Kigogo CCM anaswa uraia
*Anyimwa pasipoti kwenda ziarani China
*Apanda vyeo na kushika nafasi nyeti nchini
*Apewa maelekezo mazito kutimiza masharti
*Baba aliingia Tanzania akiwa na miaka 3
NA WAANDISHI WETU, DODOMA
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mara, Samwel Kiboye (Nambatatu), anadaiwa kuwa si raia wa Tanzania, uchaunguzi wa JAMHURI umebaini.
Kiboye ambaye anajulikana pia kwa jina la Jared Samweli Kiboye, anakiri kuwa baba yake mzazi raia wa Kenya, aliingia Tanzania (baba) akiwa na umri wa miaka mitatu na kumuoa mama raia wa Tanzania.
Utata wa uraia wa Mwenyekiti huyo umemfanya anyimwe hati ya kusafiria kwenda nchini China kwenye ziara ya mafunzo akiwa na wenzake kutoka mikoa mbalimbali nchini.
Kiboye amezungumza na JAMHURI na kurusha lawama kwa wapinzani wake wa kisiasa, akisema wameshupalia suala hilo huku wakitambua kuwa yeye amezaliwa, amesoma na kufanya shughuli zote nchini Tanzania.
“Sitaki nilisemee jambo hilo sana kwa sababu liko kwenye mikono ya wakubwa huko. Naomba uwaulize hao wakubwa wao wataongea,” amesema.
Akitaja majina ya hao anaosema ni wakubwa (JAMHURI inahifadhi majina yao), amesema, “Sasa wewe ukiongea na wakubwa hao watakuwa kwenye nafasi nzuri ya kukuambia kinachoendelea. Mimi sijawahi kuwa raia wa Kenya bwana, ndio maana nimekwambia waulize hao wakubwa watakwambia.
“Vita niliyonayo siyo ya kawaida, mimi sijawahi kuwa Mkenya hata siku moja, hayo ni maneno tu watu wanasema. Ndiyo maana nimekwambia ongea na hao wakubwa watasema. Mimi ni Mtanzania, nimezaliwa Tanzania. Bibi yangu mzaa baba yangu ni Mtanzania, sheria inasema mmoja wa wazazi akiwa ni Mtanzania hata mtoto ni Mtanzania.
“Mimi nimezaliwa Tanzania, nimekulia Tanzania na nimesoma hapa hapa. Baba yangu nilimuuliza, maana sikuwa nayajua hayo, mimi nimesoma Shule ya Msingi Ryagati, lakini sasa kilichotokea ni kwamba nilimwuliza baba yangu, maana yeye anasema ni Mtanzania.
“Lakini jambo la uraia wangu lilianza wakati wa kampeni za urais, nikiwa Katibu Mwenezi wa Wilaya [Rorya], sasa wale wakawa wanalazimisha niunge mkono upinzani.
“Mimi sikumuunga mkono jitihada za waliokuwa viongozi wangu wa mkoa na wilaya, maana wao walitaka nimpigie debe Edward Lowassa, walikuwa wameteka kila mtu huku Mara. Baada ya kuwakatalia mpango wao ndio wakaanza kunitengenezea zengwe la uraia.”
Hata hivyo, Kiboye anakiri kuwa baba yake aliingia Tanzania akiwa mtoto mwenye umri wa miaka mitatu.
“Mimi baba yangu amekuja Tanzania, akiwa na umri wa miaka mitatu, baada ya bibi yangu kuachana na babu, bibi huyo alikuwa Mtanzania na baada ya kurudi Tanzania, bibi akafa. Baba yangu amekuja hapa kabla ya Uhuru, na hata Serikali ilisema watu wote waliokutwa wakati wa Uhuru wote ni raia, sasa nashangaa mambo haya yametoka wapi tena!
