Mvua za mwaka huu zimetuathiri kiuchumi sisi Watanzania. Mafuriko yametokea karibu katika kila mkoa na kusababisha uharibifu mkubwa katika miundo mbinu ya nchi hii.
Kuna madaraja yamekatika au kumeguka au hata kusombwa na maji kabisa. Haya yametokea katika Barabara ya Dar es Salaam-Bagamoyo pale kwenye Mto Mpiji, barabara ya Dar es Salaam-Kilwa kule Kongowe penye Mto Mzinga.
Aidha, mito kadhaa imefurika na kukata mawasiliano katika maeneo ya Mto Kilombero kule Ifakara, yamekata kivuko kile cha kuunganisha Ifakara na Mahenge. Huko Kyela, vijiji kadhaa vimesombwa na mafuriko. Kilosa eneo la Dumila barabara na daraja yamekwenda na maji. Kule Godegode, reli imeng’olewa na hata hii Barabara Kuu ya Dar es Salaam-Morogoro penye Mto Ruvu, mto umefurika kiasi cha maji kupita juu ya barabara ya lami.
Haya yote yamekatisha mawasiliano katika nchi yetu. Kurekebisha hayo na kurejesha tena mawasiliano ya barabara maana yake mamilioni ya shilingi nje ya bajeti ya Serikali yametumika.
Hali hii imedumaza uchumi wa Taifa hili kwa kiasi kikubwa. Nani alaumiwe? Mimi nasema hakuna. Si Serikali wala si Mungu. Matokeo namna hii tunayaita maafa ya kimaumbile (natural disasters), maafa namna hii yanatokea ulimwenguni kote siyo hapa Tanzania tu.
Basi, uchumi wetu mwaka huu utatetereka na hakuna wa kumlaumu. Sote tunapaswa kuelewa hivyo na tuvumilie angalau anguko namna hiyo katika uchumi wa Taifa letu mwaka huu.
Tangu zamani enzi za mababu zetu Wayahudi, maafa ya mafuriko yalitokea. Tunakumbuka vizuri mafuriko enzi za Nuhu. Vyote viliangamizwa kwa mafuriko isipokuwa Nuhu na familia yake na aina zote za mifugo. (Soma kutoka Nuhu hadi Abrahamu; Kitabu cha Mwanzo Sura 8 mistari 15-17).
Baada tu ya gharika ile Mungu akasema “Sitalaani nchi tena baada ya hayo kwa sababu ya mwanadamu… wala sitapiga tena baada ya hayo kila kilicho hai kama nilivyofanya (Mwa. 8:21). Baada ya hapo Mungu akatoa ahadi yake kwa agano hili, “Mimi naweka UPINDE wangu (rainbow) MAWINGUNI nao utakuwa ni ISHARA ya AGANO kati yangu na nchi (Mw. 9: 12-14).
Ndiyo kusema gharika haitatokea tena duniani. Kwa hiyo mafuriko tunayopata hapa nchini na kwingineko ulimwenguni ni matukio ya kijiografia kutokana na msongamano wa hewa huko angani.
Hili la barabara ya Dar es Salaam-Lindi mimi niliona kama limesababishwa na sisi binadamu wenyewe kwa kule kutokuwajibika ipasavyo.
Hata Mwenyezi Mungu alisema kwa babu zetu zamani za kale. Tunasoma maneno haya “…kwa mawazo ya moyo wa mwanadamu ni mabaya tangu ujana wake…. (Mw: 8:21). Serikali yetu na hasa watendaji wake ndiyo wa kulaumiwa katika barabara hii ya Dar es Salaam-Lindi.
Kwa nini nasema hivyo? Wengi nadhani tunakumbuka tarehe 2 Agosti 2003 lilipozinduliwa au lilipofunguliwa rasmi lile DARAJA LA MKAPA pale Rufiji. Sisi wa mikoa ya Kusini ya Lindi, Mtwara na hata Ruvuma tulialikwa kushuhudia tukio lile pale Rufiji.
Lilikuwa ni tukio kubwa na la kihistoria. Baada ya hotuba ya Rais Benjamin Mkapa na maelezo ya kutumainisha sana ya John Phombe Magufuli, Waziri mhusika na barabara, tulisema “KUSINI HOYEE! UKOMBOZI leo umepatikana”.
Wayao nakumbuka walicheza na kuimba, “Watiteje ngaika, daraja liiche lelo” yaani walikuwa wanasema halitafika, daraja leo limefika, wakaendelea kusema kwa Kiyao tena “wanya wa watukombwele sambano” yaani jamani hawa wametukomboa sasa sisi wa kusini.
