Na Isri Mohamed
Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) leo saa moja usiku itashuka dimbani katika uwanja wa Stade Des Martyrs uliopo mjini Kinshasa kuumana na timu ya Taifa ya DR Congo wakiwania tiketi ya kufuzu Afcon mwaka 2025, nchini Morocco.
Kocha wa Stars, Hemed Morocco amesema wachezaji wote aliowahitaji wamewasili na tayari wameshafanya mazoezi na maandalizi ya kutosha kuwakabili wakongo ambao asilimia kubwa ya wachezaji wao wanachezea vilabu vya Ulaya.
Kauli kubwa aliyoitoa Morocco ambayo inatupa moyo na nguvu juu ya timu yetu ni ile ya wachezaji wote kutamani kucheza, yaani kila mchezaji ana kiu ya kushiriki kwenye ushindi wa leo, tena si kushiriki kwa kukaa benchi bali amwage jasho lake kwa dakika angalau hata mbili tu.
Kwa wale wenye hofu juu ya wachezaji wa Congo wengi kuchezea Ulaya, inaonesha wazi wamesahau kuwa tunaye Captain Diego Mbwana Samatta ambaye amewahi kucheza Ulaya na ana uzoefu mkubwa wa mechi za Kimataifa, huku akiwajua vizuri wakongo kwa sababu amewahi pia kuichezea TP Mazembe iliyopo nchini humo.
Uzoefu wa Samatta na wachezaji wengine wanaocheza nje ya Tanzania wakiwemo Himid Mao, Kachwele na Haji Mnoga, pamoja na wale wa ndani ambao wamecheza mechi nyingi za kimataifa kwenye vilabu vyao, unaweza kutusaidia sana kupata ushindi mbele ya Congo.
Kama Watanzania kilichobaki ni kuungana na timu yetu kwa wale waliopo Congo kufika uwanjani kushangilia na kuwapa nguvu wachezaji, na wale waliopo mbali kuiombea kwa dhati kwani hatuna Taifa lingine la kushangilia.
Jamhuri Media tunaungana na Watanzania kuitakia kila la Kheri Taifa Stars, ikiwa inapeperusha bendera yetu huko Congo.