“Sasa baada ya kuniambia bibi alikuja hapa Tanzania akiwa amembeba baba yangu mgongoni, mpaka alishiriki kumwondoa mkoloni hapa… anasema walitangaziwa na Rais Julius Nyerere kwamba watu wote waliokutwa hapa na Uhuru, wote ni raia.
“Hii juzi tena imeibuka, na mpaka imeniacha hoi na sasa nimechoka. Nilikwenda kuongea na baba yangu ambaye sasa ana umri wa miaka 85 na mama yangu ni umri wa miaka 82. Hata Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Mwigulu Nchemba, nilimwambia haya ninayokuambia,” amesema Kiboye.
Kuhusu majina mawili- Jared Samweli Kiboye na Samwel Kiboye Nambatatu, anasema, “Hilo la Jared ndilo nimesomea. Sasa mimi niliamua kwenda mahakamani nikaomba nitumie majina yote mawili, nikasema naomba majina yote yawe yangu, hasa baada ya kuona jina la Samwel Kiboye Nambatatu limekuwa maarufu sana, mimi ni mwanasiasa, jina ambalo linaeleweka sana ni mtaji kwenye siasa.
“Hapo sasa ndio nikaamua kuachana na jina la JARED, lakini hilo ni jina ambalo nimesomea shule ya msingi, lakini likaja kumezwa na Samwel Kiboye, watu wamekuwa wakiniita Samwel…Samwel…Samwel… Ikabidi niombe kubadili jina, sasa jina la ‘Nambatatu’ ndilo limenipa ujiko, sasa kama nisingeomba kibali cha Mahakama kubadili jina mimi ningeanguka maana hilo linafahamika sana.
Kiboye amezungumza pia kuhusu tofauti ya tarehe zake za kuzaliwa kwenye leseni ya udereva na pia kwenye vitambulisho vingine.
“Yamekuwa yanasemwa mengi pia kuhusu [umri], mimi nimezaliwa lini, maana kuna nyaraka zinaonesha nimezaliwa Julai 25, 1969 na nyingine Agosti 6, 1968. Mimi ndio maana nimekwambia hawa wazee wanakosea miaka tu, tena hilo ni jambo la kawaida, mwaka wangu halisi wa kuzaliwa ni ule ambao uko kwenye kitambulisho cha kupigia kura ambao ni Agosti 6, 1968. Mwaka huo ndio uko kwenye nyaraka zote mpaka zile ambazo nimeandika kwenye fomu za kugombea Uenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara.
“Ninawajua jamaa ambao wanalishupalia jambo langu hili, lakini nashangaa kwa nini haya yote yanakuja leo baada ya kuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara. Naomba nikuambie leo wanaofanya yote haya ninawafahamu wote na nitapambana nao vizuri.
“…Ninaandamwa, mpaka sasa nimeshaletewa mpaka watu kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kutoka Dar es Salaam, waje kunichunguza hapa. Walikuja nikawapa ushirikiano wa kutosha na kuwaonesha nyumba zangu zote pamoja na biashara za mke wangu.
“Sasa mimi nimeteuliwa na Katibu Mkuu wa CCM, Kinana ili niende China, alikuja huku Makamu Mwenyekiti wa CCM, Phillip Mangula, akatangaza mbele za watu pale na hakuwa anajua kama pale ninapigwa vita. Nikamwambia Mzee Mangula, kesho nakwenda Dar es Salaam, kushughulikia mambo ya safari yangu, huku nyuma hao wabaya wangu nao wakafunga safari kwenda Dar es Salaam.
“Wakiwa Dar es Salaam, wakapambana kweli kweli kuhakikisha siendi hiyo safari yangu. Nimekwenda kuomba hati ya kusafiria, nikaambiwa niandike barua ya kukana uraia wangu. Niliambiwa kuandika barua ya kukana uraia wangu, nikaandika na ninakumbuka nilipewa karibu karatasi 200, baada ya kuandika nikapeleka na ikapelekwa kwa waziri na nimeshaambiwa imesainiwa,” amesema Kiboye.