Cha kutuaminisha ni matamshi yale ya Magufuli yaliyosema “kuanzia sasa mtu anaweza kusafiri kwa gari katika barabara ya lami kuanzia Mtwara mpaka Mwanza”. Tukaitikia asante sana, Serikali ya CCM idumu. Uchumi wa kusini sasa utapanda. Tulijaa jazba ya furaha. Ieleweke jamani sisi tulikuwa tunasafiri kwa Teeteeco (Titikoo).
Hii ilikuwa ni kampuni ya Wahindi ya mabasi ya usafiri mikoa ya kusini kutoka Lindi kuja Dar es Salaam kwa muda wa siku 2 enzi hizo. Ukitoka Lindi utalala Kilwa Kivinje, siku ya pili ukitoka Kilwa kupitia Utete ndiyo tunafika hapa Dar saa 2 usiku. Sasa kwa daraja hili la Mkapa mbona mambo yamekuwa poa kabisa?
Ni saa 8 tu kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam. He, juzi juzi tunaona kwenye runinga, katika taarifa ya habari eti mawasiliano kati ya Dar es Salaam na mikoa ya kusini ya Lindi na Mtwara yamekatika.
Magari zaidi ya 100 yamekwama kati ya Mhoro na Somanga. Abiria zaidi ya 2,000 wakiwamo wanawake na watoto wamekwama huko.
Runinga ilionesha abiria wenye kubeba vifurushi vyao vichwani na watoto wadogo wanatembea kwenye matope. Magari yamenasa kwenye tope na lambo zima la maji linaonekana. Hapakuonekana aina ya barabara pale.
Hii mimi naita adha kubwa. Ni kero ya kutengenezwa na binadamu wala siyo tukio la kuletwa na Mungu (man-made disaster but not a natural disaster!). Serikali ya CCM ikagutuka, Naibu Waziri Greyson Lwenge (Mbunge) anayehusika na mabarabara akaonekana kwenye runinga akitembea kwa miguu mwenye matope.
Tulifarijika kwa matamko yake kuwa yuko na wahandisi na zana kamili kama vijiko/magreda ya kuvuta magari yaliyonasa katika matope na akaahidi kuwa hatoki pale eneo la maafa mpaka kieleweke!
Hongera sana waziri, tuokoe wakazi wa kusini. Kwa ndugu zangu wasiojua barabara hii ningewaelimisha kidogo kwa kusema mahali pale ni eneo la Muhoro ni mpakani mwa Mkoa wa Pwani na Mkoa wa Lindi Wilaya za Rufiji (Utete) na Kilwa (mkoa wa Lindi).
Barabara hii kuu ya kutoka Dar es Salaam mpaka Mtwara karibu asilimia 98 imeshatiwa lami. Yaani kutoka Dar es Salaam mpaka mahali penye ulambo wa matope Waingereza wanaita swampy area, sisi Wangoni tunaita pa litapwasi, panaitwa Malendego ni lami tupu kilometa 221 kutoka hapa Dar es Salaam.
Na ukitokea kule Mtwara ni lami tupu kilometa 335 mpaka Somanga. Kumbe kipande korofi hicho kinachoifedhehesha Serikali ya CCM ni kilometa 14 tu!
Hebu fikirieni tangu mwaka 2003 mpaka leo ni miaka 10 kamili — Serikali imeshindwaje kukamilisha lami ulambo korofi huo? Haieleweki na wala haielezeki. Kila mwaka Serikali inajigamba imejenga barabara za lami hapa nchini urefu wa kilometa maelfu kadhaa.
Na mwaka huu wa fedha 2014/2015 zimetengwa milioni kadhaa kwa mabarabara kule Kigoma, Kilombero na kwingineko. Hii ya Dar es Salaam-Lindi kilometa 14 ikasahauliwa.
Hili linatokeaje? Kweli hakuna fedha za kutia lami kilometa 14 tu lakini zipo fedha za kujenga barabara mpya maelfu ya kilometa hapa nchini.
Je, inaingia akilini hilo? Wa kusini tumekosa nini hata tusahaulike namna hiyo? Mimi siamini ila nasema ni makusudi na ikiwa hivyo basi zipo sababu maalum.
Mungu si Athumani, ameiumbua Serikali kwa kuleta mafuriko. Ninaamini wameliona tatizo hili (glaring fact) na sasa Serikali haitalifumbia macho tena tatizo hili. Kiporo cha miaka 10 kweli kinalika? Si kila waziri alipasahau hapo ndiyo maana Naibu Waziri wa barabara akasema hatoki mtu pale mpaka kieleweke.
