*TUCTA wasema watarudi katika meza ya mazungumzo

Na Aziza Nangwa, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Kanuni mpya ya kikokotoo ni kama jinamizi jipya lililoanza kuogopwa na wastaafu.

Hofu ya wastaafu kuumizwa na kanuni hiyo inakuja siku chache baada ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, kusema serikali imesikia ushauri na kupokea maoni kutoka kwa wadau mbalimbali wakiwamo wabunge, wafanyakazi na vyama vya waajiri kuhusu kuboresha mafao kwa wafanyakazi wanaotarajiwa kustaafu.

Aprili 15, mwaka huu akihitimisha hoja ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka wa fedha wa 2024/2025, Majaliwa, amesema serikali itaendelea kutoa elimu ya uhifadhi kwa jamii ikiwamo mafao.

Mei 26, mwaka juzi serikali ilitangaza kanuni mpya za kikokotoo cha mafao ya mkupuo cha asilimia 33 kwa kila mfuko wa hifadhi ya jamii.

Kuanza kwa kikokotoo hicho ni makubaliano kati ya serikali, Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA) na Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), lakini kumekuwapo malalamiko ya wafanyakazi wakitaka kirejee kama kilivyokuwa awali cha asilimia 50.

Wabunge wapinga

Wiki iliyopita wakichangia mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), baadhi ya wabunge wamekipinga kikokotoo hicho.

Mbunge wa Viti Maalumu (CHADEMA), Ester Bulaya, ameitaka serikali kukaa na wafanyakazi na kuirudisha sheria hiyo bungeni ianze kujadiliwa upya.  

Mbunge wa Manyoni Mashariki (CCM), Dk. Pius Chaya, amesema kitendo cha kuhamisha kikokotoo cha asilimia 50 kwa 50 na kupeleka asimilia 67 kwa asilimia 33 ni jambo jema lakini halikufanyiwa utafiti mzuri.

Amesema kiwango hicho cha kikokotoo hakijaangalia matarajio ya wafanyakazi kwa sababu kwa aliyedhani akistaafu atalipwa kwa mkupuo mmoja wa asilimia 50 ya mafao yake, lakini anaambiwa atalipwa asilimia 33.

Pia amesema watumishi wengi wa umma ni walimu na sekta ya afya na anaishauri serikali kupitia Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora iangalie upya suala hilo.

“Nashauri tuangalie upya. Ni suala linalopigiwa kelele lakini tuangalie ni kitu gani kitawapa motisha watumishi wetu,” amesema.

Kwa upande wake, Mbunge wa Geita Vijijini (CCM), Joseph Musukuma, amesema suala la kikokotoo haliwezi kuwa kilio cha kila siku na akaomba mawaziri watafakari kama wanaweza kurudi katika asilimia 50 ya awali au kuwa na namna nyingine ya kuwasaidia wastaafu.

Amesema haiwezekani wastaafu waendelee kulia wakati wabunge walijadili suala hilo kwa miaka mitatu mfululizo bila kupata ufumbuzi.

Pia amesema kama kuna tatizo ni vema watumishi waambiwe, la sivyo hakuna mtumishi atakayekuwa mwaminifu.

“Kama mtumishi alikuwa apate mafao ya Sh milioni 100 atapa mafao ya Sh milioni 30 halafu zile nyingine Sh milioni 70 unamtunzia. Hapo lazima niibe, kwa sababu ninajua fedha zangu sitapewa,” amesema.

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), John Heche, amewahi kunukuliwa mwaka jana akiiomba serikali kubadili msimamo wake kuhusu suala la kikokotoo kwa ajili ya kuepusha vifo vingi vya wastaafu.

Amesema suala la kikokotoo ni sawa na kuvunja makubaliano katikati ya mchezo, kwa sababu fedha ni za wastaafu si za serikali.

“Kinacholeta ugomvi serikali imekopa katika mifuko hiyo wakajenga UDOM, wakawekeza katika miradi mingi mingine ambayo haijalipa sasa wanataka kujificha.

