Na Immaculate Makilika, JamhuriMedia, Mwanza
Kawaida daraja hujengwa kwa kusudi la kuwa na njia ya kupitia juu ya pengo au kizuizi. Licha ya hivyo daraja pia linaweza kuchochea uchumi wa eneo husika kwa kuwa na faida lukuki ikiwemo usafiri na usafirishaji wa watu na bidhaa.
Akizungumza leo Juni 14, 2023 jijini Mwanza wakati wa kukagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa daraja la Kigongo – Busisi linalotajwa kuunganisha barabara kuu ya Usagara – Sengerema, Geita katika Ziwa Victoria, sambamba na kuunganisha watu wa mikoa ya Mwanza, Geita, Kagera na nchi jirani ya Uganda, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzanzia, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan aliwashukuru wananchi wa Mwanza na maeneo ya karibu kwa kutoa ushirikiano tangu kuanza kwa ujenzi wa daraja hilo hadi hatua ilipofikia.
“Daraja hili litakapokamilika ni faida kwa Watanzania wote lakini na kwenu nyie mlio karibu nalo, daraja hili limeanza kutoa ajira kwenu na litaendelea kutoa ajira kwa kuwa magari yatapita hapa kwenda maeneo mbalimbali, lakini niwaombe na wale wenye tabia ya wizi wa vifaa vya ujenzi waache na niwapongeze kwa kutoa ushirikiano wakati wote wa ujenzi”, amesema Rais Samia.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Mohamed Besta amesema kuwa kutokana na idadi kubwa ya magari yanayovuka kwa siku kivuko hutumia takribani hadi saa 2 kutoka upande mmoja kwenda mwingine, baada ya daraja kukamilika muda wa kuvuka Ziwa Viktoria unatarajiwa kupungua hadi kuwa takribani dakika nne.
Akifafanua baadhi ya manufaa ya daraja hilo linalotajwa kuwa daraja refu kuliko yote Afrika Mashariki na Kati na la sita katika bara la Afrika mara baada ya kukamilika kwake. Mhandisi Besta alisema,“Baada ya daraja kukamilika itarahisisha usafiri wa majira yote ya mwaka kwa saa 24 na kumaliza tatizo la msongamano wa magari unaotokea kila mara na kuwa kichocheo cha uchumi katika ukanda wa Ziwa Viktoria na taifa kwa ujumla kwani mazao ya wakulima na mazo ya samaki yataweza kufika sokoni kwa wakati”.
Aidha, Mhandishi Besta ameendelea kwa kusema kuwa ujenzi wa daraja hilo la Kigongo – Busisi ambalo ni kilomita tatu na barabara unganishi ni km 1. 66 linalofadhiliwa na Serikali kwa asilimia 100 unagharimu shilingi bilioni 716.33, ujenzi wake ulianza Februari 25, 2020 na unatarajiwa kukamilika Februari 24, 2024.
Aidha, kwa ujumla hatua ya utekelezaji wa mradi huo hadi sasa ni asilimia 75, na tayari mkandarasi ameshalipwa Shilingi bilioni 368.67, mhandisi mshauri amelipwa Shilingi bilioni 4, aidha Shilingi billion 3 zimetumika kufidia wananchi.