KAULI mbili zilizotolewa na Rais Jakaya Kikwete juu ya kushika wadhifa huo mkubwa nchini, zimewachanganya baadhi ya makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) waliotangaza na wale wanaotajwa kuwania kumrithi.
Rais Kikwete akiwa ziarani China, ametangaza kwamba “kazi ya urais ni ngumu” na kwamba kwa upande wake anatamani amalize kipindi chake miezi 10 ijayo ili aingie kwenye mashambani yake akalime. Kuna wakati alipata kusema angependa akistaafu afundishe.
Kauli hiyo ya Rais Kikwete aliitoa jijini Beijing, China mbele ya mabalozi wa Afrika wanaowakilisha mataifa yao nchini China waliokusanyika kwenye Nyumba ya Wageni wa Serikali ya China ya Diaoyutai.
Hii ni kauli ya pili yenye tafsiri ya utata iliyotolewa na Rais Kikwete kwani siku chache kabla ya ziara hiyo aliwaasa vijana kumchagua mtu, “anayefanana na kijana” kurithi nafasi yake katika Uchaguzi Mkuu 2015 kiasi cha kuwaibua wahusika ambao wamezungumza kauli tofauti.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Stephen Wasira ameibuka akisema: “Nataka hiyo kazi ngumu. Mimi nasema wacha watu wote wajitokeza, tutapimwa wote tunaotaka urais halafu wanachama wa CCM na wananchi wataamua wa kumpa kazi ngumu. Mimi naiweza.”
Alisema kwamba angependa wajitokeze vijana, wanawake na wazee ili kuchujwa kabla ya kupatikana yeye kwa kuwa ana uzoefu wa kazi ngumu.
Kwa upande wake Mbunge wa Nzega, Dk. Hamis Kigwangallah amesema: “Hiyo kazi ngumu lazima apewe kijana. Ndiyo maana Rais Kikwete amesema kwamba ni wakati wa vijana. Tunachangamkia fursa hiyo.”
“Mimi niliishasema kwamba Rais Kikwete yuko sahihi. Sidhani kama mzigo mzito ni wa kumpa mzee. Itakuwa ni kumuumiza,” anasema Dk. Kigwangallah na anaungwa mkono na Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba ambaye pia ameshatangaza nia kama Dk. Kigwangallah.
“Ni kupokezana. Ni zamu ya vijana,” alisema Makamba huku Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja akisema: “Maneno ya Rais Kikwete ni ya kuyaheshimu sana hasa kwa wakati huu taifa likitaka damu changa. Nchi hii kubwa inataka mtu anayeweza kukimbiakimbia.”
Mbali ya hao wengine wanaotajwa kuwania nafasi hiyo nyeti ni pamoja na mawaziri wakuu wa zamani, Edward Lowassa na Frederick Sumaye kadhalika Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe.
Pia wamo Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, Mbunge wa Songea Mjini, Dk. Emmanuel Nchimbi Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalumu), Profesa Mark Mwandosya, Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano, Dk. Mohamed Gharib Bilal.