Wiki hii Watanzania na watu wa mataifa mbalimbali duniani, tunafanya kumbukizi ya kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Mwalimu Nyerere ni miongoni mwa binadamu wachache ambao ni vigumu mno kuwaelezea. Tena basi, ni wachache wanaoweza kusimama na kutamba kuwa walimfahamu vilivyo.
Mara zote nimemshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijaalia fursa adhimu ya kumfahamu Mwalimu kwa kiasi kidogo. Nilipata bahati hiyo mara kadhaa kwa kumwuliza maswali mbalimbali, na yeye akanijibu. Wakati huo nikiwa mwanafunzi wa sekondari, nilimwuliza sababu zilizomfanya mwanasiasa Oscar Kambona akaikimbia nchi.
Swali langu lililenga kuupata ukweli kwani wapo waliodai Kambona alikimbia Azimio la Arusha, lakini wengine wakidai umaarufu wake ndiyo uliomfanya Mwalimu amchukie, na hivyo, ili aweze kunusuru maisha yake, akaamua kukimbilia ughaibuni Uingereza. Kwenye mfululizo huu wa kumbukizi ya Mwalimu kila mwaka, Mola akinijaalia siha njema, nitaeleza majibu ya Mwalimu.
Mwalimu alikuwa na sifa moja kuu. Alipendwa hata na maadui zake. Uwezo wake kujenga hoja uliwafanya wakubwa duniani kote, wakubali nguvu na ushawishi wake. Mwalimu alifanikiwa katika hilo kwa sababu alisimamia ‘kweli’ na ‘haki’.
Aliutumia muda wake mrefu kuwatumikia Watanzania na walimwengu wengine wenye mahitaji. Kwa Mwalimu, kilichokufa ni kiwiliwili, lakini fikra zake alizoziacha katika matendo, maandishi na sauti, zitaendelea kuishi daima. Hili linathibitishwa na wingi wa wageni wanaofika Butiama kufuatilia historia ya Mwalimu na kujifunza mengi.
Mwaka huu tunamkumbuka Mwalimu Nyerere, tukiwa na uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli.
Kumbukizi ya mwaka huu inaweza kuwa yenye kufikirisha zaidi kutokana na ukweli kwamba Rais Magufuli anaelekea kutekeleza baadhi ya mambo kwa staili ya Mwalimu.
Rais Magufuli, kama alivyokuwa Mwalimu, ameamua kwa dhati kupambana na wizi, rushwa, ufisadi, uzembe na kutowajibika miongoni mwa watumishi wa umma na wananchi.
Mwalimu Nyerere hakupendwa na Watanzania kwa sababu eti aliwaacha wafanye mambo walivyopenda. Mara kadhaa wapo waliomuona Mwalimu kama dikteta, lakini wakakubaliana naye kuwa alichokisimamia kililenga kuleta manufaa kwa Watanzania wote bila kujali rangi, hali, jinsi, kabila au kanda.
Mwalimu Nyerere aliheshimiwa na kupendwa kwa sababu alikuwa mtu mkweli ambaye kwa lugha ya leo tungeweza kusema ‘aliyaishi maneno yake’. Alipoonesha chuki dhidi ya rushwa, alifanya hivyo kwa vitendo. Hakuwahi kukemea rushwa, lakini yeye mwenyewe akawa anapokea au kutoka kwa njia za kificho.
Aliposisitiza kufanya kazi, alifanya kazi kweli. Ofisini alifanya kazi, na shambani pia alifanya kazi. Hakuwa ‘bwana mkubwa’ wa kuelekeza kwa maneno, bali kwa vitendo. Aliposisitiza upandaji miti, nyumbani na mashambani kwake kulikuwa darasa tosha la alichokihubiri kwa wananchi.
Chini ya Mwalimu Nyerere, watu waliopata msamaha wa kula bila kufanya kazi ni watoto, wazee (vikongwe na ajuza) na walemavu! Aliamini kazi ndiyo kipimo cha utu. Hili la kazi tunaliona sasa kwa Rais John Magufuli kupitia ‘Hapa Kazi Tu’.
Mwalimu Nyerere aliheshimu mno muda. Alizingatia ratiba, na ndiyo maana ilijulikana ni wakati gani anaingia na kutoka ofisini, muda gani anakwenda shambani, muda gani anapata kifungua kinywa; muda gani wa kupata mlo wa mchana au usiku, n.k. Itoshe kusema Mwalimu alikuwa kiongozi wa mfano. Rais Magufuli na timu yake ya uongozi hawapaswi kuhangaika kujua namna ya kuongoza! Wanachopaswa kufanya ni kurejea na kutekeleza kwa vitendo mfumo wa uongozi na maisha ya Mwalimu. Wapo rafiki zangu ambao huwaambia kuwa Mwalimu Nyerere ni encyclopedia ya uongozi ambayo ukiwa nayo, hupati shida!
Tukiwa tunamkumbuka Mwalimu, ni wajibu wetu kuunga mkono juhudi za Rais Magufuli, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu na viongozi wote wenye nia njema na nchi hii katika kuifikia Tanzania ambayo Mwalimu Nyerere, alitamani kuijenga.
