Acha kufanya mambo kwa mazoea

Binti mmoja alizoea kumuona mama yake ambaye kila alipotaka kupika samaki alimchukua samaki na kumgawanya katikati ndipo alipoanza kumpika. Jambo hilo lilimfanya binti yule atake kujua kwanini mama yake kila alipopika samaki alimgawanya katikati.

Siku moja akaamua kukata ukimya na kumuuliza mama yake kwanini kila alipopika samaki alimgawanya katikati. Mama yake alimjibu hivi: “Nilizoea kumuona mama yangu kila alipotaka kupika samaki aliwagawanya katikati.” Jibu hilo halikumtosheleza binti yule, hivyo akaamua kwenda kwa bibi yake kupata majibu ya swali lake.

Alipofika kwa bibi yake akamuuliza swali lile lile. Bibi yake akamjibu akisema: “Mjukuu wangu, zamani wakati mama yako akiwa mdogo tulikuwa na chungu kidogo hivyo samaki mzima asingeweza kuenea katika chungu hicho, ili aweze kuenea katika chungu ilitupasa tumgawanye samaki huyo katikati.” Binti huyo sasa alipata jibu, si kwamba samaki asipogawanywa katikati hawezi kuiva, bali mama yake alizoea kuona samaki akipikwa kwa kugawanywa katikati, akafanya kuwa kanuni yake ya mapishi.

Mama yake binti huyo alikuwa akifanya mambo kwa mazoea. Kuna kitu kikubwa katika hadithi hii ambacho kila mmoja wetu anatakiwa kujifunza, kitu hicho ni kuacha kufanya mambo kwa mazoea.

Dunia ya sasa inabadilika kila kukicha, dunia inakwenda kwa kasi sana. Ukiwa mtu wa kufanya mambo kwa mazoea ni wazi kuwa kuna vitu vingi utavikosa.

Kipaji chako kitakufa kama ukiendelea kufanya mambo kwa mazoea, biashara yako itakufa kama ukiendelea kufanya kwa mazoea.

Kuna kampuni ambazo zilikuwa juu kiuchumi lakini kwa kuendekeza mazoea katika kufanya kazi zao, kampuni hizo zimeshuka kiuchumi na nyingine zimepotea kabisa kwenye ramani. Hakuna mtu anayetumia bidhaa za kampuni hizo.

Mfano mzuri wa kampuni ambayo ilitumia mazoea katika utendaji wake na hatimaye kushindwa kulimudu soko ni Kampuni ya Kodak. Kampuni hiyo ilijihusisha na kutengeneza kamera za analojia, kwa wale wanaokumbuka vizuri miaka ya 2000 na kurudi nyuma kamera hizo zilikuwa maarufu sana. Zilikuwa ni kamera zilizowekewa kitu kilichojulikana kama ‘mkanda’. Ulikuwa ukipigwa picha na kamera hiyo mpiga picha anakwenda ‘kuosha’ picha hiyo na baadaye anarudisha picha yako na nyuma akiwa amebandika kitu kilichoitwa ‘Negative’ ambacho kilitoka katika mkanda.

Kodak ilifanya vema sana enzi hizo lakini hawakushtuka na kuona kwamba muda wa dijitali umewadia. Hawakuona kama kuwepo kwa dijitali kutawaondoa katika soko, wakaendelea kufanya kama walivyozoea kufanya, yaani kutengeneza kamera zao za kutumia mikanda.

Baadaye mambo yakabadilika, watu wakaanza kutumia kamera za dijitali, simu nazo zikawa na kamera zenye uwezo wa kupiga picha nzuri kuliko zile zilizopigwa na kamera za Kampuni ya Kodak. Hakuna tena mtu aliyehitaji kusikia tena kuhusu habari za Kodak.

Kosa kubwa lililofanywa na Kampuni ya Kodak ni kutotaka kujiendeleza. Hali ya kutotaka kujiendeleza ndiyo hali ya kufanya mambo kwa mazoea. Kodak hawakutaka kujua habari za dijitali wakati dunia ilielekea huko.

Kuna watu wengi leo hii wapo kazini lakini kuna mambo wanatakiwa kujifunza yanayohusiana na kazi zao, hawajifunzi mambo hayo kwa kisingizio kwamba ni wakongwe na wanajua kazi zinavyofanyika. 

Ngoja nikwambie rafiki yangu, ukongwe wa Kodak haukufanya wasitoke katika soko la kamera. Hivyo hivyo ukongwe wako hautafaa kitu kama hautakuwa tayari kujiendeleza.

Ukiwa na kipaji acha kutumia kipaji chako kwa mazoea, tafuta ujuzi wa namna ya kukuza kipaji chako. 

Kuwa na kipaji ni sawa na kuwa na gari zuri lakini ujuzi ni mafuta ya kuliwezesha gari hilo kutembea. Kuwa na gari zuri bila kuwa na mafuta utaishia kulitazama tu, hauwezi kwenda nalo mahali popote.

Tujenge tabia ya tunatakiwa tufanye nini na si tabia ya tulizoea kufanya hivi. Kufanya kwa mazoea kutawafanya watu wengine waonekane bora zaidi yako ingawaje unaweza kuwa bora. Kufanya biashara kwa mazoea kutawafanya wateja wakimbie biashara yako na kwenda sehemu ambako kila kukicha wanafikiria kwa namna gani watamfanya mteja aondoke na tabasamu na kutamani kurudi ili aendelee kupata huduma nzuri aliyopewa.

Tukiacha kufanya mambo kwa mazoea na kufanya kwa uhalisia, pia kuwa na moyo wa kutaka kujiendeleza tutafika mbali sana.