Mkuu wa Mkoa (RC) wa Mara ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa huo, Adam Malima, amezungumza na JAMHURI kuhusu utata wa Kiboye, lakini amesema hana taarifa zozote.
JAMHURI: Wewe kama Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama na mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Mkoa, jambo hili unalifahamu?
RC MALIMA: Sasa wewe unataka kujua jambo gani? Sijaelewa!
JAMHURI: Jambo hili limeshafika ofisini kwako?
RC MALIMA: Wewe jambo la uraia wa Mwenyekiti wa CCM limefika kwako kwa utaratibu gani? Umesema wewe ni Mhariri wa JAMHURI, sasa suala la uraia wa Mwenyekiti wa CCM linafikaje kwako? Mimi silijui, kuna tatizo gani kwani?
JAMHURI: Kuna taarifa kwamba Nambatatu si raia, tunataka kujua kama taarifa hii unayo.
MALIMA: Mimi ni Mkuu wa Mkoa, sitaki tufanye masihala, nenda kawaulize waandishi wenzako, watakwambia kwamba Malima is very serious guy, if you want to come to me, come with a serious manner.[Malima ni mtu makini, kama unataka kuja kwangu njoo ukiwa na mambo ya msingi]
JAMHURI: Jambo hilo limeibuka baada ya baadhi wa Wenyeviti wa CCM, kupata safari ya kwenda nchini China na Mwenyekiti wa CCM, Mara hakwenda kutokana na hilo.
RC MALIMA: How…How…Huyu ni kiongozi wa CCM wa miaka mingi, aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Wilaya, Mwenezi wa Mkoa, alikuwa Umoja wa Vijana. Kama hakwenda China, pengine ni ubinadamu, labda alighafirika.
“Mimi namfahamu Nambatatu, muda mrefu, nimekataa kulishabikia suala la uraia wake maana ni majungu tu. JAMHURI ni ka-gazeti kadogo ambako kanaibua mambo mazito mazito, ni ka-gazeti ambako watu serious [makini] kama mimi tunakosoma. Sitarajii na ninyi mtakuwa kwenye mwendelezo wa majungu, ninakuhakikishia kwamba sina taarifa hiyo, na huwezi kuwa Mwenyekiti wa CCM kama si raia. Kuna watu aligombea nao akawachapa, nadhani ndio wanaleta jambo hili na ninaamini ni majungu tu.”
Habari kutoka Tarime zinasema baba yake Nambatatu, Mzee Jared Kiboye, jina lake liko kwenye daftari la wageni [watu wasio raia] ambako alijiorodhesha mwaka 2004. Pia inadaiwa kwamba Nambatatu aliingia nchini na wazazi wake mwaka 1973 akiwa mtoto.
Wiki iliyopita, Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi, Dk. Mwigulu Nchemba, akiwasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya fedha kwa mwaka 2018/2019 alizungumzia marekebisho ya Kanuni za Sheria ya Tanzania ya Uraia, Tangazo la Serikali Na. 427/2017 kwamba imetoa punguzo la ada ya uraia kutoka dola 5,000 za Marekani hadi Sh 2,000,000. Punguzo hilo la ada linawahusu waliozaliwa Tanganyika kabla na baada ya Uhuru ambao wazazi wao hawakutambulika kuwa raia wa Tanganyika kwa mujibu wa Sheria ya Uraia ya Tanganyika Sura Na. 512 ya mwaka 1961.
“Vilevile, Kanuni imejumuisha watu waliongia nchini Tanganyika kabla na baada ya Uhuru na kuendelea kuishi nchini kwa kipindi chote pamoja na watu waliozaliwa nje ya Tanzania kwa wazazi ambao ni raia kwa Tanzania kwa kurithi. Hivyo, natoa rai kwa watu hao kurekebisha hadhi yao ya uraia ili kukidhi matakwa ya Sheria,” alisema Dk. Nchemba.
