Shukrani ni jukumu la kufanyika haraka


 
“Hakuna jukumu linalohitajika kufanyika haraka kama kurudisha shukrani,” alisema James Allen. Kushukuru ni kuomba tena.
Shukrani ni kurudisha fadhila ya kuona umefanyiwa kitu cha thamani na mtu ambaye anaweza kuwa rafiki yako, ndugu, mzazi, mfanyakazi mwenzako au mtu yeyote unayemfahamu na usiye mfahamu.
Ni jukumu letu sote kurudisha shukrani kwa wema tunaotendewa kila wakati. Hakuna jambo baya kama kufanyiwa kitu chema na ukae kimya kana kwamba hakuna kilichotokea.
Tunafundishwa kuwa watu wa shukrani tangu tukiwa watoto. Wazazi wetu wanajua kwamba kati ya vitu muhimu vya kujifunza ni kuwa na moyo wa shukrani. Wengi wanapokua wanaona kama kushukuru ni kitu kisicho na umuhimu. Ndiyo maana mwandishi wa vitabu Robin Sharma anafikia hatua ya kusema: “Watu wazima ni watoto walioharibika.”
Utotoni tunafundishwa vitu vingi lakini tunapokua tunaviacha na kufuata njia tofauti ambazo hazifai. Wengine hufikiri kwamba kufanyiwa jambo jema ni haki yao, hivyo hakuna haja ya kushukuru.
Asante ni neno linaloweza kuwa dogo kwa anayelitoa lakini lina maana kubwa sana kwa anayelipokea. Nilipokuwa mdogo nilifundishwa na wazazi wangu kusema “asante” pale nilipoletewa zawadi au nilipopewa kitu chochote. Niliposahau na kuchukua zawadi hiyo bila kutaja neno “asante mama/ baba” nilipokonywa zawadi hiyo. Nafikiri kila mmoja wetu alikulia katika mazingira ya namna hiyo.
Tuyafanye maisha yetu yatawaliwe na mioyo ya shukrani. Unapotendewa wema shukuru. Unapofanyiwa jambo hata liwe dogo namna gani shukuru.
Bila kujali wewe ni mdogo au mkubwa namna gani, kushukuru ni jukumu la kila mtu. Unaweza kufanyiwa jambo zuri na mtu unayemzidi umri, kumzidi umri lisiwe jambo la kufanya usishukuru.
Siku moja nilikuwa nimepanda basi nikielekea sehemu fulani jijini Dar es Salaam, gari hilo lilikuwa limejaa, tulipofika katika kituo kilichofuata kulikuwa na mzee wa makamo aliyetaka kupanda gari ambalo kila siti ilikuwa imekaliwa. Mzee yule alipoingia ndani nikampisha ili akalie siti niliyokuwa nimekalia. Jambo la kushangaza, mzee yule baada ya kukaa alikaa kimya, huku nikiwa nimesubiri aseme walau asante. Hadi ninashuka, masikio yangu hayakupata kusikia neno lolote kutoka kwa mzee yule.
Kuna watu wengi ambao maisha yao yanapelekwa kama ya mzee niliyekutana naye. Tunafikiri kuna mambo mengi tunapaswa kufanyiwa kama haki, kumbe tulipaswa kushukuru.
“Kushukuru jambo ulilofanyiwa inaweza kutengeneza siku au kubadilisha kabisa maisha. Msukumo wako wa kuweka maneno ya kushukuru ndicho kitu cha muhimu,” anasema Margaret Cousins. Inawezekana mtu akafanya jambo dogo kwako lakini unavyomshukuru wewe inawezekana ukabadilisha maisha yake au mtazamo wake katika kujitoa kwa wengine.
Maneno kama: “Umekuwa mtu wa thamani sana kwenye maisha yangu. Nashukuru, ubarikiwe sana.” Au “Siwezi kusahau mchango wako katika maisha yangu.” Yanaweza kuwa madogo kwa yule anayeyatoa lakini ni makubwa mno kwa yule anayeyapokea.
Inawezekana amekutendea jambo jema kwa mara ya kwanza, unapomshukuru mtu huyu, tayari anaona kuna deni la kuwatendea zaidi watu wengine mambo mema.
Maneno kama “Asante” au “Ninashukuru” ni madogo sana lakini matokeo yake pale yanapotoka yanafanana na yale ya njiti ya kiberiti. Njiti ya kiberiti ni ndogo lakini inaweza kuchoma msitu mzima.
Mwaka unapokaribia kwisha, jiulize ni watu wangapi wamechangia ili wewe uweze kusonga mbele na uwashukuru. Mwezi unapokwisha, kaa chini na tafakari ni kwa namna gani au ni watu gani wamechangia kufanikisha mambo yako na uwashukuru.
Wiki inapofikia ukingoni jiulize ni watu gani wameifanya wiki yako iwe ya furaha na amani na uwashukuru.
Siku inapokwisha usiache kusema asante kwa walioifanya iwe siku nzuri kwako.
Inawezekana ni mfanyakazi mwenzako aliyekusaidia kazi ofisini, mwambie asante.
Inawezekana ni dereva wa bodaboda anayekuwahisha kila siku kazini, mwambie asante.
Inawezekana ni mtu anayekupa hamasa kila unapokaribia kukata tamaa, mwambie asante.
Inawezekana ni mtu aliyekuhudumia chakula mgahawani, mwambie asante hata kama umelipia.
Inawezekana ni mzazi anayekulipia karo, mshukuru kwa sababu kuna kitu amejinyima ili wewe usome.
Usisite kila mara kuwa mtu wa shukrani. Mwisho wa yote usisahau kumshukuru Mungu anayekupa sababu za kuendelea kuishi. “Mungu amekupa zawadi ya sekunde 86,400 leo. Umetumia hata moja kusema, asante?” anatukumbusha William Arthur Ward.