Tangu mwaka jana juhudi za chini chini zilianza kufanywa na baadhi ya Watanzania ambao hawajaridhika kuwa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, alifariki kifo cha kawaida.
Wito sasa umeanza kutolewa wa kuhakikisha kuwa kifo hicho kinachunguzwa kama inavyofanywa sasa kwa aliyekuwa Kiongozi wa Palestina, Yasser Arafat, ambaye taarifa za karibuni zinasemekana kuwa aliuawa kwa kulishwa sumu.
Baadhi ya wafuasi wa Mwalimu Nyerere, wamekuwa wagumu kuamini kama kweli Mwalimu alikufa kifo cha kawaida, kutokana na ukweli kwamba maradhi yaliyomuua – saratani ya damu (leukemia) – hayana desturi ya kuua kwa kasi kama ilivyotokea kwake.
Samuel Kasori, aliyekuwa Katibu Myeka wa Mwalimu, amezungumza na JAMHURI na kusema; “Mwalimu anakuwa kwenye rekodi ya kufa haraka sana kwa ugonjwa wa saratani ya damu. Ugonjwa huo huua taratibu, lakini kwa Mwalimu ilikuwa tofauti kabisa. Kuna nini kilichotokea? Sitaki kuhoji sana, lakini naamini kuna siku Watanzania na walimwengu wataujua ukweli.”
Maneno ya Kasori yanaendana na ya Mwalimu James Irenge (Mwalimu wa Baba wa Taifa), aliyoyatoa mwanzoni mwa mwaka jana baada ya mvutano wa kisiasa kati ya Rais mstaafu Benjamin Mkapa, na Mbunge wa Musoma Mjini, Vincent Nyerere (Chadema).
Baada ya kauli ya Mbunge Nyerere kumtaka Mzee Mkapa aeleze chanzo cha kifo cha Mwalimu, Mwalimu Irenge alijitokeza na kusema amefurahishwa mno kusikia kuwa amepatikana kiongozi jasiri wa kuhoji namna Mwalimu alivyougua hadi kufariki dunia.
“Mfikishieni pongezi nyingi Mbunge Nyerere… huyo mtoto amefanya jambo la maana sana kuuliza jambo hili, miaka yote nalia kwa sababu naamini Mwalimu aliuawa.
“Kwa kuwa suala hili limeulizwa hadharani, sasa nipo radhi kufa. Nikifa nitakwenda moyo wangu ukiwa na furaha kwa sababu nimekuwa nikijiuliza ni nani anayeweza kuhoji namna Mwalimu… mwanafunzi wangu alivyokufa,” alisema Mwalimu Irenge.
Kauli hiyo ya Mwalimu Irenge ya Machi, mwaka jana haikupita bure, kwani Julai, mwaka huo, aliaga dunia mjini Musoma na kuzikwa kijijini kwake Busegwe Nyanza wilayani Butiama.
Mwalimu Irenge alianza kumfundisha Mwalimu Nyerere katika Shule ya Mwisenge kuanzia mwaka 1934 hadi 1936. Mwalimu Irenge aliwahi kuhojiwa na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) na kusema, binafsi hakuafiki Mwalimu kupelekwa kutibiwa nchini Uingereza.
Alisema alipinga kwa sababu alijua Waingereza si marafiki wa kweli wa Mwalimu, kwa kuwa aliongoza harakati za kuwang’oa katika Tanganyika na katika mataifa mengine, hasa Afrika Kusini na Zimbabwe, ambako Serikali ya nchi hiyo ilikuwa ikiunga mkono utawala wa kidhalimu wa Wazungu wachache.
Mwakyusa na kifo cha Mwalimu
Profesa David Mwakyusa alikuwa daktari wa Baba wa Taifa tangu mwaka 1987 hadi Oktoba 14, 1999, siku Mwalimu alipofikwa na mauti jijini London, Uingereza, kutokana na ugonjwa wa saratani ya damu (leukemia).
Katika mahojiano aliyopata kufanya muda mfupi baada ya kifo cha Mwalimu, Profesa Mwakyusa alisema walimjulisha Mwalimu kila kitu kuhusu ugomjwa wa leukemia. Hata hivyo, kwenye maelezo yake anathibitisha namna ugonjwa huo ulivyobadilika ghafla na kumsababishia mauti, ilhali kila alipopimwa ilionekana hakuwa na sababu za kuanza matibabu mapema.