Kumbukumbu zinaonyesha kuwa hii si mara ya kwanza kwa viongozi wa CCM kuwa na utata wa uraia wao. Mwaka 1995, CCM walimpitisha Azim Premji kugombea ubunge Jimbo la Kigoma Mjini, akiwa na utata wa uraia wake. Alishinda lakini matokeo yalitenguliwa na Mahakama kutokana na utata huo.
Premji akapewa uraia akawania tena ubunge kupambana na mgombea wa CHADEMA wakati huo, Dk. Aman Kabourou. Baadaye Premji akawa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kigoma.
Aliyekuwa Katibu Mwenezi wa CCM Zanzibar, Moudeline Castico, naye alibainika kuwa si raia wa Tanzania.
Kwenye mlolongo huo pia yumo aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kagera, Anatory Amani ambaye baadaye alilazimika kuomba uraia wa Tanzania baada ya kubainika kuwa hakuwa raia.
Balozi wa Tanzania nchini Nigeria, Timoth Bandora, naye ni miongoni mwa watu waliokuja kubainika baadaye kuwa si raia wa Tanzania.
ASIYE RAIA WA TANZANIA NI NANI?
Masuala ya uraia duniani kote yanaongozwa na falsafa kuu mbili ambazo ni Haki za Kidamu (Jus Sanguinis – The rights of blood), ambapo mtu hupata uraia kutokana na uhusiano wa kidamu na wazazi wenye uraia wa nchi husika. Hii ina maana kwamba, pamoja na mtu kuzaliwa katika nchi husika anatakiwa pia kuwa na mzazi ambaye ni raia wa nchi hiyo. Falsafa hii ndiyo inayofuatwa na nchi ya Tanzania.
Kwa maana nyingine kuzaliwa pekee nchini Tanzania hakumpi mtu haki ya moja kwa moja ya kuwa raia wa Tanzania, bali mtu atakuwa raia ikiwa amezaliwa Tanzania na wakati wa kuzaliwa kwake mzazi wake mmoja sharti awe ni raia wa Tanzania.
Falsafa nyingine ni (Jus Soli – The right of Soil), ambayo mtu hupata uraia kutokana na kuzaliwa kwake katika ardhi ya nchi fulani. Kufuatana na falsafa hii, mtu hupata uraia kutokana na kuzaliwa katika nchi husika bila kujali uraia wa wazazi wake.
Kwa Tanzania mtoto anayezaliwa katika ardhi ya Tanzania anaruhusiwa kuendelea kuwa na uraia wa nchi mbili hadi anapofikisha umri wa miaka 18 ndipo nanapaswa kukana ama uraia wa Tanzania au wa mzazi aliyemzaa ambaye hakuwa raia. Asipokana, moja kwa moja anapoteza uraia wa Tanzania na kuchukua uraia wa wazazi wake anapotimiza miaka 18.
URAIA WA TANZANIA
Masuala ya uraia nchini Tanzania yanasimamiwa na Sheria ya Uraia ya Tanzania ya mwaka 1995 Sura 357 kama ilivyorekebishwa mwaka 2002, pamoja na kanuni zake za mwaka 1997. Sheria hii imeanisha aina tatu za uraia wa Tanzania ambazo ni;
- Uraia wa Tanzania kwa kuzaliwa
- Uraia wa Tanzania kwa kurithi
- Uraia wa Tanzania kwa Tajnisi, au kujiandikisha.
Uraia wa Tanzania wa kuzaliwa: Utambuzi wa nani ni raia wa Tanzania unazingatia vipindi mbalimbali vya historia ya Tanzania, yaani kabla na baada ya uhuru wa Tanganyika, kabla na baada ya Mapinduzi ya Zanzibar na baada ya Muungano wa Tanzania. Pia, mahali alipozaliwa na alizaliwa na nani kama inavyoainishwa hapa chini:
Mtu aliyezaliwa Tanganyika kabla ya Uhuru alitambulika kuwa ni raia wa Tanganyika wa kuzaliwa, ikiwa mmoja wa wazazi wake alizaliwa Tanganyika na anatokana na raia wa Uingereza, makoloni yake au nchi zilizokuwa chini ya udhamini wa Uingereza.
