Wiki iliyopita yametokea maandamano mjini Mtwara. Maandamano haya kwa yeyote anayeyaangalia kwa jicho la kawaida yalikuwa na nia njema. Yalilenga kuwapa fursa Watanzania wenyeji wa Mkoa wa Mtwara, kueleza malalamiko yao na haja yao ya kupata faida ya gesi. Wanataka badala ya gesi kusafirishwa kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam bomba lisijengwe.

Bomba lisijengwe kwa maana kwamba maelezo yao yanataka gesi hiyo itumike kujenga viwanda palepale Mtwara na kuuboresha mkoa huu. Mimi nasema kheri. Ni nia njema ukiliangalia kwa jicho la haraka haraka. Ni wazi hakuna ubishi kuwa kila mwananchi anastahili huduma za msingi. Mwalimu Nyerere aliainisha mwaka 1960 kuwa ili nchi hii iweze kuendelea inahitaji watu, ardhi, siasa safi na uongozi bora.

 

Sitanii, naielewa hoja au ajenda ya watu wa Mtwara. Wanataka kutimiza msemo wa kiugwana tu wa Kiswahili usemao “ukikaa karibu na walidi, basi nawe utanukia waridi”. Ni ukweli usiopingika na wala kamwe haifurahishi kuona watu wa eneo yanapotokea madini au nishati kama gesi na mafuta, wanabaki kuwa mafukara wa kutupwa.

 

Mimi nitakuwa wa mwisho kuunga mkono sera kama hii. Ninachosema ni kuwa mikataba inayoingiwa na wawekezaji lazima izingatie mambo ya msingi. Huduma za jamii kama maji, barabara, afya, elimu na umeme vinapaswa kupewa kipaumbele katika mikataba. Suala la ajira kwa wenyeji pia linapaswa kuwa sehemu ya mkataba wowote unaoingiwa kati ya Serikali na wawekezaji katika nchi yetu.

 

Ninaposema ajira ni kuanzia kazi za migodini au kwenye mitambo ya kuzalisha umeme hadi kwenye biashara na kilimo. Kwamba wawekezaji wakiwezesha upatikanaji wa maji, wananchi wanaozunguka miradi hii watalima mbogamboga na nyanya kwa viwango wanavyotaka wao, kisha watauza kwa wahusika katika migodi hii.

 

Ni aibu kuona wawekezaji wananunua nyanya na mchicha kutoka Afrika Kusini. Wanapaswa kuwekewa masharti ya kimikataba kuwa vitu hivi vinunuliwe hapo hapo mradi unapokuwa. Ni jambo jema pia kuwa mikataba inayoingiwa inapaswa kuangalia nafasi ya wenyeji wa maeneo zinapogundulika mali ardhini, kuwa sehemu ya umiliki wa mali zinazogunduliwa katika maeneo yao.

 

Pamoja na kulipwa fidia, wabaki pia kuwa wamiliki wa mradi husika hata kama ni kwa kiwango kidogo cha asilimia mbili. Mpango huu utatoa fursa ya kutengeneza matajiri wazalendo wenye fedha halali. Kwenye migodi na miradi mikubwa kama ya gesi watu wanatajirika ajabu. Si kosa kwa Tanzania kuzalisha matajiri kupitia maliasili zetu.

 

Sitanii, nimeisikia hoja ya Wanamtwara kuwa gesi itumike kuzalisha umeme hapo hapo Mtwara na kama ni viwanda vijengwe hapo hapo Mtwara. Nasema hii ni hoja nzuri, isipokuwa utekelezaji wake ndiyo ulionitia hofu. Maandamano yaliyoandaliwa na vyama vya siasa yamepuuza uhalisia. Yanataka kuiingiza nchi hii katika laana ya rasilimali.

 

Nchi kama Nigeria na nyingine duniani, zimepata mshituko mkubwa na kuchelewesha maendeleo kwa sababu ya migogoro ya kijinga. Nasema migogoro ya kijinga kama hii kwa maana ya watu kutofikiri sawa sawa. Wanaoandaa maandamano haya wana akili timamu. Wanajua fika kuwa kwa sasa asilimia 80 ya viwanda au wateja wa matumizi ya gesi wapo Dar es Salaam.

 

Ingawa nakubaliana na hoja ya kupunguza utitiri wa viwanda Dar es Salaam, lakini uhalisia unabaki pale pale kuwa viwanda tayari vipo na vinahitaji nishati hii. China imetupa mkopo kwa njia ya msaada wenye thamani ya Sh trilioni 1.6 kwa ajili ya ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam.

