jakaya kikwete

jakaya kikwete

Rais Jakaya Kikwete, wiki ijayo atakuwa ameingia kwenye orodha ya marais wastaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kwa kiongozi aliyechaguliwa mara mbili, na kufanikiwa kumaliza kipindi chake cha miaka 10 salama, si busara sana kuendelea kumjadili au kumkosoa.

Watu waungwana wangependa kumwona kiongozi wetu anapumzika salama; na kwa maana hiyo ushauri wetu unapaswa kuelekeza kwa huyo anayekuja.

Hata hivyo, yapo mambo ambayo nafsi inashindwa kuvumilia kuyaona; ndiyo maana nimeona pamoja na heshima kubwa kwa Mheshimiwa Kikwete, ebu basi tumkosoe kwa hili- matarajio yakiwa ni kuona huyo anayekuja hayarejei haya yaliyofanywa na mtangulizi wake.

Rais Kikwete siku zake za mwisho mwisho kwenye uongozi amekuwa akifanya uteuzi na wakati mwingine akiwabadili vituo vya kazi baadhi ya viongozi na watumishi.

Katiba inatamka wazi ukomo wa madaraka ya Rais aliye madarakani; na mwanzo wa madaraka ya kuongoza nchi kwa Rais Mteule. Hilo halina ubishi. Ni kwa nguvu hizo hizo za kikatiba zinazompa mamlaka Rais aliye madarakani kuendelea na uteuzi hata akiwa Uwanja wa Taifa/Uwanja wa Uhuru akipigiwa wimbo wa Taifa na kukagua gwaride la mwisho!

Kwa maneno mengine ni kwamba Rais anaweza kufanya mabadiliko ya Baraza la Mawaziri wakati gari la kumpeleka Uwanja wa Taifa/Uwanja wa Uhuru likiwa tayari kumpeleka kwenye sherehe za kuapishwa Rais mpya!

Pamoja na ukweli huo wa nguvu za kimamlaka anazozipata Kikatiba, bado busara inaweza kumwelekeza asifanye kituko cha aina hiyo! Nasisitiza kuwa ni busara tu inayoweza kumsukuma kuacha kuendelea kuteua dakika za majeruhi!

Anaweza kuona kitendo cha kuteua Baraza jipya la mawaziri zikiwa zimesalia dakika kadhaa kabla ya kung’atuka si cha busara, na akaacha kufanya hivyo; ingawa kikatiba anajua yuko sahihi.

Rais wetu ameendelea kuwateua viongozi wengi na kuwahamisha wengine katika namna inayoibua maswali mengi. Wapo wanaosema anatoa asante ya mwisho mwisho. Wapo wanaodhani anajiandalia mazingira mazuri ya kukumbukwa akiwa ameshastaafu. Yanasemwa mengi, alimradi kila mmoja ana lake.

Kwa namna ya pekee, kuna wakuu wa wilaya walioweza kuwa wakuu wa wilaya tatu ndani ya muda usiozidi miezi mitatu! Hili jambo linaweza kuonekana jepesi, lakini ni mzigo kwa walipakodi wa Tanzania. Kuna wakuu wa mikoa ambao wamedumu katika mikoa kwa muda usiozidi miezi miwili, akawahamisha. Bado inawawia vigumu wananchi kupata au kujua sababu za msingi zinazomsukuma Rais kufanya uteuzi huu. Hitimisho la wengi kwenye uteuzi huu ni kuwa anafanya hivyo kulipa fadhila au kuwapendelea wale anaodhani watakuwa na manufaa kwake baada ya kuanza maisha mapya.

Ameteua viongozi kwenye vyombo vya ulinzi na usalama. Kwa sasa tuna makamishina na majenerali wengi kuliko wakati wowote ule. Ndiyo, inawezekana majeshi yetu yanakua na kwa hiyo sharti wawepo makamanda wengi, lakini si kweli kwamba ukuaji huo unapaswa uendane na hali yetu ya kiuchumi? Kuwahudumia hawa makamishina na majenerali ni mzigo mkubwa kwa walipakodi wa nchi hii.

Ameteua viongozi katika mhimili wa Mahakama, mashirika ya umma, mabalozi na mwishoni mwa wiki iliyopita aliteua makatibu wakuu, naibu makatibu wakuu, makatibu tawala; na akafanya uhamisho wa hapa na pale.

Rais Kikwete ni aina ya kiongozi asiyependa lawama. Mara zote ametaka awafurahishe wengi kadri anavyoweza. Yawezekana wapo waliopata uteuzi kwa sababu wameomba, na kwa kuwa hapendi lawama, naye akaona awafurahishe. Hili linawezekana kwa sababu katika hali ya kawaida ni vigumu kujua hasa sababu ya DC mmoja kuhamishwa wilaya tatu ndani ya miezi isiyozidi mitatu! Je, inawezekana ni kwa sababu DC fulani anakuwa hakufurahia kupelekwa wilaya fulani?

Uteuzi tu si jambo la kuumiza vichwa. Jambo la kujadiliwa zaidi kwenye uteuzi huu ni aina ya baadhi ya hao anaowateua.

Wapo wengi, lakini kuna mtu anaitwa Madeni Kipande. Huyu alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA). Huyu mambo aliyoyafanya TPA ni mengi na mabaya. Chini ya uongozi wake TPA iliyumba. Alikuwa mmoja wa viongozi waliotumia madaraka yao vibaya kabisa. Kuna magunia ya nyaraka za kuthibitisha hilo. Gazeti la JAMHURI limefichua maovu mengi ya Kipande. Ushahidi wa yote hayo upo. Habari zake mbaya zimeandikwa kwa wino mwepesi na mzito! Huyu mtu alithibitika kutokuwa na sifa zozote zile za kuliongoza Shirika kubwa kama TPA ambalo ni lango la uchumi wa Taifa letu.

Waziri wa Uchukuzi, Samwel Sitta, akamwona hafai. Akamwondoa TPA.  Watanzania wakadhani sasa watapumua. Rais Kikwete, ameona njia pekee ya “kuwaenzi” Watanzania, na zawadi murua ya kuwaachia ni kumpeleka huyu mtu Mkoa wa Katavi kuwa Katibu Tawala wa Mkoa huo. Mtu aliyefeli Bandari, badala ya kupumzishwa, anapewa madaraka mengine makubwa.

Kwa umri wake, Kipande anapaswa kustaafu kwa mujibu wa sheria Mei mwakani. Je, hakuna kijana wa kumpa kazi hii badala yake?

Ukijaribu kutumia akili ya kawaida kutafakari vigezo vilivyotumiwa na Mheshimiwa Rais kumteua huyu bwana, huvipati. Unaweza kuishia kwenye yale yanayosemwa mitaani kwamba huyu mtu ni ndugu yake kwa hiyo ameona asimwache hivi hivi. Kwanini isiaminike kuwa kigezo cha undugunaizesheni ndiyo uliotumika hapa?

Hapa ndipo kiongozi kama Dk. John Magufuli, anaposubiriwa kwa shauku kubwa. Katika mikutano yake mingi ya kampeni, Dk. Magufuli hakuficha kutamka wazi kuwa chini ya uongozi wake, mtumishi wa umma atakayevurunda sehemu moja hatahamishiwa kwingine! Kwake yeye, mtumishi wa aina hiyo dawa yake ni kufukuzwa tu! Wapo wasomi tele wa kujaza nafasi hizo. Naandika makala hii wakati kura zikiendelea kuhesabiwa. Endapo Dk. Magufuli, atapata ridhaa ya kushika urais wa nchi hii, huu ni miongoni mwa mitihani ya awali kabisa ambayo Watanzania wanasubiri kuona majawabu yake kutoka kwa Dk. Magufuli.

Kama ni masuala ya sifa, Kipande si kiongozi wa kupewa tena uongozi wa aina aliyopewa, tena dakika hizi za mwisho mwisho.

Uteuzi mwingine uliostaajabisha ni huu wa wakuu wa wilaya na mikoa waliofeli kwenye kura za maoni. Kweli, inawezekana mtu kukosa kupitishwa kwenye kura za maoni hakuna maana kwamba hafai kuongoza. Hata hivyo, hapa ni suala la saikolojia tu ya kibinadamu. Binadamu inamwia vigumu kuiona thamani na umahiri wa kupelekewa Mkuu wa Wilaya ambaye ni zao la kushindwa kwenye kura za maoni!

Watu wanajua huyo mtu amekataliwa na wananchi kwenye jimbo lake, ghafla huyo aliyeketaliwa anapelekwa kuwaongoza wengine katika wilaya au mkoa. Saikolojia ya kawaida inakataa kukubaliana na uteuzi wa aina hiyo.

Kibaya zaidi, uteuzi wenyewe unafanywa ndani ya wiki mbili baada ya mhusika kubwagwa kwenye hizo kura. Hili hawalikubari, na kwa kweli kama Rais halielewi, ni kwamba wananchi wanalipokea kwa chuki. Haya ndiyo mambo yanayowafanya wananchi wakichukie Chama Cha Mapinduzi, maana maswali yao huwa ya aina hii: “Ameona sisi ndiyo tunaostahili kuletewa aliyekataliwa kwao?; Nchi hii haina vijana wengine wasomi wa kuwapa u-DC au u-RC isipokuwa hawa hawa tu wanaokataliwa?”

Dosari nyingine iliyoonekana wakati wa uongozi wa Rais Kikwete, ni kuwarundikia madaraka watu wachache. Mbunge mwenye jimbo anakuwa Mkuu wa Wilaya au anakuwa Mkuu wa Wilaya kwa wakati mmoja. Lini huyu DC au RC atakuwa na muda wa kutosha wa kulitumikia jimbo lake na wakati huo huo kuutumikia mkoa anaouongoza?

Mwaka 2007 kijana mwanafunzi alikuwa miongoni mwa wananchi waliohudhuria mkutano wa hadhara uliohutubiwa na Waziri Mkuu wa wakati huo, Edward Lowassa, katika viwanja vya Shule ya Sekondari Pius Msekwa mjini Ukerewe.

Lowassa alikuwa na utaratibu wa kuwapa wananchi fursa ya kumuuliza maswali. Mwanafunzi huyo akiwa karibu na meza kuu, akamuuliza Lowassa: “Mheshimiwa Waziri Mkuu, mnasema sisi vijana tusome ili tuwe viongozi wa kesho wa Taifa letu. Je, tutawezaje kusoma kama ninyi wenyewe-mtu mmoja anapewa vyeo vingi? Kwa mfano, huyo hapo ni Mkuu wa Mkoa wa Mwanza na ni Mbunge, je sisi tutapaje uongozi?”

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza kwa wakati huo alikuwa Dk. James Msekela; na pia alikuwa Mbunge wa Uyui kutoka Mkoa wa Tabora.

Kwa hakika Mheshimiwa Lowassa alikosa majibu kwa swali la huyo mwanafunzi. Hadi leo sidhani kama kijana alishapata majibu.

Mola akipenda, wiki ijayo tunaweza kuwa na Rais wa Awamu ya Tano. Huyo anayekuja ajitahidi kufungua masikio na kwa msaada wa wasaidizi wake waadilifu aweze kupokea ushauri wa yale mema yenye kuleta manufaa kwa Taifa letu.

Kwa miaka 10 ya uongozi wa Rais Mstaafu mtarajiwa, tumeandika mambo mengi yenye kulenga kuliokoa Taifa letu, lakini kwa namna ya kipekee tumepuuzwa na kuonekana tuna husda au ghiliba.

Wapo mawaziri majangili ambao tumediriki kuanika uhuni wao, lakini bwana mkubwa ameziba masikio na kuhakikisha anang’atuka nao! Sasa ndiyo hao wanaohaha usiku na mchana wakitaka endapo Dk. Magufuli ataingia Ikulu, awakumbuke. Wanajitahidi kuonyesha au kutoa aina zote za ushirikiano ili wasiachwe.

Nihitimishe kwa kumshauri Rais anayekuja kwamba uteuzi huu uliofanywa na Rais Kikwete dakika za lala salama unapaswa utazamwe upya kwa lengo la kuwaondoa baadhi ya viongozi ambao kwa ushahidi ulio wazi tunajua hawafai hata kidogo.

Watanzania wanaotaka mabadiliko hawawezi kuyaona au kuyapata endapo wataendelea kushuhudia aina ya uongozi na viongozi wabovu ambao kwa ujasiri mkubwa, Rais Kikwete, amehakikisha anawapa nafasi.

Haya tunayoyasema au kuyaandika ndiyo yanayojadiliwa mitaani. Wananchi wanakosa imani na Serikali kwa sababu wanaona kuna viongozi wasiofaa. Kuendelea kuwapa uongozi watu aina ya Kipande hakuna tafsiri nyingine, isipokuwa ni kuwaona Watanzania ni mambumbumbu. Kwa kuwakomoa wanaolalamikia uteuzi huu, haitashangaza kusikia uteuzi mwingine mkubwa ukifanywa na Rais Kikwete, wiki hii na wiki ijayo. Yupo msomaji mmoja kasema ukiona hukupata cheo katika Serikali ya huyu bwana, basi ujue unahitaji maombi maalum!