Swali: Mwalimu alikuwa anajulikana kwa Watanzania kama mtu mwenye afya nzuri. Wewe kama daktari wake unasemaje kuhusu afya ya Mwalimu kwa ujumla.
ibu: Mwalimu alikuwa mtu mwenye afya nzuri kwa ujumla, ukiacha matatizo madogo madogo ninayoweza kuyaita ya kawaida. Alikuwa na desturi ya kufanya mazoezi na alikuwa mtu anayefuata masharti na ushauri aliokuwa akipewa na madaktari.
Daktari wa kwanza aliyekuwa anamhudumia Mwalimu baada ya Uhuru alikuwa Profesa Mhonoli. Kuanzia mwaka 1979 alihudumiwa na Profesa Makene akisaidiwa na Profesa Mtulia na mimi. Mwalimu alipostaafu mwaka 1985 alibakia daktari mmoja tu, Profesa Makene. Makene alistaafu mwishoni mwa mwaka 1987 na tangu wakatu huo mimi ndiye niliyekuwa daktari wake hadi alipoaga dunia tarehe 14 Oktoba 1999.
Swali: Baada ya kulazwa katika Hospitali ya Mtakatifu Thomas jijini London, ndipo Watanzania tulipotangaziwa kwamba Mwalimu aligundulika kuwa na ugonjwa wa kansa ya damu mwishoni mwa mwaka 1998. Je, ugonjwa huu unafikiri aliupataje?
Jibu: Ugonjwa wa kansa ya chembe chembe nyeupe za damu, huwapata watu wenye umri mkubwa na utafiti wa kisayansi haujafanikiwa kutambua ni kitu gani hasa kinacholeta kansa hii. Kwa kawaida, kansa hii haioneshi dalili wakati inapoanza na wengi wanagundulika kuwa nayo bila kuihisi.
Wagonjwa wengi wanaishi zaidi ya miaka miwili bila kuhitaji matibabu, ni pale tu ambako kansa hii inapoathiri kazi ya chembe chembe nyingine nyeupe au nyekundu ndipo matibabu yanapoweza kufikiriwa.
Kinachohitajika ni mgonjwa kuonwa na daktari mara kwa mara, ili athari hizi zikionekana matibabu yaanze mara moja.
Swali: Baada ya kugundulika kwa ugonjwa wa Mwalimu, ulimshughulikia namna gani?
Jibu: Baada ya Mwalimu kugundulika kuwa na kansa mwezi Agosti 1998, alielezwa kuhusu ugunduzi huo na kuambiwa kuwa wakati ule ugonjwa ulikuwa haujafikia hatua ya kuhitaji matibabu. Alielezwa haja ya kwenda kupimwa mara nyingi zaidi kuliko ilivyokuwa kawaida yake na kwamba hapakuwa na sababu ya kubadilisha mwenendo wa shughuli zake.
Ratiba tuliyopewa ilimfanya Mwalimu arejee London, Novemba 1998, na majibu yaliyoonesha kuwa hakukuwa na sababu ya kuanza matibabu. Aidha, mwezi Januari 1999 alipimwa tena kwa mara nyingine ikaonekana hakuna haja ya kuanza matibabu.
Mwezi Mei 1999 alikwenda tena London akapimwa. Aliambiwa hakukuwa na sababu ya kuanza matibabu na akapewa tarehe nyingine mwezi Agosti, 1999.
Safari hii hitilafu zikaonekana katika damu. Hitilafu hizo zilionesha ulazima wa matibabu ya kansa kuanzishwa. Mwalimu alishauriwa kurudi London, Desemba 1999. Lakini hali yake ikabadilika kabla ya kurejea nyumbani hadi ikabidi alazwe katika hospitali ya Mtakatifu Thomas ambako alipoteza maisha yake.
Swali: Mmoja wa watoto wa Mwalimu amedai kuwa familia haikujulishwa kuhusu ugonjwa wa Mwalimu. Kuna ukweli wowote katika madai hayo?
