Heri ya mwaka mpya wa 2013 wana-JAMHURI wenzangu, hongera na poleni kwa machovu yote.

Najua sana wengine ndiyo wanaangalia tena salio kwenye akaunti zao, kwenye waleti na chenji kwenye watoto wa meza nyumbani na ofisini.

Baadhi ndiyo kwanza wanafikiria kama ilikuwa lazima kwenda sehemu kama Mwanza (na Bukoba) na kurudi kwa ndege kutoka Dar yaliko makazi yao.

 

Ada za watoto zinahitajika, wengine wanadaiwa za mwaka jana na waliahidi wangemalizia mwaka huu, kibaya zaidi kuna pango la nyumba na madeni ya umeme na maji. Ndizo changamoto za mwanzo wa mwaka, huwezi kusema ni matatizo, bali ni maisha, ukipenda sema kila kukiacha heri ya jana.

 

Nikwambie tu mwana-JAMHURI mwenzangu wewe unayesoma makala haya kwamba hayo ni maisha ya karibu kila mahali; si Tanzania au Afrika Mashariki tu, nikwambie sasa hapa Uingereza watu wazima wanalia machozi mazito.

 

Hapa kinachoumua hisia za watu ni kupandishwa kwa gharama za usafiri wa treni. Ni kweli hili huwa linakuja karibu kila mwaka, lakini baada ya matatizo makubwa ya kwenye uchumi, mfumko wa bei na kuanguka kipato mwaka jana, wadau walitarajia iwe tofauti.

 

Lakini jamaa hawakukawiza bwana, kabla watu hawajasherehekea Mwaka Mpya, tayari mipango imeshakamilika, na tarehe 2 Januari tulianza kulia machozi.

 

Kwa wastani nauli zimeongezwa kwa asilimia 4.2. Hiki ni kiasi kikubwa maana watu watatoa wapi hizo pesa? Mwaka uliopita mishahara haikupandishwa vizuri, nikwambie kima cha chini hakikupandishwa kufikia hata paundi moja.

 

Halafu kwa mwaka huu nauli ya usafiri ambao hutumiwa na watu wengi wa madaraja karibu yote, imepanda karibu mara tatu ya wastani wa kipato cha wastani tangu mwaka 2008.

 

Hapo serikali inasema watu wasilie sana, kwa sababu iliingilia kati na kuwalazimisha wahusika wasipandishe nauli zaidi ya asilimia nne. Kwa wale watu wa hali ya juu kidogo kimaisha hawana tatizo, kwa sababu au mishahara yao au kipato kinawaruhusu kulipa bila matatizo.

 

Tatizo linagomba hapa kwa watu wa hali ya chini, hasa vijana, kwa sababu kadiri muda unavyokwenda vijana wengi hawana kazi. Wenye kazi hazilipi vizuri na wamekuwa wakikimbilia usafiri wa treni kuwafikisha na kuwarudisha kazini au kwenye mitikasi mingine.

 

Wanaweza kuwa wamebahatika kununua ‘kausafiri’, lakini kwa mtindo wa hapa, bima za vijana na madereva wapya ni juu sana, wakati madereva wazoefu bima yao ni kiduchu kabisa.

 

Sasa utaona kwamba vijana hawa, watu wasio na uzoefu kuendesha na watu wa hali ya chini wamekimbilia treni ambazo nauli haijawahi kuwa rahisi, lakini sasa wanaongeza zaidi.

 

Wamepita watu hospitalini kwetu wanalia, wanasema sasa ni matatizo matupu, kwa sababu bei ya nauli ni kubwa na kila kukicha afadhali ya jana.

 

Nani alisema huku mtoni kuwa watu wanaponda raha? Ni mateso ya milima nakwambia. Heri ya Mwaka Mpya, hongera na kuponda raha ya Krismasi hapo Bongo.

 

[email protected]