Mkuu wa Idara ya Uhamiaji Mkoa wa Dar es Salaam (RIO), John Msumule, ameibeba Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kwa kupuuza agizo la kufanya ukaguzi kwa wafanyakazi kiwandani hapo.
Vyanzo vya habari vya uhakika kutoka idarani humo vimedokeza kuwa Uhamiaji walitakiwa kufanya upekuzi wa kushtukiza katika kiwanda cha bia kilichopo Ilala jijini Dar es Salaam, lakini katika hali ya kushangaza ukaguzi huo haukufanyika kama ilivyoamuriwa na viongozi wa Uhamiaji Makao Makuu.
Maafisa Uhamiaji walifika kiwandani hapo wakiongozwa na Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa (Chief Investigation Officer), Pima Salleh, ambapo baada ya kufika waliwasiliana na uongozi, hawakuweza kufanya upekuzi wa aina yoyote ile zaidi ya kuutaka uongozi kuwasilisha majina na nyaraka za wafanyakazi wa kigeni katika ofisi ya Uhamiaji Mkoa kisha waliondoka na kurudi ofisini.
Aidha inaelezwa kuwa siku iliyofuata, Afisa Rasilimali Watu kutoka TBL alifika ofisi ya Uhamiaji Mkoa na kuwasilisha nyaraka za wafanyakazi 29 tu wa kigeni waliopo kiwandani hapo.
“Tulitarajia kufanyika upekuzi kiwandani kama ambavyo hufanyika katika kufuatilia ukamataji, lakini siku hizi ni kulipua tu kazi, mnafika sehemu na kufuata maagizao tu ya bosi anavyotaka, hakuna upekuzi” anasema mtoa taarifa wetu.
JAMHURI imefanya mahojiano na Mkuu wa Uhamiaji Mkoa, John Msumule, ambaye amekiri kupokea nyaraka za wafanyakazi wa kigeni wa kiwanda cha bia (TBL).
Msumule anasema kuwa kama kuna kampuni wamefanya nazo kazi vizuri ni TBL na kuwa kampuni hiyo imewasilisha orodha ya majina ya wafanyakazi wao wote, huku wale wa kigeni wakiwa wameambatanishiwa vibali vyao vya ukaazi, hati zao za kusafiria, vyeti vyao vya shule pamoja na mikataba ya ajira.
Aidha, anasema kuwa wafanyakazi wa kigeni waliopo kiwandani hapo ni 29 tu na wote wanazo nyaraka halali ambao pia wamekidhi vigezo.
Alipoulizwa kuhusiana na maafisa wake kutofanya upekuzi wa aina yoyote kiwandani hapo, ameng’aka na kusema kuwa “akutukanaye hakuchagulii tusi” na kuendelea kusema kuwa maafisa wake walizunguka kiwandani humo na kufanya upekuzi wa kina kiwandani humo.
“Vijana wangu wamefanya kazi kubwa, tena wanafanya kazi mpaka usiku pamoja na kuwa hatuna vitendea kazi, hatuwalipi kwa kazi za usiku lakini hawavunjiki moyo. Wamefika TBL na kufanya upekuzi wa kina na hizo taarifa uliazo nazo si za kweli hata kidogo” anasema Msumule.
Gazeti hili lilitaka kupata ufafanuzi kuhusiana na kuwapo kwa taarifa za mmoja wa viongozi wa kampuni hiyo kuishi nchini bila kuwa na kibali ambapo Msumule anasema kuwa hakuna mwekezaji wa kiwanda hicho ambaye anaishi hapa nchini bali wote huingia nchini na kuondoka hivyo taarifa hizo si za kweli.
“Kwanza hakuna kaburu ambaye yupo hapa nchini, wote wanaishi nje ya nchi, na hilo suala la kuwapo kwa kiongozi kuishi bila vibali ni ngumu na ni maajabu nimesikia kutoka kwako, lakini hilo haliwezekani” anasema Msumule.
JAMHURI imefanya mahojiano na Mkuu wa Kitengo cha Upelelezi, Pima Salleh, kutaka kufahamu upekuzi uliofanywa kiwandani hapo ambapo amesema kuwa ni kweli walifika kiwandani hapo lakini yeye si mwongeaji bali atafutwe mkuu wake wa kazi.