Tanzania ya uhuru, haki, amani, upendo, mshikamano na maendeleo, ndiyo iliyokusudiwa na Mwalimu, hata akaweza kushirikiana na waasisi wenzake kujenga misingi yake.
Mwalimu alipenda Tanzania iwe nchi ya viwanda na ndiyo maana hadi anang’atuka mwaka 1985 Tanzania ilikuwa na viwanda na mashirika ya umma zaidi ya 300. Hili Rais Magufuli ameliona na sasa ameamua kwa dhati kulivalia njuga. Wajibu wetu – wananchi na wasaidizi wake – ni kuhakikisha azma hiyo inafikiwa.
Mwalimu alipinga uonevu. Hili tunaliona katika Serikali ya Awamu ya Tano. Juzi, wameoneshwa walimu-wanafunzi wakimpiga mwanafunzi kwa namna ya kusikitisha mno. Mamlaka za nchi zimechukua hatua mara moja kwa wahusika wote. Muhimu ni kuwa hicho kilichoonekana kwa walimu-wanafunzi ni tone tu katika bahari ya uonevu nchini mwetu. Imekuwa bahati mbaya tu kwa walimu. Kuna polisi wanaonea watu na kuwatia vilema vya maisha bila hatia yoyote. Kuna watendaji wa vijiji na kata ni miungu-watu. Wanaonea watu kupindukia. Wajibu wetu kama wananchi ni kuungana kuwakataa watu wa aina hiyo.
Vita dhidi ya rushwa tunaona namna inavyoendelea. Wapo waliokuwa na matumaini makubwa ya kuona vitendo hivyo vikikoma mara moja. Hawajakosea, lakini watambue kuwa mfumo wa rushwa na makosa mengine nchi mwetu ulishaota mizizi na kwa hiyo haitashangaza kuona vita hii ikichukua muda mrefu kabla ya kuonekana ushindi.
Mwalimu Nyerere aliamini njia sahihi ya kumkomboa maskini ni kuhakikisha watoto wake wanasoma. Hili tumeanza kuliona chini ya Awamu ya Tano. Watoto wanasoma bure kuanzia msingi hadi sekondari. Sasa ni wajibu wetu sote kuhakikisha kiwango cha elimu kinachotolewa kinakidhi matarajio ya ulimwengu wa leo.
Eneo jingine linalofanyiwa kazi kwa nguvu kubwa na Serikali ya sasa ni kwenye ukusanyaji mapato na matumizi ya hicho kinachokusanywa. Tulishafika mahali mtu akaona alipe au asilipe kodi! Tukapuuza ukweli kuwa ulipaji kodi si jambo la hiari. Bila kodi hakuna kitakachotekelezwa na Serikali. Wananchi nao wakiona matumizi sahihi ya kodi wanazolipa, watashawishika kulipa zaidi bila shuruti.
Tukiwa tunajiandaa kwa kumbukizi ya Mwalimu, wananchi na viongozi tujitathmini namna tunavyomuenzi kiongozi huyo.
Ilivyo sasa neno kuenzi linachukuliwa kwa wepesi tu kama msamiati wa kutimiza wajibu tu. Tujiulize, viongozi wangapi wanatekeleza kwa vitendo, badala ya maneno, yale aliyoyaamini Mwalimu? Viongozi wangapi wako tayari kubeba lawama kwa kusimamia haki katika nchi yetu?
Je, wananchi kwa upande wao wanashiriki vipi kuhakikisha wanatumia nguvu na ujuzi wao kuharakisha maendeleo ya Taifa letu? Je, nani anafanya nini katika kujenga uchumi wa Taifa letu badala ya kuketi na kulalamika kuwa Serikali haifanyi hili au haitekelezi lile? Tujiulize, nafasi yetu katika ujenzi wa Tanzania mpya ni ipi?
Tujiulize, tusipoamua sisi wenyewe kuijenga nchi yetu, waungwana wa kuifanya kazi hiyo watatoka nchi gani? Je, ulinzi wa rasilimali za nchi yetu tunaupa kipaumbele au tumeamua kuwa makuwadi wa wezi wanaokuja nchini mwetu kwa mgongo wa uwekezaji?
Mwalimu Nyerere alipenda kila mtu mwenye kufanya kazi, afanye kazi. Miaka hii 17 ya kutokuwapo kwake, inapaswa kuwa kipimo cha kujitazama kama kweli tunamuenzi kwa vitendo.
Kwa kuwa Serikali ya Awamu ya Tano kupitia kwa viongozi wetu wakuu imeonesha dhamira ya kuijenga Tanzania katika misingi na vionjo vya Mwalimu, bila shaka huko aliko anaburudika. Mwisho, nimuombe Rais Magufuli aitazame ile barabara ya Butiama. Ikiwezekana, wawekwe makandarasi wengine.
Rais Magufuli, ameonesha kuijenga Tanzania iliyokusudiwa na Mwalimu ingawa katika mazingira mapya. Maadui waliodhani baada ya kifo chake fikra zake nazo zingekufa, walikosea. Waliodhani wafuasi wake wote nao wamefariki dunia, walikosea zaidi. Tumuunge mkono Rais Magufuli kwa kuwa ameamua kumuenzi Mwalimu kwa vitendo. Hakika amewafuta machozi wafuasi wa Baba wa Taifa.
Pumzika kwa amani Mwalimu.