Aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika mkoani Kilimanjaro (KNCU), Maynard Swai, amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi, Arusha na Arumeru, jijini Arusha akishitakiwa kwa kosa la utakatishaji wa fedha.
Swai, ambaye pia ni mwenyekiti mstaafu wa Chama cha Wakulima Tanganyika (TFA), katika mashtaka hayo yumo pia ofisa wa benki moja Jijini hapa, Salvatory Mwandu, na Jesca Joseph ambaye ni mtumishi wa Ofisi ya Ustawi wa Jamii Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani.
Watuhumiwa hao wanashtakiwa kwa makosa manne likiwamo la kughushi nyaraka, wizi wa fedha na utakatishaji wa fedha – kosa ambalo kwa mujibu wa sheria, halina dhamana.
Walifikishwa mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Arusha na Arumeru, Deudedit Kamugisha, na kusomewa mashtaka hayo na Wakili wa Serikali, Blandina Msawa.
Kwa mujibu wa hati ya mashitaka iliyosomwa na wakili wa Serikali, shtaka la kwanza la kughushi nyaraka linamkabili mshitakiwa wa kwanza, Salvatory Mwandu, na mshitakiwa wa pili, Maynard Swai, wanaodaiwa kuiba Sh milioni 25 kwa kutumia nyaraka za kughushi.
Shtaka la pili pia linawahusu washitakiwa hao wawili – Mwandu na Swai – ambako ilidaiwa mahakamani hapo kuwa Novemba mwaka juzi, washitakiwa waliiba Sh25 milioni, mali ya TFA.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, shtaka la tatu linamkabili Swai pekee ambapo ilidaiwa kuwa Novemba 6, mwaka juzi, mshitakiwa alighushi nakala ya barua ikionesha ni mkurugenzi wa TFA.
Shtaka la nne na tano la utakatishaji fedha, linawakabili washitakiwa wote watatu ambapo ilidaiwa kuwa kati ya Novemba 19 na Desemba mwaka juzi, walifanya miamala mbalimbali ya fedha.
Miamala hiyo inadaiwa kufanywa kupitia akaunti za Benki ya NMB tawi la Maktaba Jijini Dar es Salaam na Arusha. Washitakiwa walikana mashtaka hayo ambapo wakili wa watuhumiwa hao, Felix Makene, aliiomba Mahakama kutengua shtaka la nne na la tano kuwa maelezo ya mashitaka hayo sio ya utakatishaji fedha.
Makene ameiambia Mahakama kuwa mashtaka hayo ni ya madai na wateja wake walishalipa fedha walizokuwa wanadaiwa na TFA ikawaandikia barua polisi kuthibitisha kupokea fedha hizo.
Hakimu Kamugisha, katika uamuzi wake mdogo, aliyakataa maombi hayo akisema mashitaka hayo yapo kwa mujibu wa sheria na kesi hiyo itatajwa Aprili 4 mwaka huu. Washtakiwa wamerudishwa mahabusu katika Gereza Kuu la Kisongo.
KASHFA NYINGINE KWA MAYNARD SWAI
Wakati kigogo huyo akisota mahabusu, mkoani Kilimanjaro, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) iko katika hatua za mwisho kukamilisha uchunguzi wa ufisadi wa karibu Sh bilioni 2 za kiwanda cha kukoboa kahawa (TCCCo).
Swai ambaye pia alikuwa mwenyekiti wa Bodi ya kiwanda hicho kutokana na nafasi yake katika Chama Kikuu cha Ushirika mkoani Kilimanjaro (KNCU), ni mongoni mwa watuhumiwa katika uchunguzi huo pamoja na meneja mkuu wa kiwanda hicho , Andrew Kleruu, wakituhumiwa kununua mtambo chakavu wa kukoboa kahawa.
Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Kilimanjaro, Alex Kuhanda, amethibitisha mchakato wa uchunguzi huo kuwa katika hatua za mwisho kabla ya watuhumiwa hao kupandishwa kizimbani.