Mtu aliyezaliwa Tanganyika baada ya Uhuru alitambulika kuwa ni raia wa Tanganyika wa kuzaliwa, ikiwa mmoja wa wazazi wake alikuwa raia wa Tanganyika. Mtu aliyezaliwa Zanzibar kabla na baada ya Mapinduzi alitambulika kuwa ni raia wa Zanzibar wa kuzaliwa.
Ila, mtu huyo hakutambulika kuwa ni raia wa Zanzibar ikiwa wazazi wake walitokana na mataifa yafuatayo; Australia, Ubeligiji, Canada, Ceylon (Sri Lanka), Ufaransa, Italia, New Zealand, Ureno, Jamhuri ya Israel, Afrika Kusini na Marekani.
Aliyezaliwa Tanzania siku na baada ya Muungano wa Tanzania:
Mtu aliyezaliwa katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania siku na baada ya Muungano, atatambulika kuwa ni raia wa Tanzania wa kuzaliwa ikiwa mmoja wa wazazi wake ni raia wa Tanzania.
Mtu hawezi kuwa raia wa Tanzania kwa kuzaliwa kama wakati wa kuzaliwa kwake hapa nchini, wazazi wake wote hawakuwa raia wa Tanzania; au baba yake ni balozi wa nchi ya kigeni na ana kinga ya kibalozi; au mmoja wa mzazi wake alikuwa ni adui wa nchi ya Tanzania na mtoto huyo alizaliwa katika eneo lililokuwa likikaliwa na adui.
Sheria ya Uraia ya Tanzania Sura 357 ya mwaka 1995 (R.E, 2002) ndiyo sheria pekee inayotambua sheria zote za nyuma, zilizokuwa zinasimamia masuala yote ya uraia katika vipindi mbalimbali vya historia ya Tanzania. Kwa mantiki hiyo mtu yeyote ambaye alikuwa raia wa Zanzibar au Tanganyika kwa kuzaliwa, kabla ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar tarehe 25/04/1964, ataendelea kuwa raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuzaliwa, mara baada Muungano.
Aidha, mtu yeyote kama hakutambulika kuwa raia wa Zanzibar au Tanganyika kabla ya Muungano, hatatambulika kuwa ni raia wa Tanzania mara baada ya Muungano.
URAIA WA TANZANIA KWA KURITHI:
Raia wa Tanzania kwa kurithi ni mtu aliyezaliwa nje ya Tanzania, na anatambuliwa kuwa raia wa Tanzania kutegemeana na kipindi alichozaliwa na uraia wa wazazi wake wakati wa kuzaliwa kwake kama ifuatavyo:
Mtu aliyezaliwa nje ya Tanganyika kabla ya Uhuru (akiwa ametokana na raia wa Uingereza na makoloni yake au himaya ya Mwingereza) alitambuliwa kuwa ni raia wa Tanganyika kwa kurithi endapo baba yake alikuwa raia wa Tanganyika.
Mtu aliyezaliwa nje ya Tanganyika baada ya Uhuru na kabla ya Muungano alitambuliwa kuwa ni raia wa Tanganyika kwa kurithi, ikiwa baba yake alikuwa raia wa Tanganyika.
Sheria ya Uraia ya Tanganyika ya mwaka 1961 haikutoa fursa kwa mama kumrithisha uraia mtoto wake aliyezaliwa nje ya nchi. Hivyo mtu aliyezaliwa nje ya Tanganyika katika vipindi tajwa hapo juu hakutambulika kuwa ni raia wa Tanganyika kwa kurithi kupitia mama yake.