“Ni kweli tulikwenda TBL, lakini nini kilitokea ni vyema ukaonana na RIO yeye ndiye mwenye mamlaka ya kuzungumzia masuala yote ya mkoa mimi siyo msemaji,” anasema Pima.
Kampuni ya TBL inao wafanyakazi wa kigeni 43 tofauti na idadi ambayo Msumule ameitoa kwa gazeti hili, jambo ambalo linakinzana na takwimu zilizoonwa na gazeti hili.
Wakati huo huo, taarifa lilizozipata JAMHURI kutoka jijini Nairobi, Kenya, zinasema Serikali ya Kenya tangu mwishoni kwa mwaka jana imefanya uchunguzi na kubaini kuwa bidhaa za TBL zilizouzwa kwa kampuni ya Crown Beverage kutoka TBL Group zilishushwa bei kwa asilimia 30.
“Wanachofanya sasa ni kuanza kuwadai kodi. Wamewaandikia wanataka TBL walipe tofauti ya kodi waliyokwepa,” kinasema chanzo chetu.
JAMHURI imefanikiwa kuona barua ya Machi 23, 2015 ambayo Mkurugenzi wa Fedha wa Crown Beverage Limited ya Kenya, Nigel Todd, alipokuwa akiomba msaada kutoka Tanzania.
Katika hali ya taharuki, mkurugenzi huyo aliomba kujulishwa wanafanyaje kuepuka madai yenye ukweli ya Serikali ya Kenya, baada ya kuwa wamepewa taarifa ya uchunguzi ya Mamlaka ya Kodi ya Kenya (KRA) Machi 19, 2015 ikiwataja wajiandae kulipa tofauti ya kodi waliyokwepa.
Uchunguzi wa ActionAid
SABmiller haiko peke yao katika mkondo huo. Njia zao za kuepuka kodi si za ajabu. Zinafanywa na kampuni nyingi za kimataifa kila sehemu duniani. ActionAid inaamini wanapaswa kubadilika.
SABmiller inapaswa kutambua kuwa inapaswa kuchukulia maendeleo endelevu kwa umakini kuhakikisha inachangamana na jamii yetu inakoendesha biashara.
Kwa mujibu wa Mtendaji Mkuu wa SABmiller, Graham Mackay, “Kwa mchango mkubwa biashara inaweza kuleta maendeleo kupitia kila kitendo cha kuendesha biashara kwa kulipa wazabuni, kwa kulipa mishahara na kulipa kodi.”
Hata hivyo, kampuni hii haina mpango mkakati endelevu wa kulipa kodi. Wala haitajwi popote katika vipaumbele vyake kumi au katika maadili ya biashara iliyojiwekea. Kampuni yoyote inayotaka kuwa kiongozi katika maendeleo ya kweli inapaswa kulichukulia suala hili kwa umakini mkubwa.
ActionAid inaitaka SABmiller kufanya mambo matatu; 1. Kuchukua mtazamo wa uwajibikaji katika kodi, kwa kuacha kutumia nchi ambazo ni pepo ya kodi kuiba faida kutoka Afrika kwa mfano, kwa kuacha malipo makubwa inayoyafanya ya haki za nembo na tozo za usimamizi kwa nchi za Uswisi na Uholanzi.
2. Inapaswa kutambua na kuweka wazi madhara ya kukwepa kodi. SABmiller inahitaji maadili ya kodi kueleza jinsi gani inavyoweka maendeleo endelevu katika misingi ya masuala ya kodi. Inapaswa kuwa wazi juu ya masuala yake ya kodi na mbinu za uepukaji.
3. Inapaswa kuwa wazi zaidi katika masuala ya taarifa za fedha. Itoe taarifa zake hadharani juu ya kampuni zake tanzu hasa hasa kampuni ambazo zipo kwenye nchi ambazo akaunti zake ni siri. Itoe nchi kwa nchi, kiwango inacholipa na taarifa za fedha.
Je, unafahamu ni mbinu zipi inazitumia SABmiller za kisheria kukwepa au kuepuka mkono wa dola katika nchi za Afrika isiweze kulipa kodi stahiki? Usikose toleo lijalo.