Jibu: Mwalimu mwenyewe aliwaeleza baadhi ya wanafamilia yake waliokuwa karibu naye, kuhusu maradhi yake na mimi nilijua hivyo kwa vile hao aliowaeleza waliniambia na wakawa wakiniuliza maswali kuhusu ugonjwa wake.
Swali: Ukiwa daktari wa Mwalimu kwa muda mrefu, uliyekuwa ukisafiri naye mara nyingi na kuwa naye karibu, je, unaweza kuzungumzia lolote kuhusu maisha yake?
Jibu: Mara nyingi tukiwa pamoja aliuliza maswali mengi kuhusu ugonjwa wake na alisoma vijitabu kuhusiana na ugonjwa huo. Nadiriki kusema kwamba aliufahamu ugonjwa huo kwa kina.
Madaraka Nyerere azungumza
Madaraka Nyerere, mmoja wa watoto wanane wa Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere, amezungumza na kusema ingawa haafiki kuanza uchunguzi wa kifo cha babake, lakini kuna viashiria fulani fulani vinavyotia shaka.
Viashiria hivyo, kwa mujibu wa Madaraka, ni namna alivyoanza kuikosoa Serikali kwa mambo mengi, jambo analosema inawezekana halikuwafurahisha wengi.
Katika mahojiano yake na JAMHURI wakati huu wa maadhimisho ya miaka 14 ya kifo cha Baba wa Taifa, Madaraka ambaye kwa kawaida ni mpole, ameeleza yafuatayo:
“Binadamu wengi wanapenda sana kuamini kuwa kila jambo likitokea, basi kuna mkono wa mtu. Na hivi karibuni kifo cha Mwalimu Nyerere kimehusishwa na njama mahususi za kumuua.
“Kwa desturi za Kizanaki, hakuna mtu anayekufa kwa sababu ya ugonjwa au uzee, lazima yuko mtu miongoni mwa wale waliobaki hai ambao wamesababisha kifo chake kwa njia za uchawi. Kwa mfano, Bibi Christina Mugaya wa Nyang’ombe, mama mzazi wa Mwalimu Nyerere, mara baada ya kifo cha mume wake, Mtemi Nyerere Burito, tarehe 30 Machi 1942, alitimuliwa Butiama na kuhamia kwa ndugu zake katika kijiji jirani cha Muryaza, baada ya kutuhumiwa kuwa alisababisha kifo cha mume wake.
“Kwa hiyo hakurithiwa kama ilivyo desturi za wakati ule za mila za Kizanaki na akaishi kwa jamaa zake hadi Mwalimu Nyerere alipotoka masomoni Uingereza na kudai arudi nyumbani na akarudi, ingawa baadhi ya ndugu zake hawakufurahia kurudi kwake Butiama.
“Kwa hiyo basi, ni kawaida kabisa kwa hisia kama hizi kuwapo ndani ya jamii. Lakini, kusema hivi haina maana kuwa haiwezekani kuwa tuhuma hizo ni za kweli. Lakini mtu yeyote muungwana hawezi kuanza kutoa shutuma nzito kama hizi bila kuwa na ushahidi usiotiliwa shaka na ambao hauna dosari.
“Lakini naweza kuelewa kwanini baadhi ya watu ambao wanashikilia hizi tuhuma kuwa zinaweza kuwa ni kweli. Tunamfahamu Mwalimu Nyerere kuwa, hata baada ya kustaafu, hakukalia kimya uamuzi au matukio ambayo aliamini yanaathiri baadhi ya misingi ambayo yeye aliiona kuwa ni nguzo inayoshikilia nchi yetu. Baadhi ya haya ni uadilifu ndani ya uongozi, umoja, uzalendo, na sera zenye kujali masilahi ya wengi badala ya sera zinazokuza na kulinda nafasi kwa wachache kujinufaisha.
“Na kwa kweli ukichunguza baadhi ya matukio kwenye nyanja ya siasa katika kipindi hiki ambacho amefariki, yametokea mengi ambayo tunaamini kuwa kama angekuwa hai asingenyamaza na angeyazungumzia kuyapinga na kuyakemea au kuyatungia kitabu pale ambako ujumbe wake aliona unapuuzwa.
