Ni siku ya historia ya pekee hapa Tanzania, siku ambayo mwandishi wa habari Absalom Kibanda na mjane wa Daudi Mwangosi, Itika, wamemwaga machozi mbele ya umati wa waandishi wa habari ukumbini.
Ni siku ya kukabidhi Tuzo ya Uandishi wa Kishujaa na Utumishi Uliotukuka ya Daudi Mwangosi, Novemba 7, 2013. Siku hiyo iliandaliwa na Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC).
Ni katika Ukumbi wa mikutano wa Hoteli ya JB Belmont ya jijini Mwanza. Waandaaji na waalikwa wote katika hafla hii ni waandishi wa habari. Maelezo ya awali kuhusu tuzo hii yametolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa UTPC, Abubakar Karsan, yakifuatiwa na wimbo maalum kuhusu Mwangosi.
Daudi Mwangosi aliyekuwa Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari (IPC) mkoani Iringa, na mwandishi wa kituo cha televisheni cha Channel Ten mkoani humo, aliuawa kwa kulipuliwa na silaha ya moto, akiwa mikononi mwa askari polisi waliokuwa wakidhibiti mkusanyiko wa wananchi katika Kijiji cha Nyololo, Wilaya ya Mfindi, Iringa, Septemba 2, 2012.
Rais wa UTPC azungumza
Rais wa UTPC, Kenneth Simbaya, anasema Tuzo ya Uandishi wa Kishujaa na Utumishi Uliotukuka ya Daudi Mwangosi imeanzishwa kwa ajili ya waandishi wa habari wanaopata matatizo wakiwa wanatekeleza kazi zao za uandishi wa habari.
Tuzo hiyo itakuwa inatolewa na UTPC kila mwaka kwa waandishi waliokidhi vigezo hivyo, ikiwa ni heshima kwa Daudi Mwangosi ambaye aliipenda na kuithamini kazi yake ya uandishi wa habari kiasi cha kuifia.
“Tukio la kifo cha Mwangosi ni la kusikitisha, lakini waandishi wa habari tusikate tamaa. Wanaweza kuua watu, lakini hawawezi kuua nia na mawazo mazuri ya kupasha jamii habari,” anasema Simbaya.
Anakumbusha kwamba hali ya tasnia ya habari hapa nchini si shwari, hivyo kuna umuhimu wa waandishi wa habari kusimama pamoja katika kupigania haki ya kupata na kutoa habari kwa manufaa ya jamii nzima.
Kwa upande mwingine, Simbaya anasema jamii inapaswa kuwaunga mkono waandishi wa habari katika harakati za kupigania uhuru wa habari, kwani iko katika hatari ya kukosa habari za mambo mbalimbali yanayojiri hapa Tanzania na duniani kwa jumla.
Absalom Kibanda atwaa tuzo
Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), ambaye pia ni Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya New Habari (2006), Absalom Kibanda, ametangazwa kuwa mshindi wa kwanza wa Tuzo ya Uandishi wa Kishujaa na Utumishi Uliotukuka ya Daudi Mwangosi, mwaka huu.
Baada ya kutangazwa kuwa ndiye mshindi wa tuzo hiyo, Kibanda alipandwa na hisia zilizomlazimu kulia na kufuta machozi kwa takriban muda wa dakika tatu kabla ya kutulizwa na kusindikizwa na mke wake, Angela Semaya, kwenda kutoa shukurani mbele ya umati wa wanahabari wenzake ukumbini.
Kumwaga chozi kwa Kibanda pengine ndiko kulikosababisha mjane wa Daudi Mwangosi, Itika, naye kulia na kufuta machozi baada ya kupandwa na hisia za uchungu moyoni akikumbuka kifo cha mume wake, Daudi Mwangosi.
Baadhi ya wanahabari walijitokeza kuwafariji Kibanda na Itika. Muda mfupi baadaye wawili hao walionekana kuwa wavumilivu na kupata ujasiri wa kuzungumza mbele ya wanahabari ukumbini.
Kibanda atoa ya moyoni
Katika mazungumzo yake baada ya kutangazwa mshindi wa tuzo hiyo, Kibanda anaanza kwa kumshukuru Mungu kutokana na kumwepushia kifo.
“Ninapenda kumshukuru Mungu kwa wingi wa rehema kwa fursa hii, pamoja na machungu ya ndugu yetu Mwanghosi,” anasema Kibanda na kuipongeza UTPC kwa kuanzisha tuzo hiyo, akisema itakuwa chachu kwa mabadiliko katika tasnia ya habari na uhuru wa habari, kutoa maoni, na kadhalika.
Kibanda hakusahau kutoa shukurani zake pia kwa watu wote waliomtembelea na kumfariji kwa namna mbalimbali akiwa Hospitali ya Taifa Muhimbili na baadaye nchini Afrika Kusini, alikopata matibabu baada ya kuvamiwa na watu waliomshambulia kwa kumtesa na kumuumiza hadi kumtoboa jicho jijini Dar es Salaam, Machi 5, mwaka huu.
“Nasikitika hadi sasa hakuna mtuhumiwa wa tukio langu aliyekamatwa, na mwenendo wa kesi ya mtuhumiwa wa mauaji ya Mwangosi una maswali mengi kuliko majibu,” anasema Kibanda na kuendelea:
“Nikikumbuka kifo cha Mwangosi nasahau mateso na kuumizwa nilivyofanyiwa. Tukio langu lilihusiana moja kwa moja na kazi zangu za uandishi. Uchunguzi wa tukio langu umekuwa ukienda ndivyo sivyo.”
Mwenyekiti huyu wa TEF anasema nchi yetu imefikia hatua mbaya ambapo waandishi wa habari wanaonekana maadui mbele ya wanasiasa na viongozi mbalimbali wanaotafuta maslahi yao binafsi, huku baadhi ya waandishi wakitumika kuwafanikishia maslahi hayo.
“Kazi yetu [uandishi wa habari] ni ya hatari, lakini uhatari huo hauna sababu ya kutufanya tuwe wanyonge ila ututie chachu ya kusonga mbele,” anasema Kibanda.
Mbali ya ngao maalum, Kibanda amekabidhiwa hundi ya Sh milioni 10 kutokana na ushindi wake wa tuzo hiyo ya Mwangosi.
Lakini katika tukio ambayo halikutarajiwa, ametangaza mchanganuo wa matumizi ya fedha hizo akisema asilimia 10 ya kiasi hicho (Sh milioni moja) atatoa sadaka kwa Mungu, nusu ya Sh milioni tisa zinazosalia, yaani Sh milioni 4.5 atampatia mjane wa Mwangosi na kiasi kinachobaki atakitumia kugharimia mahitaji katika familia yake.
“Sistahili tuzo hii, asilimia kumi [ya Sh milioni 10] ninampatia aliyeokoa maisha yangu na nusu ya fedha zitakazobaki nitampatia mjane wa Mwangosi,” amesema Kibanda.
Tamko la majaji wa tuzo
Mwenyekiti wa jopo la majaji wa mshindi wa tuzo hiyo, Hamza Kasongo, anasema kwamba pamoja na mambo mengine, msingi wa uamuzi umezingatia heshima kwa Mwangosi na mwandishi wa habari aliyeonesha ujasiri katika kutetea maslahi ya umma na waandishi wa habari.
Vigezo vya tuzo hiyo ni pamoja na kuhakikisha mshindi anakuwa mwandishi wa habari Mtanzania anayefanya kazi kwenye magazeti, redio, televisheni, blogi, mitandao ya kijamii, asasi yoyote ya kihabari na mtumishi yeyote wa umma aliyeumizwa au kuuawa akiwa kazini au anatetea uhuru wa habari hapa Tanzania.
Kasongo anataja vigezo vingine vya ushindi wa tuzo hiyo kuwa ni iwapo mtu ataumizwa au kuuawa nje ya kazi kutokana na kazi zake za kihabari, atawekwa kizuizini au kufungwa jela, atanyimwa ajira kutokana na kutetea uhuru wa habari, atafanyiwa njama za kudhuriwa kimwili au kiakili kutokana na kusimamia na kutetea uhuru wa habari.
Mtambalike wa MCT anena
Akizungumza katika hafla hiyo, mwakilishi wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Pili Mtambalike, amesema Baraza hilo liko tayari kushirikiana na UTPC kuboresha mchakato wa utoaji wa tuzo za aina hiyo.
Amesema matukio ya mauaji ya waandishi wa habari duniani yameisukuma MCT kuandaa programu ya kuhakikisha usalama wa waandishi wa habari kazini hapa nchini.
“Hali si shwari, magazeti, vituo vya redio vimefungwa, waandishi wamepigwa na kuuawa,” amesema Mtambalike na kuwasisitiza waandishi wa habari na jamii kwa jumla kuungana katika kupinga sheria kandamizi dhidi ya uhuru wa habari.
Kauli ya ofisa wa SIDA
Ofisa wa Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Sweden (SIDA), Anetle Bolmewilhelm, amesema shirika hilo lilikubali kuchangia gharama za uanzishaji wa tuzo hiyo ya Mwangosi, kutokana na kuguswa na matukio kandamizi dhidi ya uhuru wa kupata na kutoa habari.
“Usalama wa waandishi wa habari lazima ulindwe, kumekuwapo na matukio hasi dhidi ya kazi za uandishi wa habari. Tunaisaidia UTPC ili kuboresha kazi za uandishi wa habari Tanzania,” amesema Bolmewilhelm na kusisitiza kuwa vyombo vya habari ndiyo sauti kuu ya jamii.
“Kujenga mazingira mazuri kwa waandishi wa habari pia ni jambo muhimu la kuzingatia,” ameongeza ofisa huyo wa SIDA.
Tido Mhando atoa msimamo
“Hata vitani wanapigana, wengine wanauawa, wengine wanasonga mbele hadi wanapata ushindi na kurudi nyumbani wakishangiliwa,” anasema mwandishi mkongwe na mahiri, Tido Mhando, aliyekuwa mgeni mwenyeji katika hafla ya kukabidhi tuzo hiyo.
Anaendelea, “Mwangosi alikuwa mwandishi mahiri, alipenda na kuthamini kazi hii hadi kifo chake, jina lake litakumbukwa kwa mazuri na heshima aliyowapatia waandishi wa habari.”
Hata hivyo, Tido ameeleza kusikitishwa na kile alichokiita juhudi kubwa zinazofanyika kukingia kifua mtuhumiwa wa mauaji ya Mwangosi na matukio mengine ya kuwapiga, kuwaharibia vitendea kazi na kuwanyanyasa waandishi wa habari akiwamo Kibanda.
“Waandishi wanaumizwa na kunyanyaswa wasifanye kazi zao vizuri. Kufungiwa kwa magazeti (baadhi ya magazeti) ni kielelezo cha mwendelezo wa juhudi hizo,” anasema Tido ambaye kwa sasa ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Mwananchi Communication.
Tido anatumia nafasi hiyo kuwaasa waandishi wa habari kutokubali kutoa mwanya wa kuchafua na kudhalilisha taaluma ya uandishi wa habari.
“Tusikubali kurubuniwa na rushwa na kutudhalilisha utu wetu. Tusikubali hata siku moja kutumiwa kwa maslahi ya wengine. Tuwe ni watu wenye hadhi ya kufanya kazi hii,” anasisitiza na kuendelea:
“UTPC wametuonesha mfano na wajibu wetu, tuwaunge mkono. Tujitume zaidi tuachane na habari za matukio na mikutano, tufuatilie habari za uchunguzi.
Wananchi wanatutegemea kama kioo chao, tuwatendee haki wananchi.” Anaongeza kuwa jamii inawategemea waandishi wa habari wafanye kazi kwa uadilifu mkubwa chini ya msingi na silaha ya umoja wao.
Sungura wa TMF apigilia msumari
Mkurugenzi wa Mfuko wa Vyombo vya Habari Tanzania (TMF), Ernest Sungura, yeye amewataka waandishi wa habari kujenga hisia za kukataa kupigwa, kuonewa, kunyanyaswa, kukandamizwa na mifumo mibaya ikiwamo inayokandamiza malipo yao.
“Tukatae mifumo mibaya [ikiwamo] inayokandamiza malipo yetu [wanahabari] kwani inatufanya wanyonge,” anasema Sungura. Anawaasa waandishi wa habari kujikita katika kuandika habari za uchunguzi na utafiti wa kina huku wakijivunia kalamu ambayo ni mithili ya silaha yao iliyo imara hata katika kulinda usalama wao.
“Sisi [waandishi wa habari] tuna silaha kubwa na nzito [kalamu]. Inawezekanaje wenye silaha nzito kama hiyo tuonewe na kuuawa?” anahoji Sungura.
Hata hivyo, Sungura anasema ukweli daima ndiyo silaha thabiti ya waandishi wa habari na kwamba uandishi wenye kuwajibika una manufaa makubwa katika jamii.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji huyo wa TMF, Tanzania haiwezi kukuza utawala bora na demokrasia ya kweli kwa kukandamiza uhuru wa vyombo vya habari.
“Tujibebe [waandishi wa habari] tuwe tayari kuufia ukweli na taaluma yetu. Tuchukue hatua ya mwendelezo wa kukataa kukandamizwa,” anasisitiza Sungura.