Ubovu huu wa kipande cha barabara ni UZEMBE wa mwanadamu kama vile uzembe wa daktari kusahau forceps tumboni mwa mgonjwa baada ya operesheni.
Inagharimu sana kuitoa forceps (mikasi) ile maana ni lazima mgonjwa yule apasuliwe tena – ni operesheni ya pili. Vivyo hivyo ujenzi wa barabara ya Dar es Salaam-Lindi wamekisahau kile kipande cha kilometa 14 kwa miaka kadhaa, leo hii kukimaliza kitaigharimu Serikali mamilioni ya shilingi.
Kumbe wangekamilisha wakati ule ule walipofungua daraja la Mkapa, leo wa kusini tungekuwa tunawapa pole wenzetu wa Kilombero, Kyela, Kilosa, Mpwapwa na kadhalika.
Kusini sijui tuna balaa gani au mkosi gani! Enzi za ukoloni Mwingereza aliweka hata katika General Orders zake section G.8 kuwa wakati wa masika watumishi wa Serikali wapewe tiketi za ndege kwenda makao makuu ya mikoa ya kusini enzi zile ilikuwa ni Lindi na Songea (sasa Ruvuma).
Mimi nimewahi kuruka kwa ndege enzi hizo kutokana na General Orders section hiyo. Hii inadhihirisha tatizo la usafiri wa barabara mikoa ya kusini ni la miaka nenda rudi. Ni donda ndugu lisilopona mpaka leo miaka 53 baada ya Uhuru wetu.
Kuna mwaka fulani enzi za ile Serikali ya Awamu ya Tatu ya Che Mkapa. Ili kupunguza adha kwa wasafiri wa kusini, Serikali iliwahi kukodisha ile meli kubwa ikiitwa Santorini kutoka Ulaya. Siku limezindua safari yake ya kwanza hapa Bandarini Dar es Salaam, wa kusini tuliongozwa na mmoja wa mawaziri kutoka Lindi.
Pale Bandarini Dar es Salaam, wa kusini walionesha kila aina ya furaha. Zilichezwa ngoma za Sindimba, Msolopa, Lijole na kadhalika. Nakumbuka waziri akigalagala sakafuni. Wakati anapiga ngoma pale. Sisi wa kusini tuliita meli ile au tuliibatiza kwa jina la Kusini hasa tukaita Nakumbwa maana yake pakia pakia. Ilipakia mamia ya watu kwa kila safari. Huo ulikuwa ukombozi pia kwa wa kusini.
Kufumba na kufumbua limeli lile limetoweka, lahaula, tukabakia wasemavyo Waingereza back to square one yaani tukarudia kule kule kwenye barabara isiyomalizika hii ya Dar es Salaam-Lindi mpaka leo.
Kuna utani nimeletewa katika facebook kutoka Uingereza wananiuliza swali “on which side of the road do you drive if you want to go to Lindi? Kwa kawaida magari huendeshwa upande wa kushoto kama wafanyavyo Uingereza (UK na Commonwealth) na sisi hapa Tanzania au huendesha upande wa kulia kama wafanyavyo Bara Yuropa (continental Europe) au Wanyarwanda na Congo.
Basi kijana mmoja huko huko Uingereza akajibu “in Southern Tanzania people drive on either side of the road depending on the passability of the particular road” yaani kule Kusini gari linaendeshwa upande wowote ule unaopitika katika barabara!
Hapo mimi niliachwa hoi, maana magari yaliyonasa pale Muhoro sehemu yenye tope yalionekana kutapakaa kila mahali, hapakuwa la kushoto wala la kulia mradi dereva ajikwamue. Vijembe namna hii ninaamini Serikali itavimaliza na magari yatafuata utaratibu wa kuendesha kushoto kama ilivyo kawaida yetu.
Swali muhimu hapa kwa wizara ni je, baada ya kuumbuliwa na mvua hizi kule kusini mtamaliza lini kutia lami zile kilometa 14? Ni kweli sasa mtu anaweza kusafiri kwa gari kutoka Mtwara hadi Mwanza katika barabara ya lami hata pale Somanga-Nyamwage? Jamani, Serikali ilivalie njuga hili tatizo la barabara. Km 14 tu kweli zinaweza kutufedhehesha hivi?
Waziri Magufuli ulipokuwa JKT Makutopora ulidhihirisha ushupavu wako mkubwa kwenye mitaro ya mizabibu. Hebu sasa tunisha tena msuli kwenye kutia lami hizo km 14 za barabara pale Muhoro-Somanga, tuondolee matope yale nasi wa kusini tujue askari wa miamvuli amegangamala – hakuna kulala njiani tena Dar-Lindi waaa!