Kupata sifuri kwa asilimia 60 ya wanafunzi wa kidato cha nne mwaka jana, kusitufanye kushangaa kwamba watu hao wakoje. Kila mtu mzima wa Taifa hili ajiruhusu kusailiwa kuhusu yafuatayo:-
Mwili: Kuna meno mangapi kinywani, kila wiki huvuta pumzi mara ngapi, kiwambo na kongosho viko sehemu gani, aliwahi kuhesabu kope (acha nywele) zake akakuta ni ngapi, kila siku anacheka mara ngapi, anapepesa kope mara ngapi kwa siku na mwezi uliopita alikohoa mara ngapi?
Nyumbani: Ana milango na madirisha mangapi, meza na viti vingapi, sufuria na mabakuli mangapi, vijiko vingapi, anamfahamu mwenye nyumba wake na amemwona mara ngapi, ana picha ya babu mzaa baba yake, ukoo wake una watu wangapi na ana picha zao ngapi?
Afya: Kuna mbu wa jinsia ngapi, mbu wa kike ana matiti mangapi, mbu ana miguu mingapi, mabawa mangapi, aina za malaria ni ngapi, dalili za malaria ni zipi, namna ya kuepuka malaria, kifua kikuu ni nini, dalili za kawaida na kuzidiwa na kifua kikuu ni zipi, hatua za kuchukua kama nyumbani kuna mtu mwenye kifua kikuu.
Si hayo tu, lakini athari za vinyesi vya wanyama kwa binadamu hasa wakufuga ni zipi, mguu wa kuku una vidole vingapi, mkoani, wilayani au katani kwake kuna magonjwa hatari mangapi, hospitali na zahanati zipo ngapi, maji yanafaa kunywewa yakiwa baridi au vuguvugu, mwili wa binadamu una nyuzi joto ngapi, asali, alizeti, maziwa, papai vina faida gani kwa afya ya binadamu?
Utaifa: Bendera ya Taifa ina rangi ngapi, uwezo wake wa kuimba wimbo wa Taifa kutoka ubeti wa kwanza hadi wa mwisho, kama ana nakala ya Kiswahili ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 1977, ameisoma mara ngapi na familia yake, nakala zake zinapatikana wapi na kwa bei gani, sheria ambazo zipo katika Kiingereza ametafsiriwa mara ngapi, anajua majina yote ya mbunge wake na diwani wake, Tanzania ina majimbo mangapi ya uchaguzi na kata ngapi, Tanzania ina makabila mangapi, ana kamusi ya Kiswahili na anairejea mara ngapi kwa wiki na anajua angalau methali 20 za Kiswahili?
Rasilimali: Idadi ya watu katika kila mkoa, wilaya na kata hapa Tanzania ni ngapi, milima, maziwa na mito ni mingapi na iko wapi, sifa zake ni zipi, aina za madini na mazao ni ngapi, pamoja na ujinga na umaskini maajabu ya Tanzania ni yapi?
Usafiri: Meli zipo ngapi hapa Tanzania, na ni ngapi zimezama, ajali za treni zimeshatokea mara ngapi, na ndege je?
Kujielimisha: Anasoma magazeti, na ni yapi, katika familia yake wanaosoma magazeti ni nani na mara ngapi na ni yapi, katika mwezi anasikiliza taarifa za habari kwenye radio na TV mara ngapi, ni barabara ngapi mijini Tanzania zinazoitwa Lumumba kuelekea makao ya CCM na ni kwa nini, mitaa mingapi katika kata yake ina majina?
Majengo: Katika mkoa, wilaya au kata yake kuna majengo ya ghorofa mangapi na mangapi yameishaanguka?
Novatus Rweyemamu,
Wakili Mwandamizi
Simu: 0784 312623