Kampuni ya AndBeyond ya Afrika Kusini, imeingia mkataba na uongozi wa Kijiji cha Ololosokwan, Ngorongoro mkoani Arusha unaoiwezesha kuhodhi ekari 25,000 za ardhi kwa ajili ya utalii wa picha.
Malipo yote yanayofanywa na kampuni hiyo yanaishia mikononi mwa viongozi wa kijiji ambao wanasema fedha hizo wanazitumia kwa shughuli za maendeleo huku Serikali Kuu ikiwa haiambulii kitu.
Pamoja na kuingia mkataba na kijiji, eneo hilo la ardhi ni sehemu ya kilometa za mraba 4,000 ambazo ni Pori Tengefu la Loliondo. Eneo hilo linajulikana kisheria kuwa ni kitalu cha uwindaji kinacholipiwa ada zote na kampuni ya Ortello Business Corporation Ltd (OBC).
Kampuni ya AndBeyond, imekuwa ikisifiwa mno na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo, akiitaja kama miongoni mwa wadau wakuu wa maendeleo ya Arusha na Taifa.
Urafiki huo umeifanya AndBeyond imtumie Gambo kuhakikisha uwanja wake wa ndege ulio mpakani mwa Tanzania na Kenya, unafunguliwa licha ya kuwapo taarifa za kiusalama zinazozuia hatua hiyo.
Wadau wanaopambana kukomesha migogoro Loliondo wanaitaja AndBeyond kwenye orodha ya ‘wafadhili’; huku Gambo mara kadhaa akipewa hifadhi ya malazi na chakula kwenye kambi yake ya Klens iliyopo Ololosokwan.
“Kilichopo ni kuwa OBC ndio wenye kitalu hiki cha daraja la kwanza. Ada yake kwa mwaka ni dola 60,000 wanayolipa serikalini kisheria. Sasa hawa AndBeyond ni ‘parasite’ walioamua kuwekeza kwenye ardhi ambayo hawalipi ushuru wala kodi serikalini,” kimesema chanzo chetu.
Wiki iliyopita, Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Maghembe, akiwa katika Kijiji cha Ololosokwan akikagua chanzo cha maji cha Oltigomi, alitoa siku saba kwa AndBeyond, kwenda ofisini kwake ili kutoa maelezo ya namna walivyoweza kujipatia ekari 25,000 ndani ya kitalu kinacholipiwa na kampuni nyingine.
Profesa Maghembe alisema ni jambo la kushangaza kuona kampuni za raia wa kigeni zinaingia mikataba ya ardhi kubwa kiasi hicho huku Serikali ikiwa haikushirikishwa na haipati mapato yoyote.
“Hii ni hatari hata kwa usalama wa nchi, inakuja kampuni inaingia mkataba na kijiji bila wizara na Serikali kujua, natoa siku saba waje ofisini tujue walipataje eneo hili ambalo ukiacha hizo ekari 25,000 bado lipo ndani ya kitalu cha kampuni nyingine,” ameagiza Waziri Maghembe.
Hata hivyo, mbali na AndBeyond, kuna kampuni nyingine za utalii wa picha zilizo ndani ya kitalu kinacholipiwa na OBC. Miongoni mwazo ni Buffalo na Thomson Safaris.
“Huku hakuna mamlaka zinazoratibu shughuli zao kwa hiyo ni rahisi kufanya mambo wanavyotaka tofauti na wakiwa kwenye Hifadhi za Taifa au kwenye Mapori ya Akiba,” kimesema chanzo chetu.
Wizara ya Ardhi yatoa neno
Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angelina Mabula, amezungumza na JAMHURI na kusema suala la AndBeyond ni jipya kwake kulisikia, na ameahidi kulifuatilia kupitia kwa wizara ya kisekta ambayo ni Wizara ya Maliasili na Utalii.
Kisheria, kijiji kinaruhusiwa kutoa ardhi kwa mwekezaji isiyozidi ekari 50. Zaidi ya hapo mwekezaji anapaswa kupitia wizara yenye dhamana ya ardhi na pia katika Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC).
Uwekezaji wa kampuni ya Andbeyond Limited katika Kijiji cha ololosokwan
Utangulizi
Wilaya ya Ngorongoro ilianzishwa mwaka 1979 kama Wilaya kwa mujibu wa Sheria ikiwa na Tarafa tatu za Sale, Loliondo na Ngorongoro. Wilaya imepakana na Kenya kwa upande wa Kaskazini, Mashariki imepakana na wilaya za Longido na Monduli, Karatu upande wa kusini na upande wa magharibi imepakana na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
Kijiji cha Ololosokwan kipo ndani ya Pori Tengefu Loliondo na kinapakana na Hifadhi ya Taifa Serengeti upande wa Mashariki. Kaskazini kinapakana na Kenya.
Kijiji cha Ololosokwan kimeingia mkataba na Kampuni ya AndBeyond Limited kwa ajili ya kuendesha shughuli za utalii wa picha katika eneo lenye ukubwa wa ekari 25,000. AndBeyond Limited imekuwa ikifanya shughuli za utalii wa picha katika eneo hilo tangu mwaka 1996.
Kulingana na Sheria ya Wanyamapori Na.12 ya mwaka 1974, Sheria ya Wanyamapori Na.5 ya mwaka 2009 eneo lote la Tarafa ya Loliondo na sehemu ya Tarafa ya Sale linatambulika kama Pori Tengefu la Loliondo lenye ukubwa wa takribani kilomita za mraba 4,000. Eneo hili ni kitalu cha uwindaji ambako kampuni ya OBC imepewa dhamana ya kuwinda katika eneo la Pori Tengefu Loliondo. Pamoja na eneo hilo kutambulika kama kitalu cha uwindaji, bado kumekuwepo vijiji vilivyoingia mikataba na kampuni nyingine za utalii wa picha, kikiwamo Kijiji cha Ololosokwan.
AndBeyond Klein’s Camp na mchango wake kwa serikali
Kwa mujibu wa Sheria ya Wanyamapori, eneo la Pori Tengefu la Loliondo ni kitalu cha uwindaji. Kampuni ya OBC walipewa kitalu hiki kwa ajili ya shughuli za uwindaji wa kitalii Pamoja na kwamba OBC ndiyo inayomiliki eneo hilo, kumekuwapo kwa mkanganyiko mkubwa katika matumizi ya pori hili; jambo ambalo limesababisha vijiji kuingia mikataba na kampuni nyingine zinazofanya shughuli za utalii wa picha.
Shughuli za utalii zinazofanywa na AndBeyond
*Matembezi ya wageni (Walking safaris)
*Matembezi kwa magari (Game Drive),
*Utalii wa kiutamaduni (Cultural boma visit),
*Matembezi ya magari usiku (Night game drive)
Mchango wa AndBeyond Limited
Kampuni ya AndBeyond imekuwa ikilipa kijiji cha Ololosokwan fedha za mkataba kutokana na makubaliano yao wenyewe. Kutokana na mkataba huo, hakuna kiasi cha fedha ambazo Serikali Kuu au Halmashauri ya Wilaya inapata kutokana na mkataba huo.
Kimsingi mapato yanayolipwa na AndBeyond Limited kwa Serikali ni kama ifuatavyo:-
Conservation fee and Entry fee ambayo hulipwa kwa CITES na mgao wake kwenda kwa wanufaika ambao ni Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro, Kijiji cha Ololosokwan na Wizara ya Maliasili. Kwa mujibu wa kanuni za utalii wa picha ya mwaka 2016; Kijiji hupata asilimia 20, Halmashauri asilimia 30 na Wizara ya Maliasili na Utalii asilimia 50.
Kisheria AndBeyond ilipaswa ilipe Ushuru wa Huduma (Service levy 0.3%) kwa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro. Katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita kampuni hii ililipa Halmashauri Sh milioni 13 pekee.
Kwa miaka mitatu iliyopita, Andeyond kulingana na mkataba wake na Kijiji cha Ololosokwan imelipa Sh 880,941,990.00. Kati ya fedha hizo, Sh 465,158,877.00 zilipwa kwa kijiji; Sh milioni 105 zikiwa ni fedha kwa ajili gharama za kuhifadhi mazingira, na Sh 310,783,113.00 kwa ajili ya mishahara ya watumishi wanaotoka Kijiji cha Ololosokwan.
Katika hali ya kawaida ni vigumu sana kwa eneo moja kuwa na matumizi tofauti kwa maana ya uwindaji na utalii wa picha. Wakati mwingine hali hii husababisha vurugu baina ya wawindaji na wapiga picha. Kila mdau anakuwa na mtazamo wa tofauti kwa kuwa kila mdau anahitaji lake tofauti na mwingine. Mwindaji anahitaji kuwinda wakati mpiga picha anahitaji kupiga picha tu.
Imeelezwa kuwa kwa kuwa kampuni ya uwindaji ya OBC ndiyo wenye kitalu kisheria, ni vyema kampuni za picha wakawekeza katika maeneo ya nje ya uwindaji ili kuepusha mgongano wa kimaslahi, lakini vile vile mgongano katika shughuli zao.