Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Kibaa
Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha mkoani Pwani imezindua rasmi kampeni ya mpango wa kutokomeza kichaa cha mbwa ambayo imeambatana na utoaji wa chanjo ikiwa ni mikakati muhimu ya kulinda afya za binadamu na wanyama.
Uzinduzi huo ambao umefanyika katika Kata ya Mtambani, ukiongozwa na Kaimu Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Halima Jongo, kwa kushirikiana na taasisi isiyo ya kiserikali TAWESO (Tanzania Animal Welfare Society).
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Jongo ameishukuru TAWESO kwa kutoa chanjo hizo bure, akisisitiza kuwa mbwa wanaodhurura mitaani wamekuwa tishio kwa usalama wa wananchi.
“Tumeona madhara makubwa yanayosababishwa na kichaa cha mbwa, ikiwa ni pamoja na vifo vya watu walioumwa na mbwa wenye ugonjwa huu. Hii si kampeni ya hiari, ni lazima wananchi wahakikishe wanyama wao wanapatiwa chanjo ili kuzuia maambukizi,” alisema.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Kibaha, Shukuru Lusanjala, amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi kuwachanja mbwa na paka wao ili kudhibiti ugonjwa huo. “Hii ni fursa muhimu kwa wananchi kuwapatiwa huduma hii bure, tunawahimiza wote wenye wanyama wa nyumbani kushiriki kikamilifu,” alieleza.
Naye Mkurugenzi wa TAWESO, Thomas Kahema, amesema mpango huo unalenga kusaidia serikali kufanikisha lengo la kutokomeza kichaa cha mbwa ifikapo mwaka 2030. “Tulipopata taarifa kuwa Kibaha kuna mbwa wengi wanaozagaa mitaani, tuliona ni muhimu kuleta huduma hii ili kuwalinda wananchi na wanyama wao,” alisema.
Evelyn Ngwila, Mkuu wa Idara ya Kilimo, Uvuvi na Mifugo, aliongeza kuwa chanjo hiyo si tu kwa mbwa bali pia kwa mifugo mingine ili kupunguza magonjwa yanayoambukiza kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu.
Baadhi ya wananchi waliojitokeza kuchanja wanyama wao, akiwemo Hassan Zuberi, wamepongeza ushirikiano kati ya serikali na mashirika yasiyo ya kiserikali kwa kuwaletea huduma hiyo karibu na makazi yao.
Kwa kuanzia, chanjo hiyo itatolewa katika Kata tatu za Mtambani, Magindu, na Soga, huku mpango wa kusambaza huduma hiyo kwa maeneo mengine ukiendelea.
