Na Alex Kazenga Jamhuri Media, Dar es Salaam
Ifikapo 2030 serikali imepania asilimia 10 ya pato la taifa itokane na uzalishaji unaofanyika kwenye kilimo.
Rais Samia Suluhu Hassan, amebainisha nia hiyo leo Septemba 07, 2023 wakati akiwahutubia vijana waliohudhuria moja ya mikutano ya Jukwaa la Mifumo ya Chakula Afrika (AGRF-2023) unaoendelea katika kituo cha Kimataifa cha mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.
“Serikali imekaa na kujadili namna ya kuwawezesha vijana kimaisha; kupitia Mpango wa Build a Better Tomorrow (BBT) tunawahamasisha vijana kushiriki kilimo chenye tija,” anasema Rais Samia.
Aidha, akijibu moja ya swali lililoulizwa na kijana mmoja kwenye mkutano huo Rais Samia amesema, kutotambua mahitaji ya soko la bidhaa za ndani na nje ya nchi ni changamoto inayowakabili wakulima wengi.
Amesema, changamoto hiyo,inachochewa na kutokuwapo kwa muunganiko kati ya soko na mkulima wenyewe na kwamba moja ya jitihada za serikali katika kuiondoa imefanikiwa kuanzisha vyama vya ushirika ambavyo huwaunganisha wakulima kwenye masoko ya bidhaa wanazozalisha.
Rais Samia anakiri vyama vya ushirika vya wakulima vya kununua mazao hasa korosho kuwa vimetoa fursa ya kuwapo kwa ushindani wa bei.
“Zao la korosho limeonyesha matokeo chanya kwa kupandisha bei, tumemsaidia mkulima kwa kumjengea ushirika wa moja kwa moja wa soko kwa kuondoa mtu wa kati,” amesema
Na kwamba hata kwenye zao la mbaazi nako matunda yameonekana ambapo anasema awali wakulima waliuza mbaazi kwa bei ya chini lakini baada ya kuwapanga wakulima na kuwapatia soko zao hilo limepanda hadi kufikia kilo kuuzwa Sh 2000.
Aidha, Rais Samia ameweka wazi kuwa serikali inafanya jitihada kujenga barabara za wilaya na mikoa kusaidia mazao ya mkulima kutoka shambani kwa urahisi ikiwa ni pamoja na kujenga barabara kuu zinazounganisha nchi na mataifa jirani ili kuyafikia masoko ya mataifa hayo.
Pia, kupitia uchumi wa bluu amesema bandari zote zinatengenezwa ili ziweze kupokea mizigo sambamba hilo anasema serikali imenunua ndege ya mizigo itakayorahisisha usafirishaji wa mazao yanayohitajiwa kwa wingi kwenye soko la dunia lakini yanaharibika kwa haraka.
“Bandarini nako kunajengwa ‘Green Belt’ hii nayo itausaidia kutunza mazao yanayoharibika haraka,” anasema.
Akijibu swali la kijana mwingine kwenye mkutano huo, Rais Samia anasema suala la matumizi ya teknolojia kwenye shughuli za kilimo kwa sasa haliepukiki.
Anasema kwa kuzingatia hilo serikali imewekeza kwenye tafiti mbalimbali hasa za udongo kujua afya ya udongo, eneo la kila mkulima pamoja na kumsajili.
Sambamba na hilo, amesema ifikapo mwaka 2025 serikali inalenga robo tatu ya mbegu za kisasa zitazotumiwa na wakulima ziwe zinazalishwa na vituo vya tafiti za serikali na binafsi vilivyopo nchini.