Na Zulfa Mfinanga, Jamhuri Media, Arusha
Miongoni mwa changamoto zilizowasilishwa katika kikao kazi cha nne cha Serikali Mtandao (e-AGA) ni mifumo ya TEHAMA kutowasiliana na kuendelea kuwapo kwa udurufu wa mifumo.
Katika hotuba ya Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete wakati akifunga kikao kazi hicho amesema suluhu ya changamoto hizi na nyingine
zilizozibainishwa ni kuziweka katika mipango ya taasisi husika kwa ajili ya kukuza na kuimarisha jitihada za serikali mtandao ili kusaidia kuboresha utendaji kazi katika taasisi na utoaji wa huduma bora kwa wananchi.
“Katika muda wa siku tatu za uwepo kwenu hapa mmejadiliana kwa kina juu ya changamoto mbalimbali zinazokwamisha utekelezaji wa jitihada za Serikali Mtandao, nafurahi kuwa changamoto hizi zimebainishwa na ninyi wenyewe ambao ni wahusika muhimu katika watekelezaji wa Sheria ya Serikali Mtandao na Kanuni zake”
“Ni jambo la kujivunia kwamba, Serikali imefanya mengi katika utatuzi wa changamoto hizi na imepiga hatua kubwa sana katika kuimarisha matumizi ya TEHAMA Serikalini, lakini kwa dhati niwaombe kutatua changamoto za kiutawala ambazo ziko ndani ya uwezo wetu ambazo kimsingi hazihitaji maazimio kwani ni majukumu yetu ya kila siku” amesema Kikwete.
Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi e-AGA Dr. Jasmine Tiisekwa amesema kupitia majadiliano yaliyotokana na mada mbalimbali zilizowasilishwa wamefikia maazimio ambayo mamlaka itasimamia utekelezaji wake na kutoa mrejesho kwenye kikao kijacho.
“Leo hii e-GA ipo tayari kupokea maelekezo yako kwa utekelezaji, sambamba na agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan la kuijenga Serikali ya Kidijitali, ambalo tunaamini litafikiwa kupitia jitihada za Serikali Mtandao zilizo imara na thabiti” amesema Dr. Tiisekwa.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao Mhandisi Benedict Ndomba amesema wataendelea kushirikiana na Taasisi za Umma katika kubuni, kusanifu na kujenga Mifumo mbalimbali ya TEHAMA itakayosaidia kutatua changamoto zilizopo katika jamii pamoja na kuiwezesha Serikali kutoa huduma kwa wananchi kwa urahisi, haraka na kwa gharama nafuu.
Miongoni mwa majukumu ya Mamlaka ya Serikali Mtandao ni Kuimarisha na Kuendeleza Utoaji wa Huduma za Serikali Mtandao kwa Taasisi za Umma, kuimarisha uzingatiaji wa Sera, Sheria, Kanuni, Viwango na Miongozo ya Serikali Mtandao kwa Taasisi za Umma pamoja na kuimarisha Utafiti, Ubunifu na Uendelezaji wa Jitihada za Serikali Mtandao.