Aidha, mtu aliyezaliwa nje ya Tanganyika hakutambuliwa kuwa raia wa Tanganyika kwa kurithi iwapo baba yake alikuwa raia wa Tanganyika kwa kurithi. Kwa tafsiri rahisi ni kwamba raia wa kurithi hawezi kurithisha tena uraia huo kwa mtoto wake aliyezaliwa nje ya Tanganyika.
Mtu aliyezaliwa nje ya Zanzibar kabla ya Muungano atakuwa raia wa Zanzibar kwa kurithi endapo baba yake ni raia wa Zanzibar. Vile vile, Sheria ya Uraia ya Zanzibar (The Zanzibar Nationality Decree, CAP 39, 1952) haikuruhusu mama raia wa Zanzibar kurithisha uraia kwa mtoto wake aliyezaliwa nje ya Zanzibar. Kwa maana nyingine, mtu aliyezaliwa nje ya Zanzibar katika kipindi hicho hakutambuliwa kuwa ni raia wa Zanzibar kwa kurithi kupitia kwa mama yake.
Mtu aliyezaliwa nje ya Zanzibar hakutambuliwa kuwa raia wa Zanzibar kwa kurithi ikiwa baba yake alikuwa raia wa Zanzibar kwa kurithi. Kwa tafsiri rahisi ni kwamba raia wa Zanzibar kwa kurithi hawezi kurithisha tena uraia huo kwa mtoto wake aliyezaliwa nje ya Zanzibar.
Mtu aliyezaliwa nje ya Tanzania siku na baada ya Muungano atakuwa raia wa Tanzania kwa kurithi endapo mzazi wake mmoja ni raia wa Tanzania kwa kuzaliwa au kuandikishwa/tajnisi. Ni vyema ieleweke kuwa mtu aliyezaliwa nje ya Tanzania hawezi kuwa raia wa Tanzania kwa kurithi iwapo baba/mama yake ni raia wa Tanzania kwa kurithi.
Sheria ya Uraia Sura ya 357 ya mwaka 1995 (R.E, 2002) imetoa fursa kwa mama ambaye ni raia wa Tanzania kwa kuzaliwa, tajnisi/ kuandikishwa kurithisha uraia wa Tanzania kwa mtoto wake aliyezaliwa nje ya Tanzania.
Aidha, mtu yeyote ambaye alikuwa raia wa Zanzibar au Tanganyika kwa kurithi, kabla ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar tarehe 25/04/1964 ataendelea kuwa raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa namna ile ile mara baada Muungano. Mtu yeyote kama hakutambulika kuwa raia wa Zanzibar au Tanganyika kwa kurithi kabla ya Muungano, hatatambulika kuwa raia wa Tanzania kwa kurithi mara baada ya Muungano. Haya yameainishwa katika Sheria ya Uraia ya Tanzania Na.6, 1995 (Sura 357, Rejeo la 2002) kifungu cha 30.
Mtu yoyote ambaye si raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuzaliwa au kurithi anaweza kuomba uraia wa Tanzania wa tajnisi kwa mujibu wa Sheria ya Uraia Sura 357 ya mwaka 1995, (R.E,2002).
Kwa mujibu wa sheria hiyo, Waziri mwenye dhamana ya kusimamia masuala ya uraia nchini (Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi), ndiye mwenye mamlaka ya mwisho ya kumpa au kutompa uraia wa Tanzania mgeni mwenye sifa anayeomba uraia.
Mgeni anaetaka kuomba uraia wa Tanzania anapaswa kuwa na sifa zifuatazo:
(i) Mwombaji awe na umri kuanzia miaka 18 na uwezo wa kufanya uamuzi unaokubalika kwa mujibu wa sheria za nchi,
(ii) Awe ameishi ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa muda wa miezi 12 mfululizo kabda ya kutuma maombi ya uraia,
(iii) Katika muda wa miaka 10 kabla ya miezi 12 hiyo awe ameishi ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kihalali kwa muda usiopungua miaka saba.
