Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam
KAMPUNI ya Kili MediAir imesema kuwa pamoja na kutoa huduma ya Uokozi kwa watalii pia inafanya utalii wa anga.
Hayo yameelezwa leo Oktoba 12, 2024 na Daktari wa Uokozi kutoka Kampuni hiyo, Jimmy Daniel kwenye Onesho la 8 la Utalii la Kimataifa la Kiswahili( S!TE 2024) linalofanyika katika ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam.
Amesema moja ya changamoto wanayokabiliana nayo ni watu wengi wanajua kuwa huduma yao ni uokozi tu hivyo wanaendelea kutoa elimu wananchi kuwa wanafanya na utalii wa anga.
“Sisi tunajihusisha na uokozi kwa njia ya anga kwa kutumia Helkopta, lakini pia kwa njia ya ardhini ambapo tunakupa daktari pamoja na mtu wa kuwa na wewe unapofanya safari zako katika Mlima Kilimanjaro.
“Lakini nje ya hapo tumejidhatiti sasa hivi tumetengeza wigo kwamba hatufanyi tu uokozi bali Utalii wa anga. Kwamba tunakutana na watu wanatamani kuweza kufanya utalii mfano katika Mlima Kilimanjaro lakini kwaajili ya umri au maradhi wanashindwa,” amesema na kuongeza:
“Kwahiyo sisi tumekuja na kifurushi hiki cha Utalii wa ambapo itamsaidia mtalii aweze kufika ajionee mwenyewe kwa kutumia Helkopta,”.
Aidha amesema kampuni hiyo inajishughulisha na usalama wa watalii katika vivutio na kwa sasa imejikita zaidi Kaskazini huku wakiwa na malengo ya kufikia vivutio vyote nchini.