Wiki hii, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli anatarajiwa kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM). Ukiacha ujumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa, ambao aliupata kwa kuwa Mbunge wa Biharamulo Mashariki kabla ya Jimbo hilo kuitwa Chato. Hajapata kugombea nafasi yoyote ya kisiasa ndani ya chama chake.
Rais Magufuli kabla ya kuchaguliwa kuwa Rais, amekuwa waziri kwa miaka 20, akishikilia Wizara ya Ujenzi, Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Uvumi na Maendeleo ya Mifugo (kitoweo). Nazifahamu harakati zilizokuwa zikiendelea ndani ya CCM kuhoji Rais Magufuli asiye na uzoefu wa uongozi wa kisiasa atawezaje kuwa Mwenyekiti wa chama.
Hata Askofu Josephat Gwajima, yupo matatani kwa kutamka maneno ya kuwasuta baadhi ya wana-CCM aliodai kuwa wanataka kufanya mbinu Rais Magufuli asipewe uenyekiti. Naielewa hofu ya baadhi ya wana CCM ikiwa ni kweli walikuwa na mawazo hayo. Wanawaza na kufikiri juu ya waliyoyashuhudia siku chache baada ya Rais Magufuli kushika madaraka.
Sitanii, yapo mambo anayotenda Rais Magufuli kwa yeyote ambaye ni kada mzoefu angefungwa mikono na mfumo ndani ya CCM. Makada, waliokunywa maji ya bendera, hawafanyi uamuzi hadi chama kimeridhia. Taratibu za chama kuridhia, zinaweza kuchukua miaka hata mitano, kutoka mkutano mkuu mmoja hadi mwingine.
Tumeshuhudia Rais Magufuli akifanya mabadiliko makubwa katika mfumo wa utumishi wa umma. Uteuzi alioufanya katika nafasi za Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri (DED) na Makatibu Tawala wa Wilaya (DAS), umedhihirisha kuwa amejipanga kuvunja mfumo wa urasimu. Majipu aliyotumbua ndani ya Serikali, na kauli kwamba ndani ya CCM yapo majipu mengi, inawaogopesha wengi.
CCM inamiliki mali nyingi. Kuna viwanja vingi nchini, majengo na mali nyingi walizojimilikisha watu ambazo ni za chama. Hawa wakisikia Rais Magufuli amepanga kurejesha mali za Waislamu, kwa nini wasipate hofu kuwa atarejesha hata mali za CCM? Ninachofahamu, ni kuwa watenda maovu ndani ya CCM hofu imewatawala.
Sitanii, ukiacha hiyo hofu, wapo wanaosema Rais Magufuli akishika urais na uenyekiti, nchi itawaka moto. Wanahofu nani atamfunga ‘gavana’ kama ilivyotokea wakati wa bomoa bomoa kwa wakazi wa mabondeni. Tulishuhudia walivyofurika wazito Ikulu, akiwamo Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa na Mwenyekiti wa CCM, Jakaya Kikwete.
Wapo wanaosema Rais Magufuli alikuwa na msimamo wa wazi kuwa nyumba zote zilizojengwa katika mita 60 ndani ya bonde kwa maana ya 30 kila upande, ilikuwa lazima zivunjwe. Eti wanasema wakubwa hawa walimweleza kuwa hata Ikulu iko ndani ya mita 30. Sasa wanasema nani atamwambia hayo ikiwa atakuwa Mwenyekiti na Rais? Nasema, sisi vigavana vidogo kupitia vyombo vya habari, tutaifanya kazi hiyo!
Binafsi nasema kwa vyovyote vile, nchi yetu ilifikia hatua mbaya. Tulihitaji kiongozi wa kurejesha maadili. Tulihitaji kiongozi wa kuturejesha kwenye mstari. Tabia ya baadhi ya wafanyabiashara kuchukua nyumba za watu kwa nguvu na kutumia jeuri ya fedha kuwapora watu haki, ililifikisha taifa hili pabaya. Kuheshimiana kulikwisha na fedha ikawa mfalme.
Leo tunashuhdia waliokuwa wanachukua fedha za watu bila kuzifanyia kazi, wameufyata. Baadhi ya hoteli zimegeuka vyuo, nyingine zimegezwa hostali za wanafunzi na nyingi zimesalia kuwa mahame ya popo. Waliokuwa wanachezea fedha na kujaza baa kwa sasa hawapo tena. Jeuri ya nitukane nikupige, nikulipe hatutaiona tena.
Sitanii, naamini Rais Magufuli atatumia fursa hiyo ya kuwa Mwenyekiti na Rais kunyoosha mambo. Hata hivyo, wakati ananyoosha mambo, itapendeza akifahamu kuwa huku mtaani ukata umezidi. Ikiwa anazipata taarifa hizi kuwa hoteli, viwanda, mashirika, kampuni zinafunga biashara si habari njema kwa ustawi wa taifa hili.
Ndoto ya Rais Magufuli kujenga viwanda inategemea ukusanyaji wa kodi. Kodi zinatokana na uzalishaji na uwapo wa viwanda na kampuni na hata hizo hoteli. Kanuni ya kubana matumizi, isiisahau sana kanuni ya kufungulia matumizi kwa ajili ya kuwezesha Watanzania kumiliki hivyo viwanda. Ikiwa atabana kila kona wengi wakarudi nyumbani bila kuwawezesha kupata fursa mpya, hali itakuwa ngumu kwa familia nyingi.
Tayari zipo familia zilizoanza kula mlo mmoja kwa siku. Nakupongeza kwa hatua hii ya nafasi ya juu kabisa uliyoishika, ila pitia majadala uone Mwalimu Julius Nyerere, Ali Hassan Mwinyi, Rais Bejamin Mkapa na Jakaya Kikwete walifanyaje kuiweka nchi katika mazingira ambayo angalau watu walifanya kazi, lakini kipato kikawapo mifukoni mwao. Mungu ibariki Tanzania.