Kiwanda hicho cha kukoboa kahawa ambacho ni kikubwa na cha aina yake katika ukanda wa Afrika mashariki, kinamilikiwa kwa aslimia 54 na KNCU huku chama cha wamiliki mashamba makubwa (TCGA) kikiwa na asilimia 36 ya hisa.
Vyama vingine vinne vikuu vya ushirika vya ACU, Usambara, MOFACU, RIVACU na Kanyovu vinamiliki asilimia 10 ya hisa zilizobaki katika kiwanda hicho kikubwa kuliko vyote Tanzania.
Kutokana na ufisadi huo, uzalishaji katika kiwanda hicho kwa sasa unasuasua huku wakulima wakilazimika kupeleka kahawa yao kwenye viwanda vya watu binafsi.
Kiwanda cha kukoboa kahawa cha Tanganyika Coffee Curing (TCCCo) cha mjini Moshi, kimeshindwa kuutumia mtambo wake mpya ulionunuliwa kwa zaidi ya Sh bilioni 1, kutokana na kuwapo kwa ufisadi uliokwaza mitambo hiyo kuanza kazi ya ukoboaji kahawa.
Mtambo huo unadaiwa kununuliwa nchini Brazil, kutoka kampuni ya Pinhalense baada ya Serikali kuridhia na bodi ya wakurugenzi wa kiwanda hicho kuuza mali zake ili kununua mtambo huo mpya.
Pamoja na kiasi hicho cha fedha kutumika kununua mtambo huo, hadi sasa umeshindwa kuanza kutumika tofauti na matarajio ya wengi huku mtambo unaotajwa kuwa ni mbovu na haufai ukiwa unaendelea kukoboa kahawa.
Uchunguzi uliofanywa na JAMHURI umebaini kuwa baadhi ya vifaa vimekuwa vikinyofolewa kutoka mtambo wa zamani na kufungwa kwenye mtambo mpya, hatua ambayo imeibua maswali mengi kuliko majibu.
Mwenyekiti wa sasa wa Bodi hiyo, Alois Kittau, amesema hana anachokijua kuhusiana na mtambo huo mpya, kwani tangu akalie kiti hicho mwaka juzi hajawahi kukabidhiwa nyaraka za ununuzi wa mtambo huo na wala hajui thamani halisi iliyotumika kununua mtambo huo.
Kittau ameliambia JAMHURI kuwa tayari bodi yake imeanza mchakato wa kutafuta wakaguzi wa hesabu kwa ajili ya kuchunguza mchakato mzima wa uuzwaji wa mali za kiwanda hicho, ambapo fedha zilizopatikana zilitumika kununua mtambo huo huku kiasi kingine kikiwa hakijulikani matumizi yake.
Sababu za kuuzwa kwa mali hizo zikiwamo nyumba, ilikuwa ni kununua mtambo huo mpya ili kukiwezesha kiwanda hicho kujiendesha kwa ufanisi na kulipa madeni ya kisheria ya zaidi ya Sh milioni 800, ambayo kiwanda hicho kinadaiwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Shirka Taifa la Hifadhi za Jamii (NSSF), Manispaa ya Moshi pamoja na madeni ya manunuzi.
Katika mkutano wake na waandishi wa habari, Machi 2013, Maynard Swai akiwa mwenyekiti wa bodi ya kiwanda hicho, alitaja madeni hayo ya kisheria kwa upande wa TRA ni Sh 377,541,680, NSSF Sh 163,391,438, Manispaa ya Moshi Sh 78,188,287, Astra Insurance Sh 44,064,038, madeni ya watumishi yakiwamo mafao ya kustaafu Sh 59,877,236.
Kiwanda hicho kinadaiwa ada ya ukaguzi wa hesabu kutoka shirika la kukagua hesabu za vyama vya ushirika (COASCO) wanaodai Sh 10,000,000, wakati SACCOs ya kiwanda hicho ikidai Sh milioni 2.800,000 huku madeni ya ununuzi yakiwa ni Sh 75,509,612 – madeni haya ni kufikia mwaka 2013.
Tayari meneja wa kiwanda hicho, Andrew Kleruu, amesimamishwa kazi kupisha uchunguzi wa tuhuma mbalimbali zikiwamo za kuhusika na upotevu wa kahawa kilo 245 kutoka vyama vinne vya ushirika ambavyo vimekuwa vikitumia kiwanda hicho kukoboa kahawa yao.
