Mengi yameandikwa juu ya ushindi wa Joshua Nassari wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) katika Jimbo la Arumeru Mashariki. Naomba wasomaji waniruhusu nami niweze kusema japo kwa ufupi mtazamo wangu juu ya ushindi wa kijana huyo.

Nilikuwapo Arumeru Mashariki kwa wiki kadhaa wakati wa kampeni. Niliandika makala kadhaa baada ya kutoka huko. Sikusita kusema wazi kwamba Chama Cha Mapinduzi (CCM) kingeshindwa. Nilijaribu kuainisha mambo kadhaa yaliyonishawishi hadi niweze kuamini kuwa Chadema ingeshinda.Mosi, nilisema wazi kwamba kwa namna ya pekee Chadema walikuwa wamejipambanua na mahasimu wao – CCM, kwa kuendesha kampeni za kistaarabu. Niliwasikiliza Chadema wakinadi sera zao.

Walimpa mgombea wao nafasi ya kutosha ya kueleza kile kilichomsukuma kuwania nafasi hiyo, na kile Chadema walichotarajia kuwafanyia wananchi wa Arumeru Mashariki endapo wangepewa ridhaa.

Mgombea wa CCM kama kuna hotuba yake ndefu, basi ilikuwa ya dakika 10. Muda wote walizungumza wale wasioijua Arumeru Mashariki.Wakati Chadema wakijaribu kuteka hisia za wapiga kura, wenzao wa CCM walikuwa wakitamba na wahuni wao majukwaani. Waporomosha matusi.

Nilipohudhuria mikutano ya CCM sikuamini kama kweli mtu kama Lusinde alikuwa kiongozi ndani ya chama kinachotawala! Nilipomsikia Mngulu Mchemba akiporomosha matusi ya ushoga anaodai unapigiwa debe na Chadema, nikajiuliza kama kweli huyu mtu anastahili kusimama jukwaani.

Nikajisemea moyoni, “Hivi waasisi wa CCM wangekuwa hai leo wangevumilia upuuzi huu? Kwa ufupi ni kwamba viongozi hao hawafai, si kusikilizwa tu, bali hata kutazamwa. Hawana staha. Hawana tafsida. Wamekosa weledi na sifa ya kuwawezeasha kuwamo kwenye chama kinachotawala. Anayetaka kusikia matusi na upuuzi wao, aperuzi kwenye mtandao wa www.youtube. Kisha aweke Lusinde au Mchemba.Pili, nilishuhudia mikutano mingi ya Chadema ikijaa kina mama na vijana. Kwenye mikutano ya aina hii ukishaona kina mama wanajitokeza kumsikiliza mgombea, hiyo ni dalili nzuri. Kura za kina mama huwa ni za uhakika.

Hapo awali ilikuwa nadra kuwaona kina mama na watu wa makamo wakiwa kwenye mikutano ya kampeni ya vyama vya siasa tofauti na CCM. Sasa mambo ni kinyume.Nikawaona vijana wenye pikipiki wakijitokeza mikutano yote ya Chadema. Masikini hawa hawalipwi chochote. Wanajitolea wenyewe. Hawa wanaacha kusafirisha abiria ili washiriki kumnadi mgombea wanayeamini atawakomboa. Hawa walioonekana kuwa ni wahuni, leo ndiyo wanaoamua nani awe kiongozi wao! Chadema wanao wengi sana.Tatu, utaratibu wa Chadema wa kuomba wachangiwe fedha za kampeni kila mwisho wa mkutano, ulikuwa ni kama kulishana yamini. Nilistaajabu kuona katika maeneo ya vijijini kama pale Msitu wa Mbogo, Ngarenanyuki, Ngabobo watu wakichanga fedha kwa ajili ya kusaidia kampeni za Chadema.

Katika hali ya kawaida, mtu anapoamua kuchanga fedha, anakuwa amejiwekea nadhiri ya kumpigia kura huyo aliyemchangia. Kwa maneno mengine ni kwamba Chadema walifanya hivyo kama mkakati wao wa kupima imani ya wananchi juu yao. Nne, ushindi wa Chadema bila shaka yoyote ulichangiwa na uamuzi wao wa kutumia helikopta. Kwa kutumia usafiri huo, ilhali CCM wakitamba na mashangingi, wananchi waliweza kuona kuwa Chadema ni chama makini kinachostahili kupewa ridhaa ya kuongoza. Tano, wananchi wanataka mabadiliko. Wanataka mabadiliko baada ya kuona CCM imewaongoza kwa miaka mingi. Arumeru wanahangaikia ardhi na maji kwa miaka mingi kabla ya Uhuru mwaka 1961. Ikumbukwe kuwa ni Waarumeru waliokuwa wa kwanza kumtuma mjumbe wao, Kirilo Japhet, katika Umoja wa Mataifa ili awatetee dhidi ya udhalimu wa walowezi waliowapoka ardhi.

CCM kwa miaka yote, ama wameshindwa au wamepuuza kilio cha wana-Arumeru. Uchaguzi mdogo ulikuwa ndiyo uwanja wa kuwakataa na kuwajaribu Chadema kwa matarajio kwamba huenda wakatatuliwa baadhi ya kero zilizodumu kwa miaka mingi.Haikushangaza kuwaona vijana wa maeneo ya vijijini kama kule Ngabobo walikataa kabisa kuwa watiifu kwa wazee wao wa Kimasai, waliowataka waichague CCM. Ngabobo ni baadhi ya maeneo mengi ambayo CCM iliambulia aibu licha ya viongozi kama Steven Wasira kumwaga ahadi kedekede. Unapoona morani wa Kimasai wanapingana na wazee wao, ujue kuwa mabadiliko yamewadia. Baada ya kusema hayo, nirejee tena kwenye msimamo wangu wa siku zote. Msimamo wangu ni kwamba wabunge wa CCM waliopo bungeni wanatosha. Niliwaomba wananchi wa Tarime wakati ule wa uchaguzi mdogo waiangushe CCM. Kweli, walifanya hivyo.