“Wanatengeneza mazingira kana kwamba watu hawakuchangia, ni kama unaweka fedha benki halafu unakwenda kuchukua benki wanakupangia uchukue kiasi gani,” amesema.

Heche amesema baadhi ya watumishi wamekopa nyumba kwa makubaliano wakilipwa mafao yao watalipa.

“Sasa wanawaambiaje wale waliowakopesha? Kumbuka hawa wazee wamefikisha miaka 60, matokeo yake wazee wengi watakufa kabla ya umri wao. Sisi hatukubali kuona wazee wetu wanakufa kutokana na kazi walizofanya.

“Unajua kuna watu kwenye baadhi ya idara walipogundua hili linakuja walistaafu kwa hiari kuanzia miaka 55. Sheria inaruhusu baada ya miaka 57, lakini walimu ambao hawana taarifa kule vijijini watu wanataka kujinyonga, wastaafu wengine wanaona wenzao wanavyofanyiwa hivyo.

“Hata hao askari, wengi wamekumbwa na tatizo la pesa za usafiri, hazipo, watu wachache wamekula, watu wasio na uelwa wanasema mifuko haina fedha,” amesema.

Katika hatua nyingine, ameitaka serikali ifanye ukaguzi na kuangalia nani amehusika, ichukue hatua, kwa sababu mafao ni haki ya wastaafu, kwa kuwa wamewekeza fedha zao.

Kwa upande wake, Rais wa TUCTA, Tumaini Nyamhokya, amesema mwanzoni suala la kikokotoo lilitokana na mifuko mingi kuonekana itakufa.

Akizungumza hivi karibuni amesema wanaopiga kelele zaidi ni wale waliokuwa na kikokotoo kilichokuwa kinalipa asilimia 50 wakashushwa kwenda 25.

“Katika kushuka huko sisi kama viongozi wa wafanyakazi tulikataa, sheria ilitungwa na kanuni zikatungwa, lakini hazikutekelezwa kwa sababu tulishindwa kuelewana, kwa hiyo tukaenda kwenye majadiliano, vyama vyote, siyo sisi tu, tukavutana ndipo tukaenda asilimia 33,” amesema na kuongeza:

“Katika vikao vyetu tulivyokaa utekelezaji ulikuwa ni asilimia 33, kelele bado imekuwa kubwa, upande wetu tunarudi tena kukaa mezani, wale wa Mfuko wa NSSF walikuwa na asilimia 25, wale wamepanda hadi asilimia 33.

“Wale waliokuwa wanalipwa asilimia 50 wakashusha asilimia 25, wakazuia isitekelezeke kupandisha kwenda asilimia 33. Sisi tupo tunaendelea na majadiliano ili wanaostaafu wasiende kufika sehemu mifuko ikaondoka, hawa wanaoendelea kusogelea umri wa kustaafu wakakuta mifuko ile haipo.”

Amesema ni wajibu wao kuhakikisha mifuko inabaki salama lakini na wanachama wao wasiendelee kupiga kelele.

“Kwa hiyo eneo la kikokotoo bado lipo kwenye mjadala na ningeomba tulivumilie, majibu yatatoka siku si nyingi.

“Nitoe wito kwa wafanyakazi walioko Arusha, Manyara, Kilimanjaro na Tanga wafike kwa wingi kwenye siku ya wafanyakazi, ili kuonyesha dhamira yetu katika kujadiliana na kudai na kukumbushana juu ya masilahi mbalimbali ya wafanyakazi,” amesema.

Vilevile amesema suala la vikokokotoo si matakwa ya serikali bali ni hali ya uchumi na hali ya mifuko ya hifadhi ya jamii ilivyo.

“Nikisema kila anayetoka apewe mafao yake, miaka miwili mifuko itakauka, kwa hiyo tuliweka hii kuweka lojisiti ya uendelezaji wa mfuko sasa kwa sababu imepigiwa kelele.

“Si tu na Jeshi la Polisi, lakini na wengine tutakwenda kuangalia, kwa sababu tunasema serikali ni sikivu, tuone nia nzuri tunayoweza kufanya ili kikokotoo kisilete maneno mengi,” amesema.

MWISHO