Kwa hiyo, mtu yeyote anayefuatilia hali ya uongozi nchini, na watu wengi wanasema hivi, ni kuwa Mwalimu Nyerere angekuwapo labda baadhi ya uamuzi na mienendo ya baadhi ya viongozi wetu ungekuwa tofauti kwa kuogopa kauli yake au kuandikiwa kitabu , kitakachojenga hoja inayopingana na uamuzi wa viongozi. Na pengine baadhi ya uamuzi ambao umefanyika, usingefanyika.
“Kwa hiyo kwa mantiki hii unaweza kuanza kujenga hoja kuwa baadhi ya wale waliofanya uamuzi unaoonekana unaenda kinyume au na maadili ya uongozi, au unapingana na masilahi ya umma, walitafakari kuwa njia rahisi ya kurahisisha mipango yao ni kumuondoa huyu mzee mapema. Hiyo unaweza kusema, lakini haitakuwa sahihi kufanya hivyo bila kuwa na ushahidi.
“Nimewahi kusikia tuhuma kuwa Rais Kikwete anatuhumiwa kuwa ndiye mtu aliyetumwa na nchi za Magharibi kukimaliza Chama Cha Mapinduzi (CCM). Nilivyosikia tuhuma hizi niliona kichekesho, lakini ukiangalia baadhi ya matukio katika uongozi wake ambayo yanaweza kuashiria hoja hiyo, unaweza kuyapata.
“Enzi za Mwalimu Nyerere waliotuhumiwa kwa makosa mbalimbali ya uongozi waliitwa pembeni na kuambiwa wajiuzulu. Miaka ya hivi karibuni wale ambao walikabiliwa na tuhuma za aina hiyo waliombwa kutafakari wao wenyewe uamuzi sahihi wa kuchukua. Uamuzi mgumu haufanyiki, upinzani wanapata mada ya kuzungumzia kwenye mkutano wao ujao, na CCM inazidi kudhoofu. Kama nilivyosema hakuna ushahidi wa wazi, lakini kuna viashiria tu.
“Nafikiri njia nzuri ya kufunga mjadala huu ni kuzungumza kama wanasheria wanavyosema: hakuna ushahidi mpaka sasa unaothibitisha hizo tuhuma juu ya njama za kumuua Mwalimu Nyerere.
“Hoja kuwa uchunguzi ufanyike kubaini kama aliuawa, sioni kama zitaleta faida yoyote kwa sababu ameshafariki tayari na hakuna uchunguzi utakaorudisha uhai wake. Tunamkumbuka Mwalimu Nyerere kwa maandishi na matamshi yake. Na naamini kuwa katika uhai wake aliandika na kutamka masuala yote aliyoamini ni ya msingi kwake na kwa jamii.
“Kuna kiongozi mmoja aliyewahi kusema iwapo kuna wazo la msingi ambalo binadamu amelisema katika uhai wake, basi hilo wazo litadumu hata kama aliyelisema hayuko tena duniani. Badala ya kutafuta wachawi sasa hivi, mimi nafikiri wale wote ambao wanaamini kuwa Mwalimu Nyerere alitoa mchango mkubwa kwa nchi hii, watumie muda wao kutafakari kazi aliyofanya na kujumuisha fikra zake na matendo yake kupima yale ambayo bado yanaweza kuwa suluhisho dhidi ya baadhi ya changamoto zinazoikabili Tanzania sasa hivi.
“Iwapo hoja zake zina nguvu katika mazingira ya sasa, basi hazihitaji yeye mwenyewe kuzisemea. Wanaoziamini wazichambue na wazitumie kama silaha ya kupambana na upungufu ambao tunauona leo katika nyanja mbalimbali.
“Lakini pia ni muhimu kwa vijana kujitafutia elimu kuhusu hayo yaliyopita, ili kupata mifano mizuri ya uongozi ambayo iliweka masilahi ya Taifa mbele na kuzuia kabisa hizi hoja za siku hizi za kumpa kila mtu fursa ya kufanya anavyotaka. Zinazungumzwa fursa za mwananchi, lakini ukweli ni kuwa baadhi ya viongozi wanapigana vikumbo na wananchi hao hao kutafuta fursa zao binafsi,” amesema Madaraka.