madaraka1Demokrasia ni dhana nzuri sana pale ambako wote tunakubaliana juu ya maana na mipaka yake. Tatizo ni kuwa si wakati wote huwa tunaafikiana juu ya maana na mipaka yake.

Nguzo moja ya kulinda na kujenga demokrasia ni uhuru wa raia kusema wanachowaza. Ni uhuru unaoturuhusu kubadilishana mawazo, kujenga uelewa wetu wa masuala mbalimbali, kusaka haki zetu, na kusaidia jamii kwa njia tofauti. Kwa bahati mbaya, mara kwa mara hatuna makubaliano juu ya nini kinaweza kusemwa na nini hakiwezi kusemwa. Na ndiyo maana nasema kwamba kwenye mazingira ya mila na desturi zetu kijijini ukijichukulia uhuru wa kusema kuwa baba yako mjinga, hata kama ni kweli, utajikuta unapambana na kundi la wazee wanaoitwa “abanyikura” ambao si tu watataka ufute kauli yako, bali watakutoza faini ya ng’ombe. Na mwisho watakuonya wasikusikie hata kuota hilo wazo lako la kipuuzi.

Lakini nchi siyo sawa na kijiji chenye mila na desturi zake. Nchi ni mwanachama wa jumuiya ya kimataifa ambayo inakubali uanachama huo kwa kutamka kuwa itaheshimu sheria za kimataifa, ikiwa ni pamoja na kulinda haki za raia wake, raia ambao wanaweza kuamka siku moja na wakaanza kusema maneno ambayo abanyikura hawawezi kuyavumilia hata kidogo. Kamwe haitawadia siku ambapo binadamu wote tutakubaliana kuhusu masuala yote yanayotawala maisha yetu, ikiwa ni pamoja na sheria zinazosimamia masuala hayo. Baadhi ya serikali zingekuwa na uamuzi zingekataa baadhi ya vipengele vilivyomo kwenye uhuru mpana unaotolewa na Tamko la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa la mwaka 1948. Zingesema kwamba raia wawekewe mipaka ya uhuru inayopaswa kuzingatiwa.

Kwa maoni yangu wengi wetu tunatambua kuwa haki za msingi zina mipaka katika mazingira yetu, lakini tupo wengi wengine ambao hatuwezi kusema haya hadharani kwa sababu yatapingana na msimamo uliopo juu ya haki za binadamu. Kuna msemo wa Kiingereza kuwa ukweli haujidhirihishi wazi kama nuru inavyotofautishwa na kiza. Demokrasia si kiwango kinachowekwa na Shirika la Viwango Tanzania; ni dhana ambayo inaathiriwa na mila, desturi, na tamaduni zilizopo.

Mila na desturi ndiyo msingi unaojenga kanuni na baadaye sheria, na unapozuka ubishi juu ya kukiukwa kwa demokrasia, kihalisia tunabishana juu ya migongano na tofauti kati ya mila na desturi, na tamaduni zetu na zile ambazo tumezipokea na zimeunda baadhi ya sheria tulizonazo.

Watu wenye misimamo mikali huchukia sana watu wasio na msimamo wowote. Mshairi wa Kitaliani Dante Alighieri aliwahi kuandika kwamba sehemu zenye joto kali kuliko sehemu nyingine zote jahanamu hutengwa mahususi kwa watu ambao panapozuka mpasuko mkubwa wa uadilifu ndani ya jamii, wao huogopa kuweka msimamo wowote.

Ubishi juu ya nini maana halisi ya demokrasia na uhuru wa kutoa mawazo unaweza kuwa chanzo cha mpasuko mkubwa ndani ya jamii, na ni ubishi ambao unatukabili nchini sasa hivi.

Mimi sichukui nafasi ya watu ambao Alighieri aliwasema, lakini naona ipo nafasi nzuri kwa mtu kusema kuwa linapojitokeza suala la kujadili ni zipi haki za msingi za raia, na nini hasa demokrasia ya kweli, hakuna ukweli wowote ulio dhahiri kwa kila mtu.

Ni kwa sababu hiyo tutakaa muda mrefu mno au tushuhudie kabisa hapa nchini ndoa ya kwanza ya jinsi moja, ambayo kwa baadhi ya nchi sasa ni haki ya msingi ya raia.

Lakini Watanzania hao hao ambao watapinga kwa nguvu zao zote ndoa za jinsi moja wanaweza kuunga mkono uhuru wa kukosoa serikali na viongozi wake, ikiwa ni pamoja na uhuru wa kumkosoa rais wa nchi.

Sidhani kama tatizo linalowakuta baadhi ya wale waliokulia kwenye enzi za Facebook na Twitter ni suala la watu wanaoamini sana kuhusu fasili ya Magharibi ya demokrasia na uhuru wa kujieleza. Ni tatizo ambalo mimi nalifananisha na la mtoto kugundua ghafla kuwa kuanza kujifunza kuandika kumempa uhuru wa kuandika siyo kwenye madaftari ya shule tu, bali kwenye sehemu nyingine nyingi.

Ataanza kuandika “nioshe” kwenye vioo vya magari yaliyoshika vumbi, halafu anaweza kuanza kuandika matusi kwenye kuta za nyumba.

Wamepata uhuru ambao hawajatambua kuwa si tu umewekewa mipaka ya kisheria, bali umewekewa pia mipaka isiyo ya kisheria, lakini inayotokana na mila na desturi zinazotuzunguka.

Tunaweza kuzua mjadala juu ya ubora au upungufu uliomo kwenye sheria, au mila na desturi hizo, lakini hayo ndiyo mazingira tuliyo nayo.

Wapo wanaharakati na wanasiasa ambao wapo kwenye kundi lililojiingiza kwenye mtafaruku wa kisheria kwa nia ya, ama kubadilisha sheria zilizopo, au kuhoji sababu ya jamii kukubali kukumbatia mila na desturi ambazo kwa maoni yao zimepitwa na wakati. Siwazungumzii hawa, ila wale ambao naamini wanajikuta kizimbani bila kukusudia kwa sababu tu walikuwa na haraka ya kutoa maoni yao bila kutafakari athari zake.

Tumepokea vigezo vya kuishi vya kimagharibi, huku kiundani tukiwa bado tunashikilia mila za mababu zetu. Suala kwangu siyo nani yuko sawa na nani hayuko sawa ila kutambua tu mazingira ambayo tunayo. Atambue hivyo anayeamka na kuamua kumuita baba yake mjinga, na atambue hivyo hivyo mzee anayeishi kijijini ambaye mwanae kumuita mjinga. Lakini mwisho wa yote, tukubali tu kuwa uamuzi wetu utahukumiwa na mila na desturi mseto zilizopo na sheria zinazoambatana na huo mseto.