro.
Rais Azali ameendelea kuwa na msimamo mkali dhidi ya Sambi kwani Agosti 23, mwaka jana Rais Samia Suluhu Hassan alimtuma Rais mstaafu Jakaya Kikwete ampelekee salamu zilizohusu hatima ya Rais Sambi, lakini duru za habari kutoka pande zote zinaonyesha kuwa kiongozi huyo hadi sasa hajaonyesha dalili za wazi kukubali au kuyakataa maombi ya Rais Samia.
Wakati wa ziara yake ya hivi karibuni nchini Ubelgiji, Rais Samia alilakiwa na mamia ya wananchi wa Comoro waliopeperusha bendera za taifa hilo na Tanzania.
Baadhi ya Wacomoro hao walishika mabango wakimsihi asaidie kutolewa kizuizini kwa Rais mstaafu Sambi.
Hayo yakiendelea, vyama vya siasa nchini Comoro vimepinga mpango wowote wa kuwa na mkutano wa upatanishi na Rais Azali, kwa shinikizo kwamba hilo litawezekana tu endapo atakuwa amemwachia huru Sambi.
Wananchi wanaompinga Rais Azali wanasema yuko madarakani kinyume cha Katiba ya Comoro, na kwamba mwisho wa utawala wake ulikuwa mwaka jana, lakini amepuuza katiba na kuendelea kushikilia madaraka.
Wakosoaji wake walioketi Desemba 4, mwaka jana walisema endapo Rais Azali anataka maridhiano ya kitaifa kama anavyoonyesha sasa, pamoja na kumwachia Sambi, sharti awaachie wafungwa wengine wa kisiasa.
Wanamtaka Rais Azali aruhusu wakimbizi wa kisiasa walio nje warejee Comoro bila masharti yoyote, na mwisho aweke mazingira mazuri ya amani ili kurejesha haki na uhuru wa watu.
Wanamtaka Rais Azali arejee kwenye utaratibu wa kuiheshimu katiba ya nchi kwa kuzingatia Makubaliano ya Fomboni yaliyoasisi utaratibu wa kuwa na rais wa Comoro kwa mzunguko wa visiwa.
Anatakiwa pia aache kuingilia taratibu za kumpata rais wa Comoro kwa kuwapa nafasi wananchi kuamua nani wanataka awe kiongozi wao.
Jumuiya ya kimataifa, wadau wa maendeleo na marafiki wa Comoro wanatajwa kama wadau wakuu wa kuipata Comoro yenye ustawi, usawa na haki.