Katibu Mtendaji Baraza la Sanaa, Sensa ya Filamu na Utamaduni Zanzibar, Dkt. Omar Adam amesema baraza lao limeweka kibali maalum cha kusuka nywele kwa wanaume ambacho hutolewa kwa gharama ya shilingi milioni moja.
Dkt Adam ameyasema hayo akiwa kwenye mahojiano na ZBC alipokuwa akielezea maendeleo ya baraza lake na mikakati ya kuwasaidia wasanii.
“Askari wanakamata wanaume wote wanaosuka nywele kama za wasichana, Baraza la Sanaa hatupendelei hilo kwa sababu si utamaduni wetu na kuna kibali maalumu cha kusuka nywele ambacho ni milioni 1 na tumeweka bei hiyo ili kuwakomoa, sasa utachagua mwenyewe utoe milioni 1 usuke au ununue kiwembe chako cha mia moja unyoe”
Mbali na hilo Dkt Adam pia amezungumzia suala la kuzingatia maadili ambapo amepiga marufuku kucheza mziki kwa mitindo isiyofaa ikiwemo kulowesha nguo.
Aidha Dkt Adam amebainisha kuwa serikali ya Zanzibar kupitia baraza lipo mbioni kutoa tuzo kwa wasanii wake.
“Serikali ipo kwenye mipango ya kutoa tuzo za sanaa kwa wasanii wa Zanzibar na tuzo hizo zitakuja muda si mrefu, kama tunavyojua suala la utoaji tuzo lina gharama kidogo hivyo hivi sasa kuna hatua tunaendelea kuzikamilisha kwa kushirikiana na Waziri Tabia Mwita, ikiwemo za kutafuta wadhamini”