MOROGORO

Na Everest Mnyele

Wakati mwingine huwa ninajiuliza, nini sababu ya kigugumizi kwa Watanzania, hasa viongozi kuhusu Katiba mpya wakati rasimu tunayo? 

Rasimu hiyo imetokana na mawazo au maoni ya wananchi yaliyokusanywa na Tume ya Warioba iliyoteuliwa na Rais wa Nne, Jakaya Kikwete, kisha kuchakatwa na Bunge Maalumu la Katiba ambalo mmoja wa viongozi wake wa juu alikuwa Samia Suluhu Hassan, ambaye sasa ndiye Rais wetu. 

Tatizo liko wapi? Rasimu ipo, walioipendekeza wengi wao wapo hai. Je, hatukubaliani na rasimu au hatuiamini? Kwa nini tusimalizie mchakato kwa wenye Katiba yao (wananchi) kuipigia kura ya maoni?

Tusidanganyane, lazima kuna kundi fulani lenye aina fulani ya hofu; kundi lenye ushawishi kwa jamii.

Nilitoe hofu kundi hilo kwa kulikumbusha kuwa kulikuwa na jambo moja tu kubwa kwenye rasimu; muundo wa Muungano na idadi ya serikali. Mengine mengi yaliyosalia ni mazuri sana kwani yanatoa ushiriki mkubwa wa wananchi katika kuiongoza nchi yao. 

Sioni sababu ya kuwapo kwa kundi lenye hofu kwa rasimu ile, badala yake lijipange vizuri tu, kwani ukitokea ‘kulamba dume’ na kupata uongozi, utatawala kwa uhakika sana kutokana na uhalali wa kupatikana kwako.

Nitaelezea baadhi ya mambo muhimu yaliyomo kwenye rasimu yatakayoondoa kwa kiasi kikubwa migongano iliyokuwapo.

Kwanza, Tume Huru ya Uchaguzi. Rasimu ya Katiba imelitatua hili vizuri kabisa, ikieleza jinsi ya kuipata; wajumbe wake na sifa zao. 

Pia imeeleza vizuri jinsi ya kumpata Mwenyekiti na Mkurugenzi wa Tume Huru, ikijibu maswali mengi yaliyokuwa yakitia shaka kwa tume iliyopo. 

Pili, kuwapo kwa wagombea huru nafasi za Rais, wabunge na madiwani. Hili nalo limefafanuliwa ikionyesha kuwa ni vema wagombea binafsi waruhusiwe kwani si lazima watu wenye uwezo wa kuongoza watokane au watoke tu ndani ya chama fulani.

Katika hili inawezekana akapatikana mgombea ambaye hajali paka awe mweupe au mweusi; muhimu ni kukamata panya. Yaani muhimu ni kuleta maendeleo chanya kwa wananchi, si lazima kuwa na chama. 

Suala la tatu ni umuhimu wa kuwa na mgawanyo wa madaraka kati ya Serikali, Bunge na Mahakama. 

Hili limezungumzwa vizuri. Katiba ya sasa inafanya mihimili mingine kuwa tegemezi kwa Serikali katika kujiendesha hasa kibajeti.

Rasimu imetamka bayana umuhimu wa kuwapo Mfuko wa Bunge, Mahakama na Tume Huru ya Uchaguzi. Hiki ni kitu kizuri na kinaweza kuleta ufanisi katika utendaji kazi wa mihimili hii mitatu, hivyo kuweza kusimamiana. 

Jingine lililowekwa kwenye rasimu ni kuhusu mamlaka ya uteuzi wa, kwa mfano Jaji wa Mahakama ya Juu, majaji na viongozi wengine muhimu, ikiweka jinsi ya kuwapata wateule kwa kuhamisha mamlaka kutoka kwa Rais kwa yeye kusaidiwa na Tume ya Sheria na Tume ya Utumishi wa Umma kuanzisha mchakato wazi wa uteuzi. 

Rasimu hii imepunguza wigo wa Rais kufanya teuzi ambazo si za lazima na kutoa fursa ya watu kushindana kupata nafasi hizo. 

Hizi ni baadhi ya sehemu zenye utata. Pia kuna suala la haki za binadamu na Rasimu imepunguza kwa kiasi kikubwa sheria kandamizi zinazopoka haki ya watu.

Kimsingi rasimu imetibu na kujibu kero nyingi zinazosababisha kelele. 

Swali ni tumekwama wapi? Kwa nini tusimalizie mchakato huu?

Ni jambo la kushangaza kuona mjadala unataka kuanza upya. Tumetumia gharama kubwa na muda wa kutosha kupata rasimu na sasa kuna dalili za kuiweka kapuni bila sababu za msingi au kwa visingizio visivyo na mantiki. 

Ombi langu kwa wasaidizi wa Rais wamsaidie sana kwa kuwa ameonyesha nia njema ya kutufikisha mwisho wa jambo hili (hivi karibuni nilimsikia akitaka Kamati ya Profesa Mukandala kulifanyia kazi zaidi suala la Katiba, ishara kwamba anaona halijakaa sawa na pengine hawakusema kuhusu rasimu iyopo).

Niseme kutoka moyoni, nia ya Rais ni njema ila hofu yangu ni kwa watu wanaomzunguka, hasa wale wasiopenda mabadiliko.

Viongozi msaidieni Rais kuijenga Tanzania ya walau miaka 100 ijayo!

Kwa mtazamo wangu, sioni kwa nini sula la Katiba mpya linawekwa muda mrefu wakati tunayo Rasimu ya Katiba mkononi.

Mwisho, ni vema tukatambua kuwa utawala wa demokrasia, Katiba shirikishi na utawala bora ni kichocheo kikubwa cha maendeleo na ustawi wa kweli kwa wananchi na huongeza furaha. 

Jukumu lipo kwa viongozi na wote wenye majukumu ya kumshauri Rais kama ile Kamati ya Profesa Mukandala. 

Kuna msemo kuwa ‘wakati wa neema hutengeneza kizazi dhaifu, kizazi dhaifu hutengeneza wakati mgumu na wakati mgumu hutengeneza kizazi kizuri’.

Tujitafakari kizazi cha sasa kipo wapi, hasa kwa wenye umri wa kati ya miaka 30 hadi 65. 

Tuisaidie nchi kupata mwongozo mzuri ambapo kila mwananchi atapata fursa sawa ya kushiriki kuiletea nchi na yeye mwenyewe maendeleo, ustawi na furaha kama Rasumu inavyotamka.

Ifahamike kuwa sijasema rasimu ndiyo mwisho wa kila kitu, inaweza kuboreshwa. Tusidanganyane, viongozi tuchukue hatua, hii nchi ni yetu sote, na wananchi wanatutegemea.