Niliwaomba wananchi wa Igunga waipunguzie CCM nafasi ya uwakilishi bungeni, hawakuwa tayari. Nadhani mwaka 2015 watakuwa wameridhia kupata mabadiliko. CCM haichukiwi kwa muundo wala sera zake, bali kwa matendo ya baadhi ya viongozi. Chama kimepoteza mwelekeo. Kimepoteza mvuto. Watanzania wanataka mabadiliko bila kujali yanatoka ndani ya CCM au nje ya chama hicho. Kama hayatokei ndani ya CCM, wapo radhi kuyapata kutoka kwenye upinzani. Bado naamini kwa dhati kwamba kama CCM watakuwa na viongozi wanaokubalika kwa watu, imani ya wananchi kwa chama hicho itarejea. Wananchi wanachotaka kuona ni mabadiliko hata kama ni ndani ya CCM.

Swali linalojitokeza hapa ni je, nani anaweza kuyaleta mabadiliko hayo? Je, ni hawa hawa kina Lusinde na Mchemba wanaofurusha matusi kama wendawazimu? Hapana. Hawa wanazidi kuichimbia kaburi CCM. Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, alisema CCM ni dodoki. Kweli, limekusanya. Wakati bado wafuasi na wapenda mageuzi wakishangilia ushindi wa Arumeru Mashariki, Mahakama Kuu jijini Arusha kwa mara nyingine imewatia majaribuni CCM. Imetengua ubunge wa Godbless Lema.

Wito umeshatolewa wa kuwashawishi Chadema na Lema wasikate rufaa. Wafuasi wa Chadema wanaamini kuwa kukata rufaa ni kupoteza muda. Wanataka Chadema iingie tena kwenye mapambano ya kampeni kwa ajili ya kulirejesha jimbo hilo kwenye himaya yao. Kila nikitafakari, sioni ni kwa namna gani CCM watachomoka kwenye aibu nyingine ya kushindwa. Kwa ari na kiu ya Watanzania wengi ya kutaka mabadiliko, kuna dalili zote zinazoonyesha kuwa CCM itaambulia aibu katika uchaguzi mdogo wa jimbo hilo. Kama ulivyo msimamo wangu siku zote, nawaomba wananchi wa Arusha – kwa heshima na taadhima – wahakikishe upinzani unaongezewa kiti bungeni. Hii ni dua ya kila Mtanzania mpenda mageuzi.

Kuna ukweli ulio wazi kwamba pamoja na uchache wao bungeni, wabunge wa kambi ya upinzani wamefanya kazi kubwa na ya kutukuka. Sauti zao zimekuwa sauti za wanyonge. Zimekuwa sauti za kusaka haki. Zimekuwa sauti za kufukua na kudadisi ukweli. Zimekuwa sauti za kuikosoa serikali ambayo kwa miaka mingi imeendesha mambo yake kwa mazoea.Kuongeza idadi ya wabunge wa kambi ya upinzani bungeni ni kustawisha demokrasia. Kutasaidia kuongeza sauti zinazohoji, sauti zinazodadisi, sauti zinazowatetea wanyonge na sauti zinazolenga kuifanya Tanzania iwe kwa ajili ya Watanzania wote.

Tukiifanya Tanzania kuwa ni yetu sote, hakuna anayeweza kushangaa kusikia wapo wanaosali jimbo hilo na mengine yanayokuja, yaishie mikononi mwa wabunge kutoka vyama vya upinzani.Chadema wasikate rufaa. Rufaa wanayo wananchi wapigakura wa Arusha Mjini. Waziri Mkuu Mizengo Pinda juzi amejipatia matumaini. Kasema CCM haiwezi kufa! Anajidanganya. Pinda anajipa matumaini kama yale anayojipa mgonjwa anayetambua kuwa hawezi kupona. Pinda ameamua kufa kisabuni. Sabuni huendelea kutoa povu hata inaposalia kichelema!

Haitaki kukubali ukweli kwamba imekwisha. Itatoa povu hadi mwisho. Pinda ameapa kuamini CCM haifi hadi hapo atakapoona haipo madarakani. Anawapa matumaini wanachama wenzake, na zaidi anataka mwenyekiti wake aishi kwa matumaini hayo. Kifo cha CCM si jambo la mjadala. Suala ni je, itakufa lini? Pinda na waumini wa nadharia yake wakitaka kujiuliza uhai wa CCM, na wajiulize upinzani ulianzia wapi, na sasa upo wapi? Je, bado wanaamini kuwa Chadema na wengine ni vyama vya msimu? Nani leo ndani ya CCM anadiriki kusema hivyo? Moto ule ule wa Arumeru Mashariki sasa unasubiriwa Arusha Mjini.

Nimepata kusema kwamba CCM ni kama kamongo. Kamongo huendelea kupanua mdomo (kuachama) mezani, hata kama kiwiliwili chote kimeshapikwa na kuliwa. Hakuna kisichobadilika, isipokuwa mabadiliko pekee!…tamati…..@@@