Na Mwamvua Mwinyi, JakhuriMedia, Kibaha
Halmashauri ya Mji wa Kibaha, mkoani Pwani, imeongeza mapato yake ya ndani kutoka asilimia 23 hadi asilimia 33 katika kipindi cha robo ya kwanza (Julai-30 Septemba) kwa mwaka wa fedha 2024/2025.
Aidha, halmashauri hiyo inaendelea na zoezi la uandikishaji wa wapiga kura, ikilenga kufikia asilimia 100 ifikapo Oktoba 20,2024.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha, Dkt. Rogers Shemwelekwa, wamevuka lengo la makusanyo kwa asilimia 8 ukilinganisha na kipindi kama hicho mwaka 2023/2024.
Akizungumza katika kikao cha Baraza la Madiwani, Oktoba 17, 2024, Shemwelekwa alisema lengo lilikuwa kukusanya sh.bilioni 8, ambapo katika kipindi kilichopita lengo lilikuwa sh. bilioni 7.
Kuhusu miradi ya maendeleo, hususan kwenye sekta za elimu na afya, alisema ujenzi wa Sekondari za Msangani, Tangini, na Viziwaziwa pamoja na Shule ya Msingi Tangini uko katika hatua za mwisho.
Vilevile Kituo cha Afya cha Pangani kiko tayari na kinatarajiwa kuzinduliwa Oktoba 18, mwaka huu kwa ajili ya kuanza kutoa huduma.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha, Mussa Ndomba, alibainisha kuwa hadi sasa katika zoezi la uandikishaji wa wapiga kura, kata ya Pichandege imefikia asilimia 105.3.
“Kata ya Misugusugu asilimia 100.9, Sofu asilimia 87.7, Kongowe asilimia 82, Mailmoja asilimia 71, Mkuza asilimia 42, huku kata ya Viziwaziwa ikiwa bado ipo nyuma “alieleza Ndomba.
Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Nickson Simon, alisema wilaya hiyo inaongoza kimkoa kwa kufikia asilimia 64 katika zoezi la uandikishaji wa wapiga kura.
Aliwapongeza watendaji na wataalamu kwa ushirikiano wao mzuri, ambao umewezesha ukusanyaji wa mapato kwa asilimia 125.
Awali diwani wa kata ya Pangani Agustino Mdachi aliiomba Halmashauri,iweke utaratibu wa kuajili maofisa wa mipango mji kila kata ili kuweka usimamizi mzuri kwa jamii.
Akitolea ufafanuzi suala hilo ,Mkuu wa kitengo cha mipango miji Halmashauri ya Mji, Denis Festo alibainisha, mwezi huu kata zote 14 kutakuwa na wataalam wa ardhi watakaosimamia migogoro na utekelezaji utaanza mara moja.