Vyama hivyo ni Isuki Amcos chenye kilo 63,Orori Amcos (kilo 135),Uduru Makoa (kilo 74) na Sonu Ngira cheche jumla ya kilo 74 ambazo meneja huyo alikiri kimaandishi kuwapo na upotevu huo katika barua yake ya Novemba, 2015 aliyomwandikia meneja wa vyama vinavyounda ushirika wa G32 KNCI-JVE Ltd.
Kittau ameliambia JAMHURI kuwa meneja huyo ambaye kwa sasa anachunguzwa na Jeshi la Polisi, ameshindwa kuonesha nyaraka zinazohusiana na uuzwaji wa mali za kiwanda pamoja na nyaraka za ununuzi wa mtambo huo mpya.
Taarifa ya mwenyekiti huyo kwa wanahabari ambayo nakala yake tunayo, ilieleza kuwa athari zinazosababishwa na uchakavu wa mitambo hiyo iliyojengwa miaka 60 iliyopita chini ya Mjerumani Heins Bueb, ni pamoja na kushuka kwa kiwango cha ukoboaji kutoka tani 65,736 msimu wa 1980/81 hadi kufikia tani 3,487 msimu wa 2012/2013.
Athari nyingine ni kushuka kwa ubora wa ukoboaji kunakochangiwa na kupondwa, punje kuvunjwavunjwa; hatua ambayo amesema inasababisha hasara kwenye madaraja na kupanda kwa kiwango cha hasara kwa mkulima.
Mwenyekiti huyo wa zamani wa bodi amesema katika kujikwamua na janga hilo, kiwanda kililazimika kupunguza wafanyakazi wake kutoka 660 hadi wafanyakazi 65, jambo ambalo lilifanywa kwa awamu nne kuanzia mwaka 1996 hadi mwaka 2003.
Pamoja na kupunguza wafanyakazi, Swai alinukuliwa akisema bado gharama za uendeshaji ziko juu kutokana na uchakavu mkubwa wa mitambo ambayo ina umri wa miaka 40, na kushuka kwa kiwango cha mapokezi ya kahawa.
Amesema kushuka kwa kiwango cha ukoboaji kahawa katika kiwanda hicho, kumechangiwa pia na hatua ya Serikali kuruhusu mfumo wa soko huria ambao uliruhusu wanunuzi binafsi wa kahawa kujenga viwanda vyao.
Viwanda hivyo vya kukoboa kahawa vya watu binafsi katika ukanda wa kaskazini vipo viwanda vinne ambavyo vimekuwa mshindani mkubwa wa kiwanda hicho kutokana na wakulima wengi kukimbilia huko.
Sababu nyingine zinazosababisha kiwanda hicho kufanya kazi chini ya asilimia 10 ya uwezo wake, zimetajwa kuwa ni kushuka kwa uzalishaji wa zao hilo katika mikoa ya kanda ya kaskazini kutokana na hali ya ukame, kushuka kwa bei ya kahawa kwenye soko la dunia, kupanda kwa bei ya pembejeo na kuharibika kwa taratibu za kuhudumia zao la kahawa .
“Bodi ilitafakari kwa kina hali ya kiwanda na kuona umuhimu wa kununua mtambo mmoja wa kisasa ili kunusuru kiwanda, mtambo unaotegemewa kununuliwa na uwezo wa kupunguza gharama ikilinganishwa na mtambo uliopo,” inasema sehemu ya taarifa ya bodi.
Taaifa za awali zinaonesha mtambo huo una uwezo wa kukoboa tani sita za kahawa kwa saa moja badala ya mitambo minne chakavu ya sasa inayokoboa kahawa chini ya tani tatu kwa saa moja.
Mtambo huo mpya ungepunguza gharama za umeme kwa zaidi ya nusu ya gharama za sasa kutokana na mtambo huo mpya kuwa na “installed capacity” ya 165KW dhidi ya 431 KW kwa mtambo wa zamani.