(iv) Awe anafahamu vizuri lugha ya Kiswahili au Kiingereza,
(v) Awe na tabia njema,
(vi) Awe na manufaa kwa taifa, yaani awe alichangia na anaendelea kuchangia katika ukuzaji wa uchumi, sayansi na teknolojia na utamaduni wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na
(vii) Awe anakusudia kuishi moja kwa moja ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwa ombi lake la uraia litakubaliwa.
Mgeni yeyote mwenye nia ya kuomba uraia wa tajnisi mwenye umri wa miaka 18 na kuendelea anatakiwa kufuata taratibu zifuatazo;
(i) Mwombaji anatakiwa kujaza fomu za maombi ya uraia ambazo zinapatikana katika ofisi zote za Uhamiaji za Wilaya, Mikoa, Afisi Kuu ya Uhamiaji, Zanzibar na Makao Makuu ya Uhamiaji, Dar es Salaam.
(ii) Mwombaji anatakiwa kutoa matangazo ya nia yake ya kuomba Uraia wa Tanzania mara mbili mfululizo kwenye magazeti yaliyosajiliwa Tanzania.
Mchakato wa kushughulikia maombi ya uraia ili kuhakikisha kuwa wageni wanaopewa uraia ni wale wenye manufaa kwa Taifa, maombi yote yanapaswa kupitia na kujadiliwa katika vikao vya Kamati za Ulinzi na Usalama za: Ngazi ya Kata au Shehia (kwa upande wa Zanzibar) katika ngazi ya Kata au Shehia anayoishi mwombaji, ambapo atahojiwa na maombi yake kujadiliwa na kikao hicho na hatimaye ombi lake kupelekwa ofisi ya Uhamiaji Wilaya kwa hatua zaidi.
Katika ngazi hii, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya itajadili maombi ya uraia yaliyowasilishwa kutoka ngazi ya Kata au Shehia, hatimaye maoni na mapendekezo yake hupelekwa katika ngazi ya mkoa.
Ngazi ya Mkoa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa nayo itajadili maombi yaliyowasilishwa na kutoa maoni na mapendekezo yake kuhusiana na ombi husika na hatimaye hutumwa kwa Kamishna Mkuu wa Uhamiaji, ambaye atatoa ushauri na mapendekezo yake kwa Waziri mwenye dhamana ya masuala ya uraia wa Tanzania kwa uamuzi.
Ombi la Uraia wa Tajnisi kwa Mwanamke aliyeolewa
Mwanamke mgeni ambaye ameolewa na raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wowote wa uhai wa ndoa yake, anaweza kuwasilisha maombi ya uraia wa Tanzania kwa tajnisi.
Ombi la uraia kwa mwanamke aliyeolewa linatakiwa kuwasilishwa pamoja na viambatanisho vifuatavyo;
(i)Cheti cha ndoa kilichosajiliwa na Mamlaka husika nchini
(ii) Pasipoti ya taifa lake ambayo haijaisha muda wake
(iii) Kibali cha kuishi nchini ambacho hakijaisha muda wake (Hati ya Mfuasi)
(iv) Vielelezo vinavyothibitisha kuwa mume wake ni raia wa Tanzania.
Ombi la Uraia wa Tajnisi kwa Mtoto
Sheria ya Uraia ya mwaka 1995 Sura 357 (RE 2002), inatoa fursa kwa mzazi au mlezi halali wa mtoto (asiye raia) wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kumuombea mtoto huyo uraia wa Tanzania. Baada ya maombi rasmi kuwasilishwa, Waziri mwenye dhamana ya uraia anaweza kuruhusu mtoto huyo aweze kupata uraia wa tajnisi.
Waziri mwenye dhamana na masuala ya uraia nchini (Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi) ndiye mwenye mamlaka ya mwisho ya kutoa au kutotoa uraia wa Tanzania kwa mwombaji yeyote kwa mujibu wa Sheria ya Uraia ya mwaka 1995 Sura 357, rejeo la 2002.