 

Ulifanyika upembuzi yakinifu kujua faida na hasara za kujenga bomba hili. Wananchi wanapaswa kuelimishwa kuwa kinachofanyika ni biashara. Mtwara izalishe gesi, iiuze na kupata bidhaa mbadala. Gesi hii imekuwapo miaka yote bila kutumiwa na hivyo haijapata kuwa na faida yoyote zaidi ya heshima kwamba gesi ipo.

 

Leo Mtwara wanaokataa bomba la gesi lisijengwe, wanatembelea kwenye barabara za lami, Daraja la Mkapa na maendeleo lukuki, ikiwamo vyuo vikuu katika mkoa huo ambavyo hawawezi kusema vyote hivi vimejengwa na fedha za watu wa Mtwara. Wao wakidai kuwa wana gesi na korosho, basi Kanda ya Ziwa wangeandamana siku nyingi.

 

Kanda ya Ziwa kuna madini (dhahabu na almasi), mazao kama kahawa, pamba, mpunga na mengine ambayo kwa kiasi kikubwa na kwa miaka mingi yameendesha uchumi wa taifa hili. Dawa zinazotumika hospitalini na chaki huko Mtwara sehemu yake imenunuliwa na fedha kutoka kanda nyingine za nchi hii. Dhambi hii ya kutaka kuligawa taifa katika kanda na mikoa kwa misingi ya utajiri inapaswa kudhibitiwa. Kwa hili sitanii hata kidogo.

 

Kichwa cha makala haya kinasema: “Kikwete chukua hatua nchi inameguka vipande.” Maandamano yale yamenitisha. Mtwara wakisema wana gesi na korosho; Kilimanjaro watasema wana Mlima wao wa Kilimanjaro fedha zote zitakazoingia ni zao; Arusha watasema wana mbuga za wanyama kama Ngorongoro; Mwanza watasema wana dhahabu; Kagera watasema wana nickel; Kabanga na Zanzibar watasema wana mafuta.

 

Ni misingi hii hii ya ubaguzi na siasa muflisi zilizoifanya Zanzibar kuharakisha mabadiliko ya 10 ya Katiba ya Zanzibar yanayovunja Katiba ya Muungano. Ibara ya Kwanza ya Katiba ya Zanzibar, inasema: “Zanzibar ni nchi ambayo eneo la mipaka yake ni eneo lote la Visiwa vya Unguja na Pemba pamoja na Visiwa vidogo vilivyoizunguka na bahari yake ambayo kabla ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ikiitwa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar.”

 

Hili ni tangazo la uasi. Nilimuuliza Rais Jakaya Kikwete tukiwa Ikulu Aprili mwaka jana, iwapo ameyaona na kuyasikia mabadiliko ya Katiba ya Zanzibar na kwamba yanavunja Katiba ya Jamhuri ya Muungano. Kikwete akajibu hivi: “Kama yanawapendeza na kurejesha amani iliyokuwa imepotea Zanzibar bora waendelee tu.”

 

Sitanii, kauli hii ya Kikwete ilinisikitisha. Niliandika makala nikionya hatari ya mabadiliko ya 10 ya Katiba ya Zanzibar. Leo Mtwara wanataka gesi isisafirishwe kutoka Mtwara kupelekwa Dar es Salaam. Ningepata fursa ningemuuliza Kikwete analionaje hili. Si ajabu ataniambia; “Kama inawapendeza watu wa Mtwara na kurejesha amani, basi waendelee tu na mpango wao wa kuzuia bomba la gesi.”

 

Ndugu zangu Watanzania, tupo katika hatari kubwa. Ikiwa kila mkoa utaona unahitaji kufanya jambo na likawa, muda si mrefu nchi hii itakuwa na Jamhuri zisizohesabika idadi ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Zanzibar walitia kidole kwenye maji wakakuta hayachomi. Wameutangazia ulimwengu kuwa wamerejea mipaka waliyokuwa nayo kabla ya Muungano. Ni nchi! Nini kitakachoizuia mikoa mingine kudai mipaka iliyokuwapo kabla ya ukoloni?

 

Nini kitakachowazuia Wanyamwezi kudai Himaya ya Mirambo? Nini kitakachowazuia Wanyambo kudai Himaya ya Rumanyika au Wahaya kudai himaya ya Kaitaba. Nini, nini, nini hasa kitakachowazuia Wachagga kudai Himaya ya Mangi Meli na nyingine kama Mkwawa, Isike na Makunganya?

 

Nasema tulipofika sasa tufunge breki. Serikali ioneshe kuwapo kwake. Watu au wanasiasa wadai haki bila kuleta hatari ya kuligawa taifa hili katika vipande. Mchezo wa kuendelea kuwafumbia macho tukidhani watajiheshimu, utatufikisha pasipo. Sijapata kuelewa na wala sielewi Serikali inatoa wapi woga wa kusimamia sheria? Kikwete chukua hatua.