NA MICHAEL SARUNGI
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinaunga mkono jitihada zinazofanywa na taasisi, vikundi na watu binafsi
wanaopambana na vitendo vinavyoashiria kuvunja amani na utulivu nchini.
JAMHURI limefanya mahojiano na Katibu wa Siasa na Uhusiano wa Kimataifa wa Halmashauri Kuu ya
Taifa (NEC) ya CCM, Kanali mstaafu Ngemela Lubinga, kuhusu matukio kadhaa ya kisiasa na kijamii
yanayotokea nchini.
Katika mahojiano hayo yalifanyika wakati wa hafla ya ibada maalumu ya kumuombea Rais John
Magufuli, iliyoandaliwa na Kanisa la House of Prayer Shield of Faith Christian Fellowship lililopo Boko
Magengeni Dar es Salaam.
JAMHURI: Hivi karibuni kumekuwa na matukio yanayoashiria kuathiri amani, utulivu na umoja wa kitaifa;
miongoni mwa hayo yakihusishwa na siasa, hali hiyo unaizungumziaje?
LUBINGA: Suala la ulinzi wa amani na utulivu ni jukumu la Watanzania wote. Haifai kuiachia Serikali na
taasisi zake ambazo nazo zinategemea taarifa kutoka kwa wasamaria.
Matukio yanayoendelea kutokea siyo ya kufumbia macho na kila Mtanzania, mzalendo mwenye kuitakia
mema Tanzania na wananchi wake wa leo na kesho.
Hakuna kiongozi yeyote anayeweza kupendezwa na ongezeko la matukio ya kihalifu yanayoendelea
kujitokeza nchini, yanayoanza kuiweka Tanzania katika ramani mbaya machoni pa mataifa.
JAMHURI: Kumekuwa na malalamiko hasa ya wapinzani na vyama vya kiraia kwamba vinaminywa na
Serikali kuhusu haki za kidemokrasia ikiwamo kuzuiwa kwa mikutano ya hadhara na maandamano ya
amani, hivyo kushindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo. Una maoni gani kuhusu mtazamo huo?
LUBINGA: Upotoshaji unaoenezwa na baadhi ya watu kwa kumtuhumu Rais Magufuli kuwa amezuia
mikutano ya siasa ni visingizio vinavyopaswa kupuuzwa. Vyama vya upinzani vinapaswa kujitathmini juu
ya udhaifu wa demokrasia ndani yao, badala ya kuendelea kumhusisha Rais Magufuli pale
vinapokumbwa na misukosuko. Vyama hivyo havina nguvu hasa katika maeneo ya vijijini, udhaifu
ambao vimeshindwa kuufanyia kazi tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992.
Vyama vya siasa vinapaswa kuangalia njia sahihi ya kutanua mianya ya demokrasia ndani yao kabla
ya kuanza kunyoosha vidole kwa Rais Magufuli kwa kutoa visingizio vya kunyimwa nafasi.
Kutokana na vyama hivyo kukosa sera nzuri, mikakati ya pamoja na tabia ya viongozi wao vimeshindwa
kutumia mitaji ya wanachama wao kujijenga. Chama cha siasa chenye malengo ni lazima kisimamie na
kutekeleza kile inachokiamini katika itikadi yake, na ilani yake iliyoinadi kwa wananchi.
JAMHURI: Unautathmini vipi uhusiano wa CCM na vyama vingine vya upinzani hasa baada ya kuwapo
kwa shutuma za kuhusishwa na vurugu na wizi wa kura katika chaguzi mbalimbali zilizofanyika hapa
nchini siku za karibuni?
LUBINGA: Uhusiano na vyama vingine vya siasa upo japo kuna changamoto mbalimbali zinazohitaji
kufanyiwa kazi, kati ya wanasiasa wa vyama husika na chama tawala.
JAMHURI: Tangu kupatikana kwa uhuru wa Tanganyika (sasa Tanzania) mwaka 1961, Tanzania
ilijulikana kwa msimamo wa kutofungamana na upande wowote kimataifa na kupinga ubaguzi wa kila
aina, unautathmini vipi msimamo huo kwa hali ilivyo sasa?
LUBINGA: Siasa ya kutofungamana na upande wowote na kupinga ubaguzi na ukandamizaji ndivyo
vilivyoiwezesha Tanzania kuwa kitovu cha wapigania uhuru ndani ya nchi nyingi hasa barani Afrika. Sera
ya Tanzania kimataifa haijabadilika, bali imekuwa ikitekelezwa kulingana na mabadiliko yanayoendelea
kutokea duniani hasa upande wa diplomasia ya uchumi unaobadilika kila kukicha.
Diplomasia ya uchumi duniani imegeuka kuwa ni fursa kubwa itakayoiwezesha Tanzania kufikia azma
yake ya kuwa nchi ya viwanda ifikapo mwaka 2025, licha ya changamoto mbalimbali. Sasa ni jukumu la
balozi za Tanzania nje ya nchi kuona zinasaidia katika utafutaji wa masoko kwa ajili ya bidhaa za ndani
na kutangaza vivutio vya kitalii.
JAMHURI: Wakati wa utawala wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, uhusiano wa Tanzania na
nchi kama Israel haukuwa mzuri sana kutokana na uonevu wa nchi hiyo dhidi ya taifa la Palestina,
unaonaje msimamo wa sasa wa Tanzania katika eneo hilo?
LUBINGA: Tanzania ni moja ya nchi zinazoheshimika duniani baada ya waasisi wake kufanya kazi

kubwa ya kulijenga Taifa katika misingi ya umoja na mshikamano miongoni mwa watu wake.
Mzee Mkapa (Rais mstaafu Benjamin Mkapa) na Rais mstaafu Jakaya Kikwete alipokuwa Waziri wa
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, waliasisi sera mpya ya mambo ya nje, iliyojikita katika
diplomasia ya kiuchumi na kusaidia kuongeza washirika wa maendeleo.
Ni jukumu la viongozi kuendeleza msukumo wa diplomasia na siasa yetu ya kimataifa, unaojikita katika
kutafuta usawa na heshima baina ya mataifa na kushiriki katika jitihada za kutafuta na kulinda amani.