Misimamo mikali ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, kwenye masuala yenye utata mkubwa inatajwa kama sababu kubwa ya Marekani kumwekea vikwazo vya kusafiri kwenda kwenye nchi hiyo kubwa kiuchumi na kijeshi duniani.
Wiki iliyopita taarifa iliyotolewa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Mike Pompeo, ilisema kuwa makonda pamoja na mke wake wamezuiliwa kuingia nchini humo.
Taarifa hivyo iliorodhesha sababu kadhaa za uamuzi huo lakini ikizitaja kwa jumla jumla kama vile ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu na kukandamiza wapinzani. Taarifa hiyo inabainisha kuwa vikwazo dhidi ya Makonda vimewekwa kwa mujibu wa Kifungu cha 7031(c) cha Sheria ya masuala ya programu za mambo ya nje.
Ikifafanua, taarifa hiyo inabainisha kuwa uvunjifu wa haki za binadamu wa Makonda unatokana na hatua ya kiongozi huyo kuzuia haki ya watu kuishi, uhuru wa watu au usalama wao.
“Wizara ina taarifa za uhakika kuwa Makonda alihusika na ukiukwaji huo akiwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam. Katika wadhifa huo, amekwisha kuhusishwa na matukio ya kukandamizwa kwa wapinzani wa kisiasa, kuzuia haki ya watu kutoa maoni yao na kukusanyika, kuwakandamiza watu waliotengwa na hivyo kufanya maisha kuwa magumu,” inaeleza taarifa hiyo.
Wakati taarifa ya Marekani ikitaja tuhuma hizo kwa ujumla wake, uchambuzi wa JAMHURI unaonyesha kuwa moja ya sababu kubwa ambazo zimesababisha Marekani kumwekea vikwazo vya kusafiri Makonda ni msimamo wa mwanasiasa huyo kijana kuhusiana na suala ya ushoga na ndoa za jinsi moja.
Oktoba mwaka juzi Makonda aligusa masilahi ya nchi nyingi duniani kufuatia hatua yake ya kushughulikia watu wanaojihusisha na mapenzi ya jinsi moja. Aliunda kamati maalumu kwa ajili ya kuwasaka watu hao na kuhakikisha wanachukuliwa hatua za kisheria.
Kamati hiyo pia iliagizwa kuwashughulikia mashoga wanaojitangaza na wasiojitangaza, lakini wanajulikana kuwa ni mashoga. Aidha, kamati ilipewa maelekezo kuwashughulikia watu wanaotengeneza picha au video za ngono.
Makonda alitoa amri kwa wakazi wa mkoa wake kuhakikisha kuwa wanafuta picha zote za ngono kwenye simu zao za viganjani.
Tangazo hilo lilijibiwa na Ubalozi wa Marekani ambao ulisema katika taarifa yake kuwa kitendo hicho ni cha kibaguzi, kwani kinaminya haki za watu wengine.
Hata hivyo, hilo halikumtikisa Makonda ambaye alitoa onyo kwa mashirika ya haki za binadamu kuwa Tanzania ina tamaduni zake na ushoga ni kesi ya jinai kwa mujibu wa Kifungu cha 154, ambacho kinasema mtu yeyote ambaye anamuingilia mtu yeyote kinyume cha maumbile au, anamuingilia mnyama kimwili au anamruhusu mwanamume kumuingilia yeye mwanamume au mwanamke kinyume cha maumbile, atakuwa ametenda kosa, na atawajibika kwa adhabu ya kifungo cha maisha na wakati mwingine kifungo kisichopungua miaka thelathini.
Tukio jingine ambalo lilimhusisha Makonda ambalo liliibua hisia za watu wengi ni kuingia kwake kwa nguvu kwenye studio za Clouds Media na kulazimisha kurushwa kwa kipindi ambacho kilikuwa hakijapitiwa na kituo hicho.
Tukio hilo la aina yake lilitokea Machi 2017. Video zinazomwonyesha Makonda akiwa ameandamana na watu wenye silaha wakiwa wanaingia kwa nguvu katika kituo hicho zilisambaa mitandaoni. Tukio hilo lililaaniwa na watu wengi.
Aliyekuwa Waziri wa Habari, Nape Nnauye, aliunda kamati kushughulikia suala hilo lakini ripoti ya kamati hiyo ilipotolewa hadharani Nape alifutwa kazi kama waziri na siku chache baadaye akanusurika kuuawa na mtu aliyemwonyesha bastola katika eneo la Oysterbay ambako Nape alipanga kukutana na waandishi wa habari.
Makonda pia anahusishwa na kuondolewa kwa aliyekuwa Meya wa Dar es Salaam kwa tiketi ya Chadema, Isaya Mwita, ambaye hivi karibuni alipigiwa kura ya kutokuwa na imani naye na madiwani wenzake.
Marekani inaeleza katika taarifa yake kuwa pamoja na Makonda, marufuku hiyo pia inawahusu ndugu zake wa karibu, akiwemo mke wa kiongozi huyo, Mary Felix Massenge.
“Hatia dhidi ya Makonda inaonyesha jinsi hali ya haki za binadamu ilivyozorota nchini Tanzania, pia kuunga kwetu mkono kuwawajibisha wote wanaohusika na ukiukwaji kama huo,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo.