Maisha hayahitaji watu wepesi wepesi
Nimeamka asubuhi na mapema huku nikifurahia tukio moja zuri sana, ni pale jua linapoliambia giza, “Inatosha sasa, huu ni wakati wangu wa kutawala.”
Napaki mizigo yangu na kutoka nje. Naanza kwenda katika kituo cha magari, ni sehemu iliyopo katikati ya nchi ya Tanzania, jiji la Dodoma. Mahali hapa panaitwa Chemba ni wilaya iliyopakana na wilaya ya Kondoa.
Inafika muda wa saa 12:30 alfajiri basi la kampuni ya Machame Investment linafika kituoni. Naweka begi langu kwenye buti na kupanda kwenye basi. Nasalimu abiria wenzangu tulioketi wote kiti cha nyuma kabisa. Naketi na kumuomba Mungu atujalie tufike salama jijini Dar es Salaam.
Huku nikivuta hewa safi ya oksijeni ambayo pia huvutwa na vigogo wengi wa nchi hii, naendelea kutazama nje na kuona jinsi Jiji la Dodoma linavyokua kwa kasi. Najisemea kimoyomoyo, “Itabidi nifanye mpango na mimi ninunue kiwanja Dodoma.”
Baada ya kutulia nachukua kitabu changu cha 5 AM Club kilichoandikwa na mwandishi Robin Sharma, naanza kukisoma. Majirani zangu wanaanza kunishangaa kama ambavyo watu wengi hunishangaa siku zote. Sitasahau siku ile nasafiri nilipofungua kitabu kusoma kama alivyofanya yule mtunza fedha wa Ethiopia katika kitabu cha Matendo ya Mitume. Nilisikia mmoja aliyeketi jirani na nilipokuwa akisema, “Huyu si Mtanzania, atakuwa mgeni ametembelea nchini, haya mambo ya kusoma ukiwa unasafiri wanafanya Wazungu tena mara nyingi kwenye ndege.”
Sikutaka kuingilia nikajua nimezungukwa na watu walio gizani kama isemavyo methali hii, “Usilolijua ni kama usiku wa giza.”
Muda unapita sasa huku nikiwa nimepata ‘madini’ yasiyo ya kawaida kutoka kwa Robin Sharma. Nafunga kitabu changu na kukirudisha katika begi la mgongoni. Nainua macho na kutazama video ya kwenye basi. Wanaanza kuonyesha na kutuelezea historia ya Mto Amazon, tena historia hii inaelezwa kwa lugha yetu pendwa ya Kiswahili. Nafurahi kuyafahamu mambo mengi kama kijana wa maarifa kuhusu Amazon.
Nilijua Amazon ni mto mrefu, lakini sikujua kama ni mto wa pili kwa urefu duniani, tena tukaambiwa pamoja na kuwa na urefu huo, mto huo ndio wenye maji mengi kuliko mito mingine duniani.
Tunaoneshwa pia msitu wa Amazon ambao asilimia kubwa ya hewa safi ya oksijeni ambayo dunia inaifurahia bila kulipia chochote huzalishwa hapa. Si kuzalishwa tu, bali hata asilimia kubwa ya hewa chafu inayozalishwa na viwanda duniani kote hufyonzwa na msitu wa Amazon. Tena nikaona picha ya miti inayotembea kwa jina maarufu kama walking palms (mitende inayotembea) inayopatikana katika msitu mnene wa Amazon.
Nikasema kweli safari hii nimejifunza mengi ama kweli mkaa bure si sawa na mtembea bure, na wahenga hawakukokesea waliposema tembea uone. Mimi niliona maajabu ya Amazon.
Historia ya Amazon inakwisha. Inafuata filamu inayoonyesha maisha ya wanyama. Humu tunamuona simba. Maisha ya simba yanatoa funzo zuri sana kama ukimtazama kwa makini.
Simba si mnene kama alivyo tembo, wala si mrefu kama alivyo twiga, wala hana mbio kama akimbiavyo duma, lakini bado anaitwa mfalme wa mbunga. Angurumapo simba wanyama wengi – kama si wote huwa wapole.
Ni nini kinachompa jeuri hii simba? Nabaini kitu kimoja juu ya simba. Huyu ni mnyama jasiri na anayejiamini. Ndipo sasa nakumbuka msemo wa John Wanamaker aliyesema, “Kujiamini! Kujiamini! Kujiamini! Huo ni mtaji wako.”
Simba hana mtaji mwingine tofauti na kujiamini na ujasiri. Anapoutumia mtaji huo kila siku anaendelea kupata chakula safi cha nyama iliyonona toka kwa wanyama wengine.
Simba ananifundisha kuwa maisha hayahitaji watu wepesi wepesi, bali watu wanaojiamini. Ukiwa mwepesi maisha yatakuvunja vunja kama bilauri ya kioo inavyovunjika.
Nawaza tena na kujiuliza hivi simba angekuwa binadamu angefanya haya yote? Binadamu huyu ambaye anafanya maisha ya kujilinganisha kuwa sehemu ya maisha yake, anasahau maneno ya Theodore Roosevelt aliyesema, “Kujilinganisha ni mwizi wa furaha.”
Ukitumia muda mrefu kujilinganisha na wenzako utachelewa kufika unakokwenda. “Sijui siri zote za mafanikio, lakini njia pekee ya kushindwa ni kujilinganisha na wengine,” alisema mwandishi wa vitabu na